Maana Na Masharti 8 ya Hijaab

Hijaab ni amri ya Allaah ta’ala. Allaah ta’ala amefaradhisha hijaab katika aya mbali mbali nasi tutazizungumzia mbili tu, Allah ‘azza wa jall anatufahamisha katika Surat Al Ahzaab

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ قُل لِّأَزْوَاجِكَ وَبَنَاتِكَ وَنِسَاءِ الْمُؤْمِنِينَ يُدْنِينَ عَلَيْهِنَّ مِن جَلَابِيبِهِنَّ ۚ ذَٰلِكَ أَدْنَىٰ أَن يُعْرَفْنَ فَلَا يُؤْذَيْنَ ۗ وَكَانَ اللَّهُ غَفُورًا رَّحِيمًا
Ewe Nabii! Waambie wake zako, na binti zako, na wake za Waumini wajiteremshie nguo zao (Jalaabib zao). Hivyo ni karibu zaidi kuweza kutambulikana wasiudhiwe. Na Allaah ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu. [Qur’aan, Surat Al Ahzaab,  Aya  ya 59 (33:59)]

Hivyo hijaab ni amri ya Allaah ta’ala. Neno lililotumika kama vazi kwenye aya hii ni’jalaabib’ ambalo ni wingi wa jilbaab. Jilbaab ni guo refu lenye kunin’ginia lililo pana na la nje (Cowan, J.M., Dictionary of Modern Written Arabic, uk 153.)

Ili kufahamu maana halisi ya hijaab, namna inavyotakiwa kuvaliwa na lengo lake halisi basi ni lazima tuyafahamu masharti yake kwa ukamilifu. Awali kabla ya masharti tuzungumzie lengo la hijaab: Lengo la hijaab ni mwanamke kuhifadhika na kuiepusha jamii na fitna ya zinaa. Mwanamke ajifunike atakavyojifunika iwapo kujifunika huko hakutaihifadhi jamii kutokana na fitna hii basi hijaab yaikukamilika. Yaani iwapo kujifunika kwake kutamfanya bado awe kivutio chenye kupelekea kwenye kuzini au kuikaribia zinaa basi hiyo hijaaba haikutimia lengo. 

Sasa na tuingie kwenye masharti:

1. Ifunike mwili mzima isipokuwa zile sehemu zilizoruhusiwa.

Katika kuielezea aya iliyofaradhisha hijaab (33:59) Imam Ibn Kathir ameelezea katika maelezo ya tafsiri yake kwamba, ninanukuu

أي : لا يظهرن شيئا من الزينة للأجانب إلا ما لا يمكن إخفاؤه ،
Hii ina maana wanawake hawatakiwi kuonyesha sehemu yoyote ya mapambo (sio tu mwili) kwa watu wasio mahrim wao, isipokuwa zile sehemu ambazo haziwezekani kufunikwa (mfano macho au baadhi ya wamazuoni wameeleza kuwa ni uso na viganja)

2. Isiwe ni pambo au kivutio.

Amri ya kuwa hijaab isionyeshe uzuri,  au isiwe ni pambo inapatikana kwenye surat An Nuur, Allaah (عز وجل) anatuambia:

…لَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا لِبُعُولَتِهِنَّ أَوْ آبَائِهِنَّ أَوْ آبَاءِ بُعُولَتِهِنَّ أَوْ أَبْنَائِهِنَّ أَوْ أَبْنَاءِ بُعُولَتِهِنَّ أَوْ إِخْوَانِهِنَّ أَوْ بَنِي إِخْوَانِهِنَّ أَوْ بَنِي أَخَوَاتِهِنَّ أَوْ نِسَائِهِنَّ  …
…Na waangushe shungi zao juu ya vifua vyao, wala wasionyeshe uzuri wao ila kwa waume zao, au baba zao, au baba wa waume zao, au watoto wao, au watoto wa waume zao, au kaka zao, au wana wa kaka zao, au wana wa dada zao, au wanawake wenzao… [24:1]

Hivyo ni wazi hijaab yenye mapambo au yenye kuvutio inavunja amri hii ya Allaah (عز وجل). Hali ya siku hizi ni kinyume, yaani wanawake wanapokuwa na waume zao ndio hawajipambi, lakini wanapotoka nje ambapo huonekana na wasio mahrim wao ndio hujipamba. 

3. Isiwe ni yenye kuonyesha (transparent au translucent)

يقول صلى الله عليه وسلم : "سيكون في آخر أمتي نساء كاسيات عاريات على رؤوسهن كأسنمة البخت العنوهن فإنهن ملعونات " زاد في حديث آخر :"لا يدخلن الجنة ولا يجدن ريحها وإن ريحها لتوجد من مسيرة كذا وكذا  رواه مسلم من رواية أبي هريرة .
Amesema Mtume (صلي الله عليه وسلم)  katika siku za mwisho za umma kutakuwa na wanawake ambao wamevaa lakini wapo utupu, vichwani mwao watakuwa na vitu mfano wa nundu ya ngamia (yaani jinsi watakavyozifunga nywele zao), walaanini kwani wamelaaniwa na katika hadithi nyingine “hawataingia peponi or hata kusikia harufu yake wakati harufu yake itasikika kwa masafa kadhaa wa kadhaa (marefu) [Imenakiliwa na Muslim katika riwaya ya Abuu Huraira]

