SALAF SWAALIH NA RAMADHAN


Assalaamu alaykum warahmatullahi wabarakaatuh.
Alhamdulillahi Rabil’aala miin, wasswalaatu wassalaamu ala Rasuuli LLahi wa’ala aalihi wasahbihi wasallama.
Baada ya kumshukuru Allaah na kumtakia rehema na amani Mtume Muhammad.
Salaf swaalih na Ramadhani, tunakusudia salaf swaalih hapa Maswahaba, Mataabi’in na Mataabi’i taabi’in: Yaani Maswahaba na wale walio fuata karne mbili baada yao.
Tunazungumzia swaumu zao ili tuweze kupata mwanga zaidi kuhusiana na funga ya mwezi mtukufu wa Ramadhani, kwani tukumbuke ya kwamba maswahaba radhi za Allaah ziwe juu yao wao waliishi na Mtume (rehma na amani juu yake), kwa hiyo bila shaka ibaada zao mbali mbali zitakuwa ni zenye kufanana sana na ibaada za Mtume kwani yeye ndiye aliye kuwa mwalimu wao. Pia tukumbuke ya kwamba miongoni mwa maswahaba  wapo ambao wamebashiriwa kuingia peponi. Vile vile katika salaf swaalih kuna walio onesha mifano mbali mbali katika ibaada ambayo hatujaiona katika zama nyingine. Na tukumbuke ya kwamba maswahaba wameridhiwa na Allah kama anavyo tueleza Mwenyezi Mungu katika kitabu chake kitukufu cha Qur’aan: 
(وَالسَّابِقُونَ الْأَوَّلُونَ مِنَ الْمُهَاجِرِينَ وَالْأَنْصَارِ وَالَّذِينَ اتَّبَعُوهُمْ بِإِحْسَانٍ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُمْ وَرَضُوا عَنْهُ وَأَعَدَّ لَهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي تَحْتَهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا ذَلِكَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ) التوبة :100
(Na wale walio tangulia, wa kwanza, katika Wahajiri na Ansari, na walio wafuata kwa wema, Allaah ameridhika nao, na wao wameridhika Naye; na     amewaandalia Bustani zipitazo mito kati yake, wadumu humo milele. Huko ndiko  kufuzu kukubwa.)   
Surat Tawba:100
Tunaelezea kuhusiana na funga za salaf swaalih kwani Mtume Muhammad rehema na amani ziwe juu yake  anasema: katika hadithi iliyosimuliwa na Abdullahi bin Masu’ud (radhi za Allah ziwe juu yao) 
عَن عَبْدِاللّه بْن مَسْعُوْد رَضِي الْلَّه عَنْهُمَا قَال: قَال رَسُوْل الْلَّه صَلَّي الْلَّه عَلَيْه وَسَلَّم  (خَيْر الْنَّاس قَرْنِي, ثُم الَّذِيْن يَلُوْنَهُم, ثُم الَّذِيْن يَلُوْنَهُم 
رَوَاه الْبُخَارِي
(Wabora katika watu ni karne yangu kisha inayo fuata kisha inayo fuata) (Bukhari)
Hadithi hii yathibitisha ya kwamba katika watu walio kuwa bora zaidi  katika umati huu ni karne aliyo ishi mtume kisha karne mbili baada yake.
Mtume Muhammad rehema na amani ziwe juu yake alikuwa pindi unapo ingia mwezi wa Ramadhani akiwabashiria maswahaba wake kheri na akisema Kama alivyosimuli Abu Hurayara radhi za Allah zimshukie:
عَن أَبِي هُرَيْرَة رَضِي الْلَّه عَنْه قَال : قَال رَسُوْل الْلَّه صَلَّى الْلَّه عَلَيْه وَسَلَّم : " أَتَاكُم شَهْر رَمَضَان ، شَهْر مُبَارَك ، فَرَض الْلَّه عَلَيْكُم صِيَامَه ، تُفْتَح فِيْه أَبْوَاب الْجَنَّة ، وَتُغْلَق فِيْه أَبْوَاب الْجَحِيْم ، وَتُغَّل فِيْه مَرَدَة الْشَّيَاطِيْن ، وَفِيْه لَيْلَة هِي خَيْر مِن أَلْف شَهْر ، مَن حَرَّم خَيْرَهَا فَقَد حُرِم ".
(Umekujieni mwezi wa Ramadhani mwezi wenye Baraka. Allaah kakufaradhishieni kufunga katika mwezi huu. Katika mwezi huu inafunguliwa milango ya mbinguni, na inafungwa milango ya motoni, na mashetani wanafungwa pia, katika mwezi huu Allaah  kaandaa usiku ambao ni bora kulikoni miezi alfu moja.Yule mwenye kuharamishiwa kheri zake hakika huyo kaharamishiwa kheri nyingi sana!)

