BISMILLAAHI RAHMAANI RAHIIM
Utangulizi wa Tafsiri ya Qur'ani
Elimu ya tafsir ya Qur’ani ni katika elimu muhimu sana. Kwani elimu hii hupelekea kufahamu maneno, matamshi na ibara za Qur ani tukufu, kujifunza hukumu mbali mbali za kisheria na kufikia malengo yaliyo kusudiwa na na Qur ani.
Maana ya tafsiri kilugha: Tafsir kama neon la kiarabu lina maana ya ubainifu na uwazi.
Na maana ya tafsiri kiistwilaah: Ni elimu ambayo makusudio yake ni kupelekea kufahamu kitabu cha Mwenyezi Mungu Mtukufu kilicho shushwa kwa Mtume wake Muhammad (rehema na amani ziwe juu yake) na kubainisha maana yake na kutoa hukumu zake na hekima zake. Au kwa kifupi ni Kubainisha maana za Qur’ani tukufu.
Elimu ya tafsiri ya Qur’ani ni katika elimu zilizoanza tokea kipindi cha Mtume Muhamadi-rehema na amani ziwe juu yake-.
Maswahaba-radhi za Allah ziwe juu yao-walikuwa wakiitilia umuhimu wa hali ya juu Qur’ani kwa kujifunza kuisoma,kufahamu maana yake na kuifanyia kazi.
Swahaba wa Mtume Ibun Masuudi (radhi za Allah ziwe juu yake) anasema:
<<Alikuwa mmoja wetu pindi anapojifunza aya kumi, havuki kwenda mbele mpaka ajue maana zake na kuzifanyia kazi.>>
Kipindi hiki mwalimu wao mkuu alikuwa ni Mtume Muhamadi (rehema na amani ziwe juu yake)
Kama anavyo tueleza Allah ndani ya kitabu chake kitukufu:
(وَأَنزَلْنَا إِلَيْكَ الذِّكْرَ لِتُبَيِّنَ لِلنَّاسِ مَا نُزِّلَ إِلَيْهِمْ وَلَعَلَّهُمْ يَتَفَكَّرُونَ)
سورة النحل:44
( Na tumekuteremshia wewe Ukumbusho {Qur’ani} ili uwabainishie watu yaliyo teremshwa kwao, huenda watapata kufikiri) Suratun Nahl:44.
Kisha baada ya hapo maswahaba ndio walio endeleza jukumu hili la kufasiri Qur’ani. Na katika hao, kuna maswahaba walio kuwa ni mashuhuri juu ya elimu hii wakiwemo makhalifa wa Mtume waongofu ambao ni Abubakari, Omari, Othmani na Ally (radhi za Allah ziwe juu yao). Vile vile ‘Abdullahi bin ‘Abasi (radhi za Allah ziwe juu yake na baba yake), na alikuwa akiitwa "Mfasiri wa Qur’ani" kutokana na umahiri wake juu ya elimu ya Qur’ani. Tukumbuke ya kwa Mtume siku moja alimuombea dua swahaba huyu kwa kusema:
اللهم فقهنا في الدين وعلمنا التأويل
(Ewe Allah mfahamishe dini na mfundishe tafsiri).
Vile vile katika maswahaba walio kuwa ni maarufu katika kufasiri Qur’ani ni Abdullahi bin Masuudi (Allah amridhie)
Na alikuwa akisema: <<Haikushuka aya katika kitabu cha Allaاh, isipokuwa ninajua imeshuka kwa ajili ya nani, na wapi imeshuka, na laiti kama ningekuwa ninajua ya kwamba kuna mtu ni mjuzi wa kitabu cha Allah kulikoni mimi, kuna uwezekano wa kumfikia kwa farasi basi ningemwendea>>
Kisha baada ya hapo wakachukua tafsiri kutoka kwa maswahaba, mataabi’ina (kizazi kilichofuatia baada ya maswahaba wakiwemo Al Hassan al Basry, Saidi bin Jubair, Ikrima mawla wa ibn Abasi na wengineo.
Hawa mataabi’ina wakawapatia wanazuoni walio kuja baada yao na maimamu na wakaandika katika vitabu mbali mbali ambavyo vimetufikia.
Katika vitabu vya tafsiri mashuhuri ni:
1:Tafsiri Twabari:
Hii ni tafsiri iliyo andikwa na Imam wa wafasiri Muhammad bin Jariir at Twabari (rahimahu Llaah). Ibn Jariir alitokea Baghdad, Iraq na alifariki mwaka 310H.
Ibn Jariir amekusanya kauli hadithi za mtume kauli za maswahaba na kauli za mataabi’i na mataabii taabi’ina.
Tafsiri hii huzingatiwa kuwa ndio marejeo ya kwanza katika tafsiri,na wafasiri walio kuja baada yake walitegemea sana kitabu hiki katika kuandika tafsiri zao.
2: Tafsiri al Qurtubi:
Tafsiri hii imeandikwa na imamu Abu abdillah Muhammad bin Ahmad al answaariy al kurtubiy (rahimahu Llaah). Alikuwa akitokea Qurtuba (Cordoba) ilioko Hispania ya leo. Alifariki mwaka 671H.
3:Tafsiri al qur’an al adhwiim.
Tafsiri hii ilitungwa na imam Ismail bin Kathiir (Allaah amrehemu), alikuwa akitoke Damascus Siria. Imam ibn Kathir alifariki mwaka wa 774H. Tafsiri ambayo ni maarufu kwa jina la “Tafsir ibn Kathir ilikuwa ni marejeo ya pili baada ya Tafsiri ya imam Twabari.
In shaa Allah makala ijayo tutazungumzia kuhusiana na aina za tafsiri.