FUNGA ZA SUNNA


Duniani ni sehemu ya kuchuma pasipo na hesabu na kesho, siku ya mwisho ni hesabu pasipo ya kuchuma. Kwa hiyo inatakiwa muumini azitumie fursa mbali mbali ili kuhakikisha ya kwamba siku ya mwisho hesabu yake mbele ya Allah anakuwa ni nyepesi.
Sasa ni mwezi mmoja na siku chache tangu kumalizika kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani, mwezi ambao tumeonja ladha za ibaada, ikiwemo ibaada ya funga.
Tukumbuke ya kwamba ibada yafunga si mwezi mtukufu wa Ramadhani na sitatush shawwaal tu bali kuna funga  nyingine ambayo  ni sunna kuzifunga na kuweza kujipatia malipo ya hali ya juu.
Mtume rehma na amani ziwe juu yake anatueleza katika hadithi Al Qudsy iliyo pokelewa na Abu Hurayra (Allah amridhie)
عَنْ أَبِيْ هُرَيْرَةَ رَضِيَ الْلَّهُ عَنْهُ قَالَ : قَالَ رَسُوْلُ الْلَّهِ - صَلَّىَ الْلَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ - إِنَّ الْلَّهَ قَالَ: مَنْ عَادَىْ لِيَ وَلِيا فَقَدْ آَذَنْتُهُ بِالْحَرْبِ ، وَمَا تَقَرَّبَ إِلَيَّ عَبْدِيَ بِشَيْءٍ أَحَبَّ إِلَيَّ مِمَّا افْتَرَضْتُ عَلَيْهِ ، وَمَا يَزَالُ عَبْدِيَ يَتَقَرَّبُ إِلَيَّ بِالْنَّوَافِلِ حَتَّىَ أُحِبَّهُ ، فَإِذَا أَحْبَبْتُهُ كُنْتُ سَمْعَهُ الَّذِيْ يَسْمَعُ بِهِ ، وَبَصَرَهُ الَّذِيْ يُبْصِرُ بِهِ ، وَيَدِهِ الَّتِيْ يَبْطِشُ بِهَا ، وَرِجْلَهُ الَّتِيْ يَمْشِيَ بِهَا ، وَإِنْ سَأَلَنِيْ لَأُعْطِيَنَّهُ ، وَلَئِنْ اسْتَعَاذَنِيْ لَأُعِيْذَنَّهُ (رَوَاهُ الْبُخَارِيُّ)
Yule atakaye mfanyia uadui walii wangu {mtu mwenye kumuamini Allah na kumcha} basi mtu huyo nimemtangazia vita. Na mja wangu hawezi jikurubisha Kwangu kwa kitu ambacho ni chenye kupendeza zaidi kwangu kulikoni kuyafanya yale ambayo nimemfaradhishia. Na mja wangu hato acha kuwa ni mwenye kujikurubisha kwangu kwa sunna mpaka ninampenda. Na nikimpenda nitakuwa ni sikio lake analo litumia katika kusikia, na jicho lake  analo litumia katika kutizama na mkono wake anao utumia katika kugusa ,na mguu wake anao utumia kutembelea, na iwapo kama  ataniomba basi nitampatia kile anacho kiomba, na iwapo kama atataka ulinzi kwangu basi nitamlinda) 
Hadithi imepokelewa na Imamu Bukhari
Hadithi hii inatujulisha ya kwamba hakuna jambo lililokuwa  muhimu zaidi na lenye ulazima kuliko yote katika kuyatekeleza yale  ambazo Allah katufaradhishia, na mja iwapo atajitahidi katika mambo ya sunna basi Allah ta’ala atampenda, na kumuwafikisha katika masikio yake, macho yake,mikono yake, miguu yake na kuwa nae na kumjibu dua zake na kumkinga na shari mbali mbali. Kwa hiyo mja huyu atakuwa haoni isipokua yale ambayo Allah anayapenda na hasikilizi isipokuwa yale ambayo Allah anayapenda n.k. Ni uzuri na ni furaha iliyoje kupendwa na Allah Muumba wa ulimwengu na vilivyomo, mlezi wa waja na mfalme wa wafalme?