SALAFU SWAALIH  NA QUR'ANI KATIKA MWEZI WA RAMADHAN
Qur'ani ni kitabu cha Allah kitakatifu na maneyo Yake matukufu, nacho ndio katiba yetu na mfumo wetu wa maisha. Ndani yake kuna utukufu wetu na nguvu zetu na ushindi wetu. Hatukufikia tuliko fikia katika unyonge na udhalili, isipo kuwa pindi tulipo kipa mgongo kitabu hiki kitukufu.
Anasema Allah ndani ya kitabu chake kitukufu:
لَقَدْ أَنزَلْنَا إِلَيْكُمْ كِتَابًا فِيهِ ذِكْرُكُمْ ۖ أَفَلَا تَعْقِلُونَ
الانبياء:10
(Na hakika tumekuteremshieni Kitabu ambacho ndani yake yamo makumbusho yenu {nguvu zenu,utukufu wenu} Je! Hamzingatii?
Surat Al anbiyaa:10
Mwezi wa Ramadhani una mafungamano makubwa sana na Qur’aan. Kwani Qur’aan tukufu imeshushwa ndani ya mwezi wa Ramadhani. Kama anavyo elezea Allaah ndani ya kitabu hiki:
شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِي أُنزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ هُدًى لِّلنَّاسِ وَبَيِّنَاتٍ مِّنَ الْهُدَىٰ وَالْفُرْقَانِ ۚ فَمَن شَهِدَ مِنكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ
(Mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa ndani yake Qur'aan kuwa ni uwongofu kwa watu, na ubainifu katika uongofu na upambanuzi. Basi yule atakaye ushuudia mwezi na afunge)
Surat Al baqara:185
Aya hii inathibitisha kwamba mwezi wa Ramadhani una mafungamano makubwa sana na Qur’aan tukufu. Maswahaba walikuwa wakiitilia umuhimu sana Qur’aan katika mwezi huu.
Imepokelewa ya kwamba Othmani radhi za Allah ziwe juu yake: Alikuwa akikhitimisha Qur’aan kila siku katika mwezi wa Ramadhani.
Umuhimu huu wa maswahaba juu ya Qur’aan haukuishia katika  kuisoma tu, bali walikuwa wakisoma kwa unyenyekevu na mazingatio ya hali ya juu Kwa sababu walijua ya kwamba maneno wanayoyasoma si maneno ya binadamu bali ni Manenyo ya Allaah ta’ala.
Anasimulia imamu Al Bayhakiy kutoka kwa Abi Hurayra radhi za Allah ziwe juu yake: Pindi zilipo shuka aya hizi
 أَفَمِنْ هَـٰذَا الْحَدِيثِ تَعْجَبُونَ (59)
Je! Mnayastaajabia maneno haya?
 وَتَضْحَكُونَ وَلَا تَبْكُونَ (60)
Na mnacheka, wala hamlii
النجم:59-60
Surat An-najim: 59-60
Basi As haabu suffa (Maswahaba walio kuwa wametokea maeneo mbali mbali  na hawana makaazi wakawa wakiishi msikitini) wakalia sana mpaka machozi yakawa yakitiririka katika  nyuso zao. Pindi Mtume alipo sikia kulia kwao basi nae akalia nasi tukalia kutokana na kulia kwake, kisha akasema: (Hakika Hawezi ingia motoni yule aliyelia kwa kumukhofu Allah ).
Ibn Omar radhi za Alla ziwe juu yao: Alisoma surat Al Mutwafifiin mpaka alipo fikia katika kauli yake Allah
 (يَوْمَ يَقُومُ النَّاسُ لِرَبِّ الْعَالَمِينَ)
المطففين:6
(Siku watakapo simama watu mbele ya Mola Mlezi wa walimwengu {kwaajili ya hesabu}) 
Surat Al Mutwafifiin:6

Basi akalia mpaka akadondoka, na akajizuia kwa muda ule kuendelea kusoma aya zinazo fuata.
Muzaahim bin Zufari anasimulia ya kwamba:   Sufiyaani Thauriy  rahimahu Llaah alituswalisha swala ya Magharibi.Akasoma surat  al faatiha mpaka alipo fika katika kauli yake Allaah:
إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ
الفتحة:5
(Wewe tu tunakuabudu, na Wewe tu tunakuomba msaada)
Surat Al Faatiha:5
Akalia mpaka kikakatika kisomo chake, kisha baada ya hapo akaanza  mwanzo  wa surat al faatiha.
Al as wadu bin Yaziid rahimahu Llaah alikuwa  akikhitimisha Qur’aan katika mwezi wa Ramadhani kila baada ya siku mbili, alikuwa akilala kati ya magharibi na ishaa. Na alikuwa akikhitimisha Qur’aan katika miezi mingine   kila baada ya siku sita.
Al Waliid bin Abul Malik rahimahu Llaah alikuwa akithitimisha Qur’aan kila baada ya siku tatu, na akakhitimisha katika mwezi wa Ramadhani mara kumi na saba.
Kataada rahimahu Llaah, alikuwa akikhitimisha Qur’aan kila baada ya wiki, na katika mwezi wa  Ramadhani alikuwa  akikhitimisha  kila baada ya siku tatu. Na likiingia kumi la mwisho alikuwa akikhitimisha kila siku.
Rabii bin Sulayman anasimulia ya kwamba: Alikuwa imamu Shaafi  rahimahu Llaah akikhitimisha Qur’aan katika mwezi wa Ramadhani mara sitini (yaani mara mbili kila siku, mchana mara moja na usiku mara moja) na alikuwa akikhitimisha katika miezi mingine mara thelathini kwa  mwezi.
Hii ni baadhi ya mifano tu juu ya salaf swaalih na Qur ani katika mwezi wa mtukufu wa  ramadhani.
Twamuomba Allah aturuzuku elimu yenye manufaa na matendo mema.