Tunamshukuru kwa dhati kabisa Allah sub-hanahu wa ta'ala kwa kutuwezesha kufika tulipo fika katika mwezi huu wa Ramadhani, pia rehma na amani zimshukie Mtume, pamoja watu wake na sahaba zake na wale wote wenye kufuata mwenendo wake mpaka siku ya qiyama. Na tunashuhudia kwamba hapana Mola anayestahiki kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allah na Muhammad ni mja na Mtume wake.
Mwezi mtukufu wa Ramadhani ndio umefikia ukingoni, wengi ni wenye huzuni kwani ingawa ni mwezi mmoja tu, wamejenga mazoea makubwa ya kufanya mambo mbali mbali ambayo hatuyapati katika miezi mingine, mikusanyiko ya pamoja katika milo ya iftaar, misikiti kujaa, itikafu, qiyamul layl na du’a za kuomba maghfira kama vile
Mwezi mtukufu wa Ramadhani ndio umefikia ukingoni, wengi ni wenye huzuni kwani ingawa ni mwezi mmoja tu, wamejenga mazoea makubwa ya kufanya mambo mbali mbali ambayo hatuyapati katika miezi mingine, mikusanyiko ya pamoja katika milo ya iftaar, misikiti kujaa, itikafu, qiyamul layl na du’a za kuomba maghfira kama vile
(اللَّهُمَّ إِنَّكَ عَفُوٌّ تُحِبُّ الْعَفْوَ فَاعْفُ عَنِّيْ)
Haya ni baadhi tu ya mambo ambayo wengine yanawatoa machozi kwani hatuna uhakika wa kuwa hai mpaka mwezi wa Ramadhani mwakani.
Wakati tukiwa na majonzi kufuatia kuondokewa na mwezi huu yaliyochanganyika na furaha ya sherehe za ‘Idil Fitwr, la muhimu zaidi ni kufanya tathmini juu ya mafanikio tuliyoyapata baada ya mwezi wa Ramadhani. Ili tuweze kufanya tathmini sahihi hatuna budi kufahamu nini tunatakiwa kukifikia baada ya Ramadhani. Tunachotakiwa kukifikia kimeelezewa kwenye Qur’ani katika aya ambayo Allaah ‘azza wa jall ametufaradhishia kufunga, Allaah ta’ala anatuambia:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُتِبَ عَلَيْكُمُ الصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ
Enyi mlio amini! Mmeandikiwa Swawm, kama waliyo andikiwa walio kuwa kabla yenu ili mpate kuwa wenye taqwa.
Kwa hiyo lengo la kufaradhishiwa swawm au funga ni kuwa na taqwa. Suala la kujiuliza ni ‘taqwa ni nini?’
Pia ni vipi tutaweza kujua kama tumefanikiwa kuongeza au kuwa na taqwa baada ya mwezi wa Ramadhani. Taqwa ni dhana yenye maana pana, lakini Ibn Abu Shaibah anasema katika Kitab Ul Imaan kwamba tabi’i Talq ibn Habib aliulizwa juu ya maana ya taqwa na alisema “Taqwa ni kufanya matendo ya utiifu kwa Allaah, kuwa na matarajio ya rehma zake”, akaendelea kusema kwamba “Taqwa ni kuacha matendo ya kumuasi Allaah kwa kutokana na kumuogopa” Hivyo kwa mukhtarasi tunaweza kusema kwamba mwenye taqwa ni mwenye kumcha Allaah, yaani kumtii Allah kwa kuwa na matarajio ya malipo mema na kutomuasi Allaah kwa kumuogopa.
Tukiwa tumepata mwangaza juu ya maana ya taqwa sasa tujaribu kuangalia mwenye taqwa anakuwa na mwenendo gani katika maisha yake ili tujue baada ya Ramadhani tumeweza kuwa na mwenendo huo, Allaah ‘azza wa jall anatuambia katika Qur’ani kwamba Qur’ani ni kitabu ambacho hakina mashaka ndani yake na ni muongozo kwa wenye taqwa.
Baada ya maelezo haya, Allaah ta’ala anatutajia baadhi ya sifa za wenye taqwa kwa kutuambia:-
الَّذِينَ يُؤْمِنُونَ بِالْغَيْبِ وَيُقِيمُونَ الصَّلَاةَ وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنفِقُونَ
Ambao huyaamini ya ghaibu na hushika Swala, na hutoa katika tuliyo wapa.
وَالَّذِينَ يُؤْمِنُونَ بِمَا أُنزِلَ إِلَيْكَ وَمَا أُنزِلَ مِن قَبْلِكَ وَبِالْآخِرَةِ هُمْ يُوقِنُونَ
Na ambao wanayaamini yaliyo teremshwa kwako, na yaliyo teremshwa kabla yako; na Akhera wana yakini nayo.
