Ramadhani: Salafi Swaalih na Ukarimu na Sadaka


Sadaka ndani ya mwezi mtukufu wa Ramadhani ni bora kulikoni sadaka katika miezi ya kawaida. Na ndio maana mtume "swalla llahu alayhi wasallama" akauita mwezi huu ya kwamba ni mwezi wa kuliwazana. Kwani masikini pia katika funga zao hupatwa na njaa na kiu, na mikononi mwao hawana kile kitakacho watosheleza, basi pindi wanapo patikana watu wanao wapatia sadaka na kuwafanyia ukarimu, nao hufarijika na kuliwazika. LEngo la kuwasaidia masikini hawa ni kumtii Allah ‘azza wa jall ndani ya mwezi huu mtukufu.

قَالَ رَسُوْلُ اللهِ صَلَّي اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: مَنْ فَطَرَ فِيْهِ صَائِمَا كَانَ كَفَّارَةَ لِذُنُوْبِهِ وَعِتْقَ رَقَبَتِهِ مِنَ الْنَّارِ وَكَانَ لَهُ مِنَ الْأَجَلِ مِثْلُ أَجْرِ الْصَّائِمِ مِنْ غَيْرِ أَنْ يَنْقُصَ مِنْ أَجْرِهِ شَيئَا 
سُنَنٌ الْتِّرْمِذِي
Anasema mtume rehema na amani ziwe juu yake (Yule mwenye kumfuturisha mfungaji katika mwezi huu wa Ramadhani basi kitendo chake hicho kitakuwa ni kafara ya madhambi yake. Na ataachwa huru na moto wa jahannam. Na atakuwa na malipo mfano wa malipo ya mfungaji, pasina ya kupungua malipo ya mfungaji japo kidogo)

Sunani Tirmidhiy.
Hadithi hii ni dalili tosha kuonesha ubora wa sadaka ndani ya mwezi huu mtukufu wa Ramadhani.
Matendo  mbali mbali ya kheri hupata ubora zaidi au huwa na fadhila nyingi zaidi kutokana na ubora wa mahala yanapo tendewa matendo hayo au muda ambayo hutendwa matendo hayo ya kheri. Kutokana na hivyo na ndio maana swala katika msikiti wa Maka na Madina ni bora zaidi kulikoni swala katika msikiti wowote ule، fadhila hizi ni kutokana na ubora wa maeneo haya. Vile vile swadaka katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani ni bora zaidi  kulikoni swadaka katika miezi mingine, kwani Allaah kaujaalia mwezi huu kuwa ni msimu wa kheri na kujitahidi katika utiifu na ni mwezi wa waja kuinuliwa daraja zao.
BAADHI YA MIFANO YA SALAF SWAALIH YA UKARIMU NA SADAKA KATIKA MWEZI MTUKUFU WA RAMADHANI:         
عَنْ ابْنٍ عَبَّاسٍ رَضِيَ الْلَّهُ عَنْهُمَا قَالَ: (كَانَ رَسُوْلُ اللهِ صَلَّىَ اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ أَجْوَدَ النَّاسِ بِالْخَيْرِ، وَكَانَ أَجْوَدُ مَا يَكُوْنُ فِيْ شَهْرِ رَمَضَانَ، إِنَّ جِبْرِيْلَ عَلَيْهِ الْسَّلَام كَانَ يَلْقَاهُ فِيْ كُلِّ سَنَةٍ فِيْ رَمَضَانَ حَتَّىَ يَنْسَلِخَ فَيَعْرِضُ عَلَيْهِ رَسُوْلُ اللهِ صَلَّىَ اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ الْقُرْآَنَ، فَإِذَا لَقِيَهُ جِبْرِيْلُ كَانَ رَسُوْلُ اللهِ صَلَّىَ اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ أَجْوَدُ بِالْخَيْرِ مِنَ الْرِّيحِ الْمُرْسَلَةِ) [مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ].
Imepokewa kutoka kwa Ibun Abbasi radhi za Allah ziwe juu yake na Baba yake kasema: (Alikuwa Mtume "swalla llahu alayhi wasallama" mzuri wa watu katika kheri. Na uzuri huu ulikuwa ukizidi zaidi katika mwezi mtukufu wa ramadhani. Jibril "alayhi salaam" alikuwa akimjia  Mtume kila mwaka katika mwezi wa Ramadhani kwa ajili ya kumpitisha katika Qur ani. Alikuwa mtume akikutana na Jibril ni mtu wa kheri kulikoni hata upepo uliotumwa) Mutafakun alayhi.
Ni jambo linalojulikana ya kwamba upepo huja na kheri nyingi, ikiwemo kuyasukuma mawingu na kuyapeleka sehemu mbali mbali kwa ajili ya kunyesha mvua.
Swahaba huyu anamfananisha mtume na upepo na kusema ya kwamba mtume alikuwa ni mbora kuliko hata upepo kutokana na ukarimu wake  na utoaji sadaka wake.
Al muhallab "rahimahu Llaah" anasema juu ya hadithi hii: Na katika hadithi hii tunajifunza baraka za matendo ya kheri. Na kwamba baadhi ya haya matendo hufungua milango ya matendo mengine ya kheri na humsaidia mja kufanya matendo mengine ya kheri. Huoni baraka ya funga na na kukutana na Jibril na kupitishwa Qur ani kulizidisha katika ukarimu wa Mtume na kujitolea sadaka?mpaka akawa ni mbora kulikoni hata upepo ulio tumwa?
Anasema Ibn Rajab "rahimahu Llaah” amesema imamu Shaafi"rahimahu Llaah": Inapendeza zaidi kwa watu kuzidisha ukarimu katika mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa kumuiga Mtume" rehema na amani ziwe juu yake" na kutokana na mahitaji ya watu {masikini}, pia kutokana na watu wengi kushughulishwa zaidi na funga na swala kulikoni  kazi zao.
Ukarimu huu haushii katika kutoa sadaka tu, bali ikiwezekana hata kuwakusanya masikini na kufuturu nao pamoja. Shughuli hii licha ya kupata thawabu kwa mfanyaji lakini huwa ni yenye kumuondolea mja kiburi na kujiona katika moyo wake. 
Ibn Omar "radhi za Allah ziwe juu yake na Baba yake" alikuwa akifunga na hafuturu isipokuwa pamoja na masikini. Na iwapo kama jamaa zake watawazuia masikini basi alikuwa hali usiku huo. Na alikuwa iwapo atamjia masikini anayehitaji chakula  naye anakula basi alikuwa akichukua sehemu yake ya chakula na kumpa  huyo masikini. Na anarudi anakuta jamaa zake washamaliza chakula chote kilicho kuwapo katika chombo, basi kesho yake anaunganisha swaumu hali ya kuwa usiku hakula.
Yunus bin Yaziid anasema: Alikuwa ibn Shihab pindi inapoingia Ramadhani basi kwake yeye unakuwa ni mwezi wa Qur ani na kuwalisha masikini.
Alikuwa Hamad bin Sulayman "Allaah amrehemu" Alikuwa akifuturisha katika mwezi wa Ramadhani watu mia tano. Na alikuwa akiwapatia baada ya iddi kila mmoja dirham mia moja.
Mwezi mtukufu wa Ramadhani ni msimu wa utiifu wa hali ya juu, ukarimu, sadaka na kheri mbali mbali. Na wala si mwezi wa ubakhili.
Twamuomba Allah azikubalie funga zetu, swala zetu na sadaka zetu. Allahumma aamiyn.