Vile vile katika hadithi iliyo pokelewa na Abii Saidi-Allah amridhie-anasema:Nimemsikia mjumbe wa Allah-Rehema na amani ziwe juu yake- akisema:
عَنْ أَبِيْ سَعِيْدٍ رَضِيَ الْلَّهُ عَنْهُ قَالَ: سَمِعْتُ الْنَّبِيَّ صَلَّىَ الْلَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَقُوْلُ: (مَنْ صَامَ يَوْما فِيْ سَبِيِلِ الْلَّهِ، بَعُدَ الْلَّهُ وَجْهَهُ عَنْ الْنَّارِ سَبْعِيْنَ خَرِيْفا). وَوَاهٍ الْبُخَارِيُّ وَمُسْلِمٌ 
(Yule mwenye kufunga siku moja kwa ajili ya njia ya Allah, Allah atauweka mbali uso wake na moto muda wa miaka sabini) Hadithi imepokelewa na Bukhari na Muslimu.
Ni nani miongoni mwetu asiye tamani kuwekwa mbali na moto wa jahannam? Bila shaka hakuna.
FUNGA AMBAZO NI SUNNA
1: KUFUNGA SITA KATIKA MWEZI WA SHAWWAAL:
Siku sita hizi waweza zifunga mfululizo au kwa kupumzika.
Vile vile Unaweza zifunga mwanzoni katikati au mwisho, vyovyote vile suala muhimu ni kuzikamilisha.
Imesimuliwa kutoka kwa Abi Ayubu Al Answariy-Radhi za Allah ziwe juu yake-Hakika mjumbe wa Allah-Rehema na Amani ziwe juu yake kasema:
عَنْ أَبِيْ سَعِيْدٍ رَضِيَ الْلَّهُ عَنْهُ قَالَ: سَمِعْتُ الْنَّبِيَّ صَلَّىَ الْلَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَقُوْلُ: (مَنْ صَامَ يَوْما فِيْ سَبِيِلِ الْلَّهِ، بَعُدَ الْلَّهُ وَجْهَهُ عَنْ الْنَّارِ سَبْعِيْنَ خَرِيْفا). وَوَاهٍ الْبُخَارِيُّ وَمُسْلِمٌ 
(Mwenye kufunga Ramadhani kisha akafuatisha siku sita basi atakuwa ni kama vile kafunga mwaka mzima) Hadithi imepokelewa na Muslimu.
Atakuwa ni kama vile kafunga mwaka kivipi?
Jema moja linalipwa kwa thawabu :10
Kwa hiyo siku thelathini itakuwa ni kama ifuatavyo:
30 x10 = 300 ukijumlisha siku sita za mwezi wa shawali:
6 x 10 = 60.    
 300 + 60 = 360
Na mwaka wa kiislamu una siku 360.
2:KUFUNGA SIKU NA KUPUMZIKA SIKU:
Funga hii ni funga iliyokuwa bora zaidi katika funga za sunna.
Imepokelewa kutoka kwa Abdullahi Ibun Amru Ibun Al Aaswi-Radhi za Allah ziwe juu yake na baba yake-Hakika ya Mtume-swalla Allahu alayhi wassalama-kasema:
عَنْ عَبْدِالْلَّهِ بْنِ عَمْرِوٍ ابْنِ الْعَاصِ – رَضِيَ الْلَّهُ عَنْهُمَا– أَنَّ رَسُوْلَ الْلَّهِ صَلَّىَ الْلَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: (إِنَّ أَحَبَّ الصِّيَامِ إِلَىَ الْلَّهِ صِيَامُ دَاوُدَ . وَأُحِبُّ الصَّلَاةَ إِلَىَ الْلَّهِ صَلَاةُ دَاوُدَ . كَانَ يَنَامُ نِصْفَ الْلَّيْلِ ، وَيَقُوْمُ ثُلُثَهُ . وَيَنَامُ سُدُسَهُ . وَكَانَ يَصُوْمُ يَوْما وَيُفْطِرُ يَوْما) مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ

(Hakika funga inayo pendeza zaidi mbele ya Allah,ni funga ya nabii Dawdi-Alayhi salaamu-.Na swala inayo pendeza zaidi mbele ya Allah ni swala ya Dawdi-Alayhi salaamu-.Alikuwa akilala nusu ya usiku na kusimama[katika ibaada] theluthi yake,na analala sudusi yake[moja ya sita].Na alikuwa akifunga siku na kufuturu siku) Hadithi imepokelewa na Bukhari na Muslimu.
