Siku 10 ambazo Allaah anapenda matendo mema

Shukrani zote zinamstahiki Allah na rehma na amani zimshukie Mtume Muhammad, watu wake, na masahaba wake na wale wote wenye kufuata mwenendo wake mpaka siku ya qiyama. 

Dhul Hijjah ni mwezi miongoni mwa miezi ya Allah, ni mwezi ambao una ibada muhimu kabisa, ambayo ni nguzo ya tano ya kiislamu isiyopatikana katika mwezi mwengine wowote. Mbali na ibada ya hijjah, siku kumi za mwanzo katika mwezi huu ni siku maalum, ni siku zenye fadhila kubwa, kama inavyonukuliwa katika hadithi iliyosimuliwa na Ibn Abbaas:

عن ابن عباس رضي الله عنهما، أن النبي صلى الله عليه وسلم قال: ((مَا مِنْ أَيَّامٍ الْعَمَلُ الصَّالِحُ فِيهَا أَحَبُّ إِلَى اللَّهِ مِنْ هَذِهِ الْأَيَّامِ)) يَعْنِي أَيَّامَ الْعَشْرِ قَالُوا:  يَا رَسُولَ اللَّهِ وَلَا الْجِهَادُ فِي سَبِيلِ اللَّهِ؟  قَالَ: ((وَلَا الْجِهَادُ فِي سَبِيلِ اللَّهِ إِلَّا رَجُلٌ خَرَجَ بِنَفْسِهِ وَمَالِهِ فَلَمْ يَرْجِعْ مِنْ ذَلِكَ بِشَيْ)) البخاري

Imetoka kwa Ibn Abbaas (radhi za Allah zimshukie) kwamba Mjumbe wa Allaah amesema: <<Hakuna siku ambazo vitendo vyake vyema Anavipenda Allaah kama siku kumi hizi>> (siku kumi za mwanzo wa mwezi wa Dhul-Hijjah) Akaulizwa, je, hata Jihaad katika njia ya Allaah? Akajibu (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ((Hata Jihaad katika njia ya Allaah isipokuwa mtu aliyekwenda na nafsi yake na mali yake ikawa hakurudi na kimojawapo)) [Al-Bukhaariy].

Hivyo basi Allaah ta’ala anapendezewa sana na ibada zifanywazo katika siku kumi za Dhul Hijjah, Mtume (rehma na amani juu yake) amezipa ubora ibada zifanywazo katika siku kumi hizi kuliko hata jihaad, ukiondoa yule ambaye amekufa shahid na pia metumia mali zake kwa ajili ya jihaad. Tukizingatia wengi miongoni mwetu hatukupata bahati ya kuwa katika jihaad, basi siku kumi hizi hatuna budi kufanya juhudi kubwa katika utekelezaji wa ibada. 

Allaah ‘azza wa jall amezipia siku kumi hizi katika surat al Fajr, pale Allah alopotuambia:
وَالْفَجْرِ 
وَلَيَالٍ عَشْرٍ 
Naapa kwa Alfajiri
Na kwa masiku kumi (Al-Fajr: 1-2)
Hivyo kwa kuziapia siku hizi, Allah ‘azza wa jall amezitukuza. Pia mbali na ibada ya Hijjah katika siku kumi hizi kunapatikana siku ya ‘Arafa, ambayo ni ya tisa ya mwezi wa Dhul Hijjah. Kufunga katika siku tisa za mwanzo za mwezi wa Dhul Hijjah ni sunna miongoni mwa sunna kubwa za mwezi huu. 

وعن هنيدة بن خالد عن امرأته عن بعض أزواج النبي صلى الله عليه وسلم قالت : ( كان رسول الله صلى الله عليه وسلم يصوم تسع ذي الحجة ويوم عاشوراء وثلاثة أيام من كل شهر أول اثنين من الشهر وخميسين ) رواه الإمام أحم ، وصححه الألباني 

Kutoka kwa Hunaydah ibn Khaalid aliyesimulia kutoka kwa mkewe ya kwamba mmoja kati ya wake za Mtume amesema: << Mtume rehma na amani juu yake alikuwa akifunga siku tisa za Dhul Hijjah na siku ya ‘Ashura na siku tatu za kila mwezi, na Jumatatu ya mwanzo na Alkhamisi mbili (Imesimuliwa na Imam Ahmad na Imam Albani amesema kuwa ni hadithi sahihi)

Hivyo basi kwa wale ambao hawakujaaliwa kwenda Hijjah kufunga siku tisa za mwanzo ni ibada ambayo imesunniwa. Pia tukumbuke kuwa ni haram kufunga siku ya ‘Idi. Kwa ibada zaidi za kutekeleza katika mwezi huu fuata link hii siku 10 za mwezi wa Dhul Hijjah, tunamalizia kwa kukumbusha tena maneno ya Mtume (rehma na amani juu yake kwamba “Hakuna siku ambazo vitendo vyake vyema Anavipenda Allaah kama siku kumi hizi”