Nyakati za Futari na Daku


Inshallah tunaingia katika mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani. Katika mwezi huu Waislam huwa tuna milo miwili mikubwa badala ya ile ya kawaida. futari, yaani chakula ambacho tunakila baada ya kutua kwa jua baada ya kufunga siku nzima tangu kabla ya kuchomoza kwa jua na daku, chakula tunachokila kabla ya kuingia kwa sala ya alfajiri.
Uislamu haujaacha kuhimiza na kuelekeza namna ya utekelezaji wa kila jambo ikiwemo nyakati za daku na futari. Katika suala la kufungua au kufuturu Uislam unahimiza kwamba ni muhimu kuwahi kufungua mara tu baada ya kuingia wakati, yaani mara baada ya kutua au kuzama kwa jua. Hili linathibitishwa katika hadithi iliyosahihi.


وَعَن سَهْلِ بْن سَعْدٍ رَضِيَ اللَّه عَنْهُ، أَنَّ رَسُوْلَ الْلَّه صَلَّي الْلَّه عَلَيْهِ وَسَلَّم قَال: (لَا يَزَالُ النَّاسُ مَا عَجَّلُوْا الْفِطْرَ) مُتَّفَق عَلَيْه
Amesimulia Sahl bin Sa’ad  Allaah amuwie radhi, amesema Mtume rehma na amani juu yake: “watu wataendelea kuwa na kheri iwapo wataharakisha kufungua” (Bukhari na Muslim)
Na katika riwaya ya Abu Dawud imeongezewa kwamba kwa sababu “mahahudi na manasara huchelewesha kufungua mpaka nyota zinapokitokeza”. Kwa hiyo kuwahi kufungua mara baada ya kuingia kwa wakati ni suala muhimu sana ambalo Mtume salla llahu ‘alayhi wa sallam amelihimiza sana. Vile vile ni miongoni mwa sunna za Mtume salla Llahu ‘alayhi wasallam ni kuchelewa kula daku. Hili nalo limesimuliw katika hadithi ya bwana Mtume.
عَن أَبِي ذَرِّ رَضِيَ الْلَّه عَنْهُ قَالَ: قَالَ رَسُوْلُ الْلَّه صَلَّي الْلَّه عَلَيْهِ وَسَلَّم لَا تَزَالُ أُمَّتِي بِخَيْرٍ مَا عَجَّلُو الْإِفْطَارَ وَأَخَّرُو السُّحُورَ 
Amesimuli Abu Dharr (radhi za Allaah zimshukie) Amesema Mtume (rehma na amani juu yake) Umma wangu utabaki kwenye kheri iwapo wataharakisha kwenye kufutari  na kuchelewa kula daku.
Hivyo kuchelewa kula daku ni miongoni mwa sunna za Mtume salla Llaahu ‘alayhi wa sallam. Imam Maalik anasimulia kutoka kwa Abdullahi bin Ubaya bin Abii Bakar anasema: Nimemsikia baba akisema: Tulikuwa mwezi wa Ramadhani tukitoka (msikitini)  baada ya kumaliza  Qiyamu llayl kuelekea majumbani mwetu, wakawa wafanyakazi wetu wakiharakisha  kuandaa chakula (daku) kwa kuhofia kuchomoza alfajiri.
Hivyo basi kuchelewa huko ni mpaka muda mchache kabla ya kuingia kwa sala ya Alfajiri. Hivyo basi hatuna budi kuachana na tabia ya kula daku kabla ya kulala kwani huo si mwenendo wa Mtume na salaf swaalih.

Mahimizo haya yanadhihirisha kwamba Uislamu unatutakia iabada zetu ziwe nyepesi, ibada ya funga na nyingine zote hazikuletwa kwa ajili ya kutufanyia ugumu katika maisha bali tuweze kuwa na utiifu kwa Allaah sub-hanahu wata'ala