Maana ya Hadith


Maana ya Kilugha:
Maana ya neno hadith katika lugha ya kiarabu ni simulizi au taarifa za kweli au za kutunga, zinazohusiana na wakati uliopo au uliopita. Vile vile neno hili katika lugha lina maana ya mpya yaani kinyume cha kukuu. Neno hili limerithiwa katika lugha ya Kiswahili kama hadithi.
Maana katika Istilaah:
Hadith katika uislam ina maana ya maneno, matendo, maamuzi ya mtume (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) ikiwa ni pamoja na yote ambayo yalifanywa na kusemwa na masahaba (Allah awawie radhi) mbele yake na akayathibitisha kwa kutoyapinga au kuyakataza. Pia hadith hujumuisha maelezo kuhusu maumbile na tabia za Mtume (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ)
Matumizi ya neno Hadith katika Qur’an
Neno hadith linapatikana katika Qur’an likiwa linatumika katika maana ya kilugha na sio katika istilaah ya sayansi ya hadith. 
Mifano kutoka kwenye Qur’ani tukufu:
هَلْ أتَاكَ حَدِيثُ مُوسَى
Je! Imekufikia hadithi ya Musa? (79:15)
فَذَرْنِي وَمَن يُكَذِّبُ بِهَذَا الْحَدِيثِ سَنَسْتَدْرِجُهُم مِّنْ حَيْثُ لَا يَعْلَمُونَ
Basi niache na wanao kadhibisha hadithi hizi (yaani zilizomo katika Qur’ani)! Tutawavutia kidogo kidogo kwa mahali wasipo pajua. (68:44)

Hadith na  Sunna
Ma’ulamaa wengi hutumia maneno haya kama maneno mbadala yenye maana moja. Hata hivyo tofauti kati ya sunna na hadith ni kwamba sunna ni matendo yenyewe ambapo hadith ni masimulizi au maelezo ya matendo hayo yanayohusiana na maisha na mwenendo wa Mtume (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) au kwa kifupi hadith ni maelezo ya sunna.