3:KUFUNGA SIKU TATU KATIKA KILA MWEZI:
Siku tatu hizi ni siku zinazo julikana kwa jina la Ayyaam ul baydh (masiku meupe). Siku hizi ni tarehe 13,14 na 15 katika mwezi wa kiislam ya Hijra.
Kama ilivyo simuliwa kutoka kwa Ibn Milhaan - radhi za Allah ziwe juu yake anasema:
  وَعَنْ ابْنِ مِلْحَانَ رَضِيَ الْلَّهُ عَنْهُ قَالَ:(كَانَ رَسُوْلُ الْلَّهِ صَلَّىَ الْلَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَأْمُرُنَا أَنْ نَصُوْمَ الْبِيْضَ ثَلَاثَ عَشْرَةَ وَأَرْبَعَ عَشْرَةَ وَخَمْسَ عَشْرَةَ قَالَ: وَقَالَ: هُنَّ كَهَيْئَةِ الْدَّهْرِ) رَوَاهُ أَبُوْ دَاوُدَ
(Alikuwa mtume-Rehma na Amani ziwe juu yake-Akituamrisha kufunga Al Biydh (masikku meupe) kumi na tatu, kumi na nne na kumi na tano, na akasema:masiku haya ni kama mwaka [yaani mwenye kufunga masiku haya ni kama vile kafunga mwaka/anapata thawabu za kufunga mwaka mzima])
Hadithi imepokelewa na Abu Dawdi.
Na amri iliyo pokelewa katika hadithi ni ya sunna na wala si ya ujuub (uwajibu na ulazima).
4:KUFUNGA SIKU TISA ZA MWANZO WA MWEZI WA DHUL HIJJA:
Kuanzia mwanzo mpaka siku ya tisa ambayo ndio siku ya Arafa. 
Kapokea imamu Bukhari hadithi iliyo simuliwa na Ibn Abbas - radhi za Allah ziwe juu yake -k utoka kwa mtume -rehma na amani ziwe juu yake, anasema:
رَوَىَ الْبُخَارِيُّ فِيْ صَحِيْحِهِ مِنْ حَدِيْثِ ابْنِ عَبَّاسٍ رَضِيَ الْلَّهُ عَنْهُمَا عَنْ الْنَّبِيِّ - صَلَّىَ الْلَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ - قَالَ:( مَا مِنْ أَيَّامٍ الْعَمَلُ الْصَّالِحُ فِيْهَا أَحَبُّ إِلَىَ الْلَّهِ مِنْ هَذِهِ الْأَيَّامِ -يَعْنِيْ الْأَيَّامِ الْعَشْرِ-قَالُوْا يَا رَسُوْلَ الْلَّهِ وَلَا الْجِهَادُ فِيْ سَبِيِلِ الْلَّهِ؟قَالَ وَلَا الْجِهَادُ فِيْ سَبِيِلِ الْلَّهِ إِلَّا رَجُلٌ خَرَجَ بِنَفْسِهِ وَمَالِهِ ثُمَّ لَمْ يَرْجِعْ مِنْ ذَلِكَ بِشَيْءٍ)
(Hakuna masiku ambayo matendo mema ndani yake ni yenye kupendeza zaidi mbele ya Allah kulikoni masiku haya [masiku kumi] Maswahaba wakauliza: Ewe Mtume wa Allah wala jihadi kwa ajili ya njia ya Allah? Mtume akajibu: wala jihadi kwa ajili ya njia ya Allah, isipokuwa kwa yule aliye toka na nafsi yake na mali yake kisha kikawa hakijarudi chochote katika hivyo)
Funga ni katika matendo mazuri na yenye kupendeza mbele ya Allah. Kwa hiyo ni juu ya mja kuitumia fursa  ya masiku haya kwa kufunga na kufanya amali nyingine zilizokuwa  njema na kuridhiwa mbele ya Allaah.