Katika kuifafanua hadithi hii hasa yale maneno wamevaa lakini wako utupu imeelezwa:
قال ابن عبد البر :  أراد صلى الله عليه وسلم النساء اللواتي يلبسن من الثياب الشيء الخفيف الذي يصف لا يستر فهن كاسيات بالاسم عاريات في الحقيقة . نقله السيوطي في تنوير الحوالك (3/103)
Amesema  ibn Abul Barr alichokimaanisha  Mtume (صلي الله عليه وسلم)  ni kuwa .wanawake ambao wamevaa nguo ambazo ni za kitambaa chepesi au hazistiri inavyotakiwa. Wamevaa lakini wako utupu. [as-Suyuti katika Tanwiyr al-Hawaalik, 3/103.]

Kwanza kabisa hadithi hii imetudhihirishia kuwa wanawake ambao hawavai hijabu ipasavyo basi wamelaaniwa na Mtume (صلي الله عليه وسلم)  ametumrisha tuwalaani. huu ndio uzito wa kuidharau au kuiacha hijaab, na mwenye kulaaniwa basi maskani yake ni motoni. Dalili kubwa za wanawake hawa ni mbili:

Hijaab zao hazitowastiri (wamevaa lakini wako utupu)
Nywele zao zitatengenezwa au kusukwa kwa mitingo yenye kuzinyanyua kama nundu ya ngamia.
Haya hoye siku hizi tunayaona usiku na mchana, tena wanawake hawa hata wasi wasi hawana wanapofanya jambo hili lenye kupelekea wao kupata laana.


4. Isiwe ni yenye kubana na kufuata sehemu yoyote ya umbo

Turudie tena kuwa lengo la hijaab ni kuepusha fitna kwa hiyo iwapo nguo inabana au kuonyesha maumbile basi baso ni yenye kuleta fitna hivyo haitimizi lengo la hijaab. Hivyo hijaab iwe ni nguo ambayo haitoi taswira ya maumbile ya mwanamke kwa ukubwa au udogo wa sehemu yoyote.

Usama ibn Zayd amesema Mtume (صلي الله عليه وسلم)  amenipa guo la Kimasri kama zawadi ambayo alipewa na Duhya al Kalbi, nikampa mke wangu aivae. Akasema [Mtume (صلي الله عليه وسلم)] Mbona sikuoni kulivaa lile guo la Kimasri? Akasema (Usama) nimempa mke wangu alivae. Akasema [Mtume (صلي الله عليه وسلم)] akasema Mwambie avalie nguo nyingine kwani nakhofia huenda ikaonyesha maumbile yake ukubwa wa mifupa [Imesimuliwa na al-Diyaa’ al-Maqdisi katika al-Ahaadeeth al-Mukhtaarah, 1/442, na Ahmad pamoja na al-Bayhaqi, na isnaad yake ni hasan)

Hivyo ni wazi kuwa usia wa Mtume (صلي الله عليه وسلم)  katika riwaya hii ni ushahidi wa kutosha kuwa haifai nguo kuwa ni yenye kubana au kuonyesha umbo.  

5. Isitiwe manukato wala kufukizwa

Kuna hadithi nyingi za Mtume (صلي الله عليه وسلم)  zinazokataza wanawake kujitia manukato wanapotoka nje. Tutanukuu baadhi ambazo zina isnaad zilizo sahihi:

عن أبي موسى الأشعري قال : قال رسول الله صلى الله عليه وسلم :"أيما امرأة استعطرت فمرت على قوم ليجدوا من ريحها فهي زانية "
Abuu Musa al Ash’ari amesema: Kasema Mtume (صلي الله عليه وسلم)  mwanamke yoyte anayejitia manukato na kupita mbele za watu basi ni mzinifu.

عن زينب الثقفية أن النبي صلى الله عليه وسلم قال : " إذا خرجت إحداكن إلى المسجد فلا تقربن طيبا ".
Zaynab ath Thaqafiya ameripoti kwamba Mtume (صلي الله عليه وسلم)  amesema: Yoyote kati yenu enyi wanawake anapokwenda msikitini basi asiguse manukato.

أبي هريرة قال : قال رسول الله صلى الله عليه وسلم : " أيما امرأة أصابت بخورا فلا تشهد معنا العشاء الآخرة " .
Abu Hurayra amesema: Kasema Mtume (صلي الله عليه وسلم): Mwanamke yoyote aliyejifukiza basi asije kusali nasi sala ya ‘Isha. 

Hivyo katazo la kujifukiza lipo kwenye nguo na hata mwili pale mwanamke anapotoka nje. Kujifukiza na kujitia manukato kunasihi pale mwanamke anapotaraji kukutana na mume wake na sio walio haramu kwake.

