Tawhid katika lugha maana yake ni kufanya kitu kuwa kimoja au kuutengeneza umoja. Asili ya neno Tawhid ni (وحد) wahhada, lenye maana ya kuunganisha au kufanya moja. Lakini kwa kawaida, katika Uislamu tunapojadili Tawhid huwa tunamaanisha Tawhidullah. Tawhidullah ina maana kuutambua na kuudumisha upweke (umoja) wa Allah (سبحنه وتعل) katika maneno, matendo na itikadi (imani) zetu zote.
Neno Tawhid halipatikani katika Qur’ani wala katika hadithi. Hata hivyo anasimulia Ibn Abbas (رضي الله عنه) kwamba Mtume (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) alipompeleka Muadh ibn Jabal (رضي الله عنه) kuwa gavana wa Yemen katika mwaka 9 Hijra alimwambia.
إِنَّكَ تَقْدَمُ عَلَى قَوْمٍ مِنْ أَهْلِ الْكِتَابِ فَلْيَكُنْ أَوَّلَ مَا تَدْعُوهُمْ إِلَى أَنْ يُوَحِّدُوا اللَّهَ تَعَالَى...
“Utakwenda kwa Ahlul kitaab, kwa hiyo la mwanzo wafundishe umoja wa Allah mtukufu (يُوَحِّدُوا اللَّهَ تَعَالَى) (Bukhari)
Hata hivyo katika Qur’ani tukufu kuna aya nyingi zenye mafunzo ya Tawhid. kwa mfano Allah (عز وجل) anasema katika suratul Baqarah:-
اللّهُ لاَ إِلَـهَ إِلاَّ هُوَ الْحَيُّ الْقَيُّومُ لاَ تَأْخُذُهُ سِنَةٌ وَلاَ نَوْمٌ لَّهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الأَرْضِ مَن ذَا الَّذِي يَشْفَعُ عِنْدَهُ إِلاَّ بِإِذْنِهِ يَعْلَمُ مَا بَيْنَ أَيْدِيهِمْ وَمَا خَلْفَهُمْ وَلاَ يُحِيطُونَ بِشَيْءٍ مِّنْ عِلْمِهِ إِلاَّ بِمَا شَاء وَسِعَ كُرْسِيُّهُ السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضَ وَلاَ يَؤُودُهُ حِفْظُهُمَا وَهُوَ الْعَلِيُّ الْعَظِيمُ
“Allah - hapana mungu ila Yeye Aliye hai, Msimamia mambo yote milele. Hashikwi na usingizi wala kulala. Ni vyake pekee vyote viliomo mbinguni na duniani. Ni nani huyo awezaye kuombea mbele yake bila ya idhini yake? Anayajua yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma yao; wala wao hawajui chochote katika vilio katika ujuzi wake, ila kwa atakalo mwenyewe. Enzi yake imetanda mbinguni na duniani; na wala haemewi na kuvilinda hivyo. Na Yeye ndiye aliye juu, na ndiye Mkuu” (2:255)
Baadhi ya dondoo muhimu katika aya hii yenye sentensi kumi kamilifu kimaana ni:-
Allah (سبحنه وتعل) ndiye Mola Muumba na Mlezi pekee na msimamizi wa mambo yote.
Allah (عز وجل) peke yake ndiye anaestahiki kuabudiwa kwa haki bila ya ushirika wa aina yoyote.
Allah (عز وجل) pekee ndiye mwenye sifa kamilifu, baadhi ya zilizotajwa katika aya hii ni “Na Yeye ndiye aliye juu, na ndiye Mkuu”, “Yeye Aliye hai, Msimamia mambo yote milele.”
Ukamilifu wa sifa zake haufanani na sifa ambazo mwenyewe Allah (سبحنه وتعل) amewapa viumbe vyake. Kwa mfano sisi binadamu tumepewa uhai lakini kwanza hatukuwepo, kisha tukahuishwa, kisha tutakufa na mwisho kufufuliwa. Kwa hiyo tuna upungufu katika uhai wetu wa namna mbili kwanza hatukuwepo kisha tutakufa. Sifa hizi pungufu hazimo katika uhai wa Allah (عز وجل) Katika aya hii kuna sifa ambazo Allah (سبحنه وتعل) hana kwa vile sifa hizo ni upungufu sifa hizo ni kama ”Hashikwi na usingizi wala kulala” hizi ni sifa za viumbe.
Mwisho kabisa ni lazima tufahamu kuwa tawhid ni somo muhimu kwa kila muislam, ni lazima tulifuatilie kwa kina kwani ukosefu wa elimu ya tawhid ni chanzo cha wengi wetu kuingia katika shirki, ambayo ni dhambi kubwa na wakati mwingine humtoa mtu kwenye Uislam.