5:KUFUNGA SIKU YA ARAFA:
Siku ya arafa ni siku ya tisa ya mwezi wa Dhul hijja,siku ambayo mahujaji wanakuwa wamesimama katika viwanja vya arafa.Kwa yule ambaye hakushiriki katika ibaada hii ya hijja ni suna kwake kufunga siku hii.
Kapokea imamu Tirmidhiy  hadithi iliyo simuliwa na Abu Katada-Radhi za Allah ziwe juu yake-anasema:
رُوِيَ الْامَامِ الْتِّرْمِذِيُّ عَنْ أَبِيْ قَتَادَةَ الْأَنْصَارِيِّ رَضِيَ الْلَّهُ عَنْهُ أَنَّ رَسُوْلَ الْلَّهِ  سُئِلَ عَنْ صَوْمِ يَوْمِ عَرَفَةَ ، فَقَالَ : (يَكْفُرْ الْسَّنَةَ الْمَاضِيَةَ وَالْسَّنَةَ الْقَابِلَةِ)
Mtume (rehma na amani ziwe juu yake) aliulizwa juu ya funga ya siku ya arafa akajibu: (Inafuta madhambi ya mwaka ulio pita na mwaka ujao)
Na kufutiwa madhambi huku ni iwapo kama mja atakuwa kajiepusha na madhambi makubwa kama vile kuuwa, uchawi, ulevi, uzinzi na mengineyo. Kwani madhambi haya huhitaji toba maalum.
6: KUFUNGA SIKU YA ‘ASHURAA:
Siku ya ‘Ashuraa ni siku ya kumi ya mwezi wa muharram (mwezi wa kwanza wa kiislam).
Ni sunna kufunga siku hii
Imepokelewa kutoka katika Musnadi ya Imamu Ahmad-Rahimahu LLAH- ya kwamba:
  وَفِيْ مُسْنَدِ الْإِمَامِ احْمَدُ " أَنَّ الْنَّبِيَّ مَرَّ بِأُنَاسٍ مِنْ الْيَهُوْدِ قَدْ صَامُوَا يَوْمَ عَاشُوْرَاءَ فَقَالَ مَا هَذَا مِنْ الْصَّوْمِ قَالُوْا هَذَا الْيَوْمِ الَّذِيْ نَجَّى الْلَّهُ عَزَّ وَجَلَّ فِيْهِ مُوْسَىْ عَلَيْهِ الْسَّلامُ وَبَنِيَّ إِسْرَائِيْلَ مِنْ الْغَرَقِ ، وَغَرَّقَ فِيْهِ فِرْعَوْنَ ،  وَهَذَا يَوْمٌ اسْتَوَتْ فِيْهِ السَّفِيْنَةُ عَلَىَ الْجُوْدِيِّ ، فَصَامَ نُوْحٌ وَمُوَسَى عَلَيْهِمَا الْسَّلامُ شُكْرَا لِلَّهِ عَزَّ وَجَلَّ فَقَالَ الْنَّبِيُّ : "أَنَا أَحَقُّ بِمُوْسَى وَأَحَقُّ بِصَوْمٍ هَذَا الْيَوْمِ فَأَمَرَ أَصْحَابَهُ بِالْصَّوْمِ"

Hakika ya mtume (salla Allahu alayhi wasallam) Alipita kwa watu miongoni mwa Wayahudi ambao walikuwa wamefunga siku ya ‘Ashuraa. Akawauliza siku hii ina munasaba gani na funga? Wakasema: Hii ndio siku ambayo Allah ‘azza wajall alimuokoa Musa (amani iwe juu yake) Na banu Israil dhidi ya kuzama. Na akamzamisha Fir’aun. Na hii ndio siku ambayo Safina (ya nabii Nuh) ilitulia katika mlima wa Judiy. Nabii Nuhu akafunga na nabii Musa pia (Alayhima ssalaam) Kwa kumshukuru Allah ‘azza wajall. Mtume akasema: (Mimi ndio mwenye haki juu ya Musa na ndio mwenye haki ya kufunga siku hii). 
Akawaamrisha maswahaba wake kufunga. Lakini amri yenyewe si ya uwajibu bali ni ya sunna.
