Shukran zote zina mstahiki Allaah, Mola Mlezi wa viumbe wote. Rehma na amani zimshukie Mtume wa Allaah na watu wake na sahaba zake, pamoja na wote wenye kufuata mwenendo wake mpaka siku ya qiyamah.Uislamu ni dini ya kujitoharisha; ni dini yenye kusisitiza mno kwenye suala la usafi. Dini hii imetoa ufafanuzi wa hali ya juu kuhusu mambo yote tunayoyahitaji katika suala la twahara, Uislamu umeweka wazi juu ya kanuni zote ambazo zinamnufaisha mwanadamu katika maisha yake, hakuna ambacho ni chenye manufaa katika maisha na Uislamu umekiacha, twahara ni moja katika ya mambo yenye manufaa makubwa kwa mwanadamu ndio maana Uislamu ukasisitiza utekelezaji wake.
Twahara katika lugha maana yake ni kujisafisha/usafi. Tunapozungumza twahara katika Uislamu ni kuondoa uchafu na vyenye kuchafua, hii ni sehemu ya usafi wa kimwili au mahala au kivazi. Lakini pia twahara ina upande wa kiimani au tuseme usafi wa ki’akida. Na Allaah anatuambia katika Qur’aan:
خُذْ مِنْ أَمْوَالِهِمْ صَدَقَةً تُطَهِّرُهُمْ وَتُزَكِّيهِم بِهَا وَصَلِّ عَلَيْهِمْ ۖ إِنَّ صَلَاتَكَ سَكَنٌ لَّهُمْ ۗ وَاللَّهُ سَمِيعٌ عَلِيمٌ
Chukua sadaka katika mali zao, uwasafishe na uwatakase kwazo, na uwaombee rehema. Hakika maombi yako ni utulivu kwao. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia Mwenye kujua. [9:103]
Bila ya shaka yoyote twhar itakayotokana na swadaqa itakuwa sio twahara ya kimwili bali ni twahara ya kuitakasa mali kiimani.