Kwa mukhtasari aya hizi zinataja sifa zifuatazo za wenye taqwa:-
1. Wanaongozwa na Qur’ani, yaani matendo na mwenendo wao wa maisha unakwenda sambamba na maamrisho ya Allaah yaliyo kwenye kitabu hichi pamoja na makatazo yake.
2. Wanaamini ghaibu, yaani yale wasioyoyaona, kwa mfano wanayo imani thabiti ya kuwepo kwa Allaah ‘azza wa jall pamoja na kwamba haonekani hapa Duniani. Wanaamini kwa yakini juu ya maamrisho ya Mtume salla Llahu ‘alayhi wa sallam japokuwa hawakukutana naye pamoja na mengineyo mengi.
3. Ni wenye kusimamisha swala, sio tu katika mwezi wa Ramadhani bali daima ni wenye kudumu kwenye ibada hii kwenye maisha yao huku swala aliyoiswali Mtume rehma na amani juu yake ikiwa ndio kigezo cha swala zao.
4. Ni wenye kutoa kutokana na walivyoruzukiwa na Allaah ta’ala, yaani ikiwa ni wenye elimu basi watawaelimisha waliowazunguka, ikiwa ni wenye mali watakuwa ni wenye kutoa sadaka kwa wingi kusaidia mafakiri na masikini na ikiwa ni wenye nguvu basi watawasaidia walio dhaifu, na hufanya hivyo kwa kificho sana isipokuwa pale inapobidi kudhihirika.
5. Wanaamini kitabu alichoteremshiwa Mtume Muhammad salla Llahu ‘alayhi wasallam, yaani Qur’ani na pia vitabu walivyoteremshiwa Mitume mingine waliotangulia kabla yake kama vile Tawrat, Zabur na Injil, na kuamini huku sio tu kwa maneno bali pia ni kwa vitendo, yaani wanayafanyia kazi yaliyomo kwenye vitabu hivyo.
6. Wanaamini juu ya akhera kwa yakini, yaani juu ya hili wao hawana mashaka yoyote, tena ni wenye uhakika kuwa watasimamishwa mbele ya Allaah ta’ala siku ya hukumu na kutakuwa na ama moto au pepo, muhimu zaidi ni kwamba wanaishi maisha yao hapa Duniani wakijitayarisha kukutana na Mola wao siku hiyo.
Hizi ni baadhi ya sifa za wenye taqwa. Hivyo basi baada ya Ramadhani ikiwa muumini atadumu katika matendo kama haya basi ni dalili kuwa amefaulu kuwa na taqwa na ikiwa ataachana na mambo haya ya kheri taratibu hata baada ya muda mchache atayaacha yote basi ni dalili ya kuwa taqwa haijamuingia na hivyo hakufikia lengo la swawm au funga ya Ramadhani.
Kuwa na taqwa kunatupelekea sisi viumbe kufikia lengo la kuumbwa kwetu, kwani tunakuwa watiifu kwa aliyetuumba, lakini baadhi ya faida za wazi kabisa za kuwa na taqwa ambazo Qur’ani imezielezea ni zifuatazo:
أُولَٰئِكَ عَلَىٰ هُدًى مِّن رَّبِّهِمْ ۖ وَأُولَٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ
Hao wapo juu ya uwongofu utokao kwa Mola wao Mlezi, na hao ndio walio fanikiwa.
Hivyo basi wenye taqwa ndiyo ambao wanapata hidaaya (muongozo) kutoka kwa Allaah, kitu ambacho sisi waislamu tunamuomba zaidi Allaah ta’ala atupe kuliko kitu chingine chochote kwa kumuomba kuongoka kila tunaposoma Suratul Fat-ha kwa kusema:
اهْدِنَا الصِّرَاطَ الْمُسْتَقِيمَ
Tuongoe njia iliyo nyooka.
Mbali na kupata kuongolewa pia Allah anatueleza katika aya hiyo hiyo kuwa wenye taqwa ndio waliopata mafanikio ya kweli kwani mioyo yao inakuwa safi hapa Duniani na wanakuwa ni wenye kutosheka na kesho akhera wana malipo makubwa na mazuri mno.
Vile vile Allah anatueleza kuhusu taqwa kuwa:
إِنَّ أَكْرَمَكُمْ عِندَ اللَّهِ أَتْقَاكُمْ
Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa Allaah ni huyo mwenye taqwa zaidi katika nyinyi.
Hivyo basi kwa vile mbora zaidi mbele ya Allaah sio tu mwenye taqwa bali ni mwenye taqwa zaidi, hatuna budi kuongeza bidii hata baada ya Ramadhani katika kufanya matendo ambayo yatatuongezea taqwa. Tunamuomba Allaah ta’ala atujaalie taqwa, atukubalie swawm zetu na ibada zetu nyingine, atusamehe makosa yetu, atuepushe na adhabu ya kaburi na atutunikie jannatul fir dawsi baada ya siku ya malipo.