Vile vile imepokewa na Imamu Muslimu hadithi iliyo simuliwa na swahaba wa Mtume Abu Katada (radhiya Allah anh) kasema:
وَفِيْ صَحِيْحِ مُسْلِمٍ عَنْ أَبِىْ قَتَادَةَ أَنَّ رَجُلا سَأَلَ الْنَّبِيَّ عَنْ صِيَامِ عَاشُوْرَاءَ فَقَالَ احْتَسِبْ عَلَىَ الْلَّهِ أَنْ يُكَفِّرَ الْسَّنَةَ الَّتِيْ قَبْلَهُ
Mtu mmoja alimuuliza Mtume juu ya funga ya siku ya ‘Ashuraa. Mtume akamjibu: (Ninatarajia Allah atasamehe madhambi ya mwaka ulio pita) Iwapo kama mja atajiepusha na madhambi makubwa.
Vile vile ni bora kwa mja kufunga siku ya tisa na ya kumi au ya kumi na kumi na moja kwa ajili ya kuwakhalifu Mayahudi.Kwani mtume alisema: (Iwapo kama nitaishi mpaka mwaka ujao basi nitafunga siku ya tisa na ya kumi)
7:KUFUNGA SIKU YA JUMATATU NA ALKHAMIS:
Miongoni mwa faida za funga ni kumfanya mja kuwa mchamungu na kumpunguzia matamanio.Kwa hiyo kufunga  siku hizi na nyinginezo ni muhimu sana khususani kwa vijana ambao hawajaowa au kuolewa.
Imepokelewa kutoka katika sahihi mbili(Bukhari na Muslimu)na vitabu vingine,kutoka katika hadithi iliyo simuliwa na Ibun Masuudi-Radhiya Allahu anhu-Amesema:Kasema Mtume-Rehema na amani ziwe juu yake:
وَفِيْ الْصَّحِيْحَيْنِ وَغَيْرِهِمَا عَنْ ابْنِ مَسْعُوْدٍ رَضِيَ الْلَّهُ عَنْهُ قَالَ قَالَ رَسُوْلُ الْلَّهِ صَلَّىَ الْلَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ ( يَا مَعْشَرَ الْشَّبَابِ مَنِ اسْتَطَاعَ مِنْكُمُ الْبَاءَةَ فَلْيَتَزَوَّجْ فَإِنَّهُ أَغَضُّ لِلْبَصَرِ وَأَحْصَنُ لِلْفَرْجِ ، وَمَنْ لَمْ يَسْتَطِعْ فَعَلَيْهِ بِالْصَّوْمِ فَإِنَّهُ لَهُ وِجَاءٌ)
(Enyi vijana mwenye kuweza kuowa na aowe, kwani kuowa ni kwenye kupelekea kuhifadhi macho na kuhifadhi tupu. Na kwa yule ambaye hatoweza kuoa basi ni juu yake kufunga, hakika ya funga kwake ni kinga)
Na imesimuliwa na Abu Hurayra-Radhiya Allah anhu-amesema: Hakika ya  Mtume (salla Allahu alayhi wasallam) kasema:
وَعَنْ أَبِيْ هُرَيْرَةَ رَضِيَ الْلَّهُ عَنْهُ أَنَّ رَسُوْلَ الْلَّهِ صَلَّىَ الْلَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ (تُعْرَضُ الْأَعْمَالُ يَوْمَ الِاثْنَيْنِ وَالْخَمِيْسِ ، فَأُحِبُّ أَنْ يُعْرَضَ عَمَلِيَّ وَأَنَا صَائِمٌ) 
(Huoneshwa matendo ya waja mbele ya Allah siku ya Jumatatu na Alkhamis, kwa hiyo ninapendelea matendo yangu yaoneshwe hali ya kuwa ni mwenye kufunga).
Ni muhimu tujitahidi katika ibada hii ya funga angalau kwa kuchagua baadhi ya funga ambazo tumezitaja katika makala hii na kujifungamanisha nazo. Kwa rehma za Allaah huenda ikawa ndio sababu ya kufikiwa na hidaya kutoka kwa Allaah sub-hanahu wa ta’ala. KWani hidaya hutupelekea sisi waja kupata ushindi Duniani na akhera.