6. Isifanane na mavazi ya kiume

Kuna hadithi kadhaa ambazo zinathibitisha kwamba mwanamke anapovaa kujifananisha na mwanamme basi mwanamke huyo amelaaniwa, na pia mwanamme anayejifananisha kimavazi na mwanamke pia nae amelaniwa:
عن أبي هريرة قال:" لعن رسول الله صلى الله عليه وسلم الرجل يلبس لبسة المرأة، والمرأة تلبس لبسة الرجل" .
Abu Hurayra (Allah amuwie radhi) amesema, Mtume (صلي الله عليه وسلم)  amemlaani mwanamume anayevaa nguo za kike na mwanamke anayevaa nguo za kiume.

عن عبد الله بن عمرو قال: سمعت رسول الله صلى الله عليه وسلم يقول" ليس منا من تشبه بالرجال من النساء، ولا من تشبه بالنساء من الرجال" .
Amesema Abdullah ibn ‘Amr: Nimemsikia Mtume (صلي الله عليه وسلم)  akisema; “Si miongoni mwetu wanawake wenye kujifananisha na wanaume na wanaume wanaojifananisha na wanawake.


7. Isifanane na mavazi ya wanawake wa kikafiri

Sharia ya kiislamu inaeleza wazi kuwa waislamu wanawake na wanaume wasijifananishe au kuwaiga makafiri katika ibada, sherehe na mavazi yao.Hii ni kanuni muhimu lakini kwa bahati mbaya siku hizi inapuuzwa wa waislamu wengi. Hali hii inatokana na waislamu kutokuwa na elimu, kufuata matakwa ya nafsi zao, au kuacha kuifuata dini. Lakini huchngiwa zaidi na waislamu kujichanganya na mila ambazo kwa asili ni mila za kikafiri hasa wa bara la Ulaya na Amerika. 

Uislamu ni dini iliyokamilika, laiti ingelikuwa dini iliyokosa mila yake wenyewe basi isingelikuwa ni dini liyokamilika, katika kuufikia ukamilifu huo, Allaah (عز وجل) ametuamrisha katika Qur’aan kuhusu mila kwamba:

 بَلْ مِلَّةَ إِبْرَاهِيمَ حَنِيفًا ۖ وَمَا كَانَ مِنَ الْمُشْرِكِينَ 
…Bali tunashika mila ya Ibrahim mwongofu, wala hakuwa katika washirikina. [2:135]

Bila ya shaka tutakuwa ni wenye kukubaliana kuwa hakuna mavazi ni sehemu ya mila.Tena aya hii inamalizia kuwa Ibrahim hakuwa katika washirikina katika mila yake. Hivyo basi bila ya shaka yoyote ikiwa sisi ni wenye kumfuata baba yetu Ibrahim Mtume (عليه سلم) hatuna budi kuifuata mila yake ya uongofu ilijitenganisha na mila za kikafiri.

Kufuata mila za kikafiri ni moja kati ya sababu ya umma wa Waislamu leo kuwa ni umma dhaifu, kwani kufuata mila za kikafiri kumewafanya waislamu kuwa ni watumwa wa kifikra. Hili halitoondoshwa kwetu mpaka tutakapozibadili nafsi zetu. Kwani Allaah (عز وجل) anatuambia kwamba katika kitabu chake kitukufu:
…إِنَّ اللَّـهَ لَا يُغَيِّرُ مَا بِقَوْمٍ حَتَّىٰ يُغَيِّرُوا مَا بِأَنفُسِهِمْ…
…Hakika Mwenyezi Mungu habadili yaliyoko kwa watu mpaka wabadili wao yaliyomo naf- sini mwao… [13:11]

8. Isiwe ni nguo ya kujifakharisha au kujionyesha 

Kujifakhari si hulka miongoni mwa hulka za kiislamu kwani Allaah (عز وجل) ameweka wazi kwenye Qur’aan kuwa Yeye si mwenye kuwapenda kila wenye kupenda kujifalharisha, pale alipotueleza kwenye surat al Luqmaan:
إِنَّ اللَّـهَ لَا يُحِبُّ كُلَّ مُخْتَالٍ فَخُورٍ
Hakika Mwenyezi Mungu hampendi kila anaye jivuna na kujifakhirisha. [31:18]

Hivyo nguo za kufakharisha na kujivuna si nguo ambazo zinaendana na mila na desturi za kiislamu, kwame muislamu haifai kuvaa kwa lengo la kutafuta kujifakharisha kwani kujifakharisha ni kwenye kumchukiza Allaah (عز وجل). Pia tunafunzwa na Mtume (صلي الله عليه وسلم)  juu ya mavazi ya kifakhari kwamba:

فلحديث ابن عمر رضي الله عنه قال: قال رسول الله صلى الله عليه وسلم " من لبس ثوب شهرة في الدنيا ألبسه الله ثوب مذلة يوم القيامة ثم ألهب فيه ناراً

Amesimulia Ibn Umar (رضي الله عنهم): Amesema Mtume (صلي الله عليه وسلم)  kwamba: “Yoyote atakaevaa kwa ajili ya umaarufu na fakhari ya Dunia, Allaah atamvalisha guo la kumdhalilisha siku ya qiyama, na atamfanyia moto utakaomzunguka”