Maana ya Swawm



Maana ya kilugha
Swawm imetokana na neno la kiarabu swaama ambalo ni lina maana ya kujizuilia
1 na mambo ambayo kawaida unayoyafanya kama vile kusema, kula na kunywa2. Mwenye kuyafanya haya huwa ni swaaim, yaani mwenye kujizuia. Hata Qur’an imelitumia neno hili katika maana hii ya kawaida pale Malaika alipokuwa akizungumza na Mayram, Mama yake Nabii ‘Isa alayhi salaam, Maryam aliambiwa:-
فَكُلِي وَاشْرَبِي وَقَرِّي عَيْنًا ۖ فَإِمَّا تَرَيِنَّ مِنَ الْبَشَرِ أَحَدًا فَقُولِي إِنِّي نَذَرْتُ لِلرَّحْمَٰنِ صَوْمًا فَلَنْ أُكَلِّمَ الْيَوْمَ إِنسِيًّا
Basi kula, na kunywa, na litue jicho lako. Na pindi ukimwona mtu yeyote basi sema: Hakika mimi nimeweka nadhiri kwa Ar Rahmaan ya sawm; kwa hivyo leo sitasema na mtu.3
Neno swawm kama alivyolitumia Mama Yetu Maryam, halina maana ya Swawm kama ile ya Ramadhani au ya kisheria kwa sababu mbili:-
  1. Aya hii anaamrishwa ale na anywe.
  2.  Aya hii inamalizia kwa “kwa hiyo leo sitasema na mtu” kwa swawm ya hapa kwa Bibi Maryam ni kule kujizuilia na kusema.

Maana ya Kisheria
Swam katika misingi ya kisheria, ni tendo la kumuabudu Allaah, kwa kujizuilia na yote yenye kufunguza, kama vile kula, kunywa, kufanya tendo la ndoa na kutokwa na maji ya uzazi kwa kuwa na matamanio baida ya kipindi cha kutoka jua hadi kuzama kwakwe.
4 Ingawa maana hii inaonekana kama ni kujizuia kwa sehemu mbili yaani tumbo na tupu, lakini kwa mwenye kutegemea malipo kamili ya funga basi hana budi pia kujizuia sehemu nyingine kama vile macho, ulimi masikio na viungo vingine vywa mwili.5
قَالَ الرَسُوْلُ الله صَلَّى الله عَلَيْهِ وََسَلَّم: "مَنْ لَمْ يَدَعْ قَوْلَ الزُّوْرِ وَالعََمَلَ بِهِ فَلَيْسَ لِله حَاجَةٌ فِيْ أَنْ يَدَعَ طعَامَهُ وَشَرَابَهُ" (رواه البخاري والترمذي وأبو داود وابن ماجه وأحمد)

Imetokana na Abu Hurairah (Radhi za Allaah ziwe juu yake), Amesema Mtume rehma za Allaah na amani zimshukie): “Yoyote ambaye hatoacha kauli za uwongo (chafu) pamoja na matendo, basi Allaah hana yaja ya mtu huyu kuacha kula na kunywa. (Imepokelewa na Bukhari, MuslimAbu Dawud, Ibn Majah na Ahmad)6

Yaani Allaah ta’ala hana haja ya funga ya mtu ambaye hujizuilia na kula na kunywa tu hali ya kuwa anafanya machafu mengine. Hadithi hii inathibitisha kuwa kufunga si tu kujizuiliza na kula na kunywa bali pia kuvizuia viungo vingine na machafu yote. 

Hivyo basi, swawm ni mambo matatu:-
  1. Kujizuia na vyenye kufunguza vya msingi yaani kula, kunywa na tendo la ndoa, baina ya kipindi cha kuchomoza hadi kuzama kwa jua.
  2. Kujizuia na yenye kufunguza mabayo ni machafu ya viungo vingine kama vile kusema uongo na kufanya matendo maovu.
  3. Kuzuilia moyo na akili kuelekea kwenye matamanio ya nafsi ambayo ni yenye kufunguza na bdala yake kumkumbuka Allaah ta’ala (dhikrullaah)
Ni lazima tujiepushe kuifahamu funga katika maana ile finyu ambayo ni kutokula na kunywa tu kama wanavyoieleza wasio Waislam au wasiofahamu Uislam.
1. Cowan J. M, Dictionary of Modern Written Arabic, pp 621
2. Shua’ib T. B., Essentials of Ramadhaan The Fasting Month, pp 8
3. Qur’aan, Surat Dhaariyaat, aya 55
4. Shua’ib T. B., Essentials of Ramadhaan The Fasting Month, pp 8
5. Shua’ib T. B., Essentials of Ramadhaan The Fasting Month, pp 9
6. Ibn Hajar Al Asqalani, Bulugh Al Maraam Min Adillatil Ahkaam (English Translation) (Attainment of the Objective Accroding to Evidence of the Ordinances, pp 212