Shukrani zote zinamstahiki Allah, rehma na amani zimshukie Mtume (ﷺ), ali zake na masahaba wake pamoja na wote wenye kufuata mwenendo wake mpaka siku ya qiyama.
Leo ni siku ya mwanzo kati aya siku tatu za Tashriq. Yaani tarehe 11, 12 na 13 za mwezi wa Dhul Hijjah. Siku hizi ni ziku zenye uzito mkubwa kwa vile zimetajwa katika Qur’aan Majiyd pale Allaah (عز وجل) alipotuambia:
وَٱذْكُرُوا۟ ٱللَّـهَ فِىٓ أَيَّامٍ مَّعْدُودَٰتٍ ۚ …
Na mdhukuruni (mtajeni) Allah katika zile siku zinazo hisabiwa. [2:203]
Maulamaa ni wenye kukubaliana kuwa siku za zinazohisabiwa (ayyaman ma’duuudaat) zilizokusudiwa katika aya hii ni siku za Tashriq ikiwa ni pamoja na siku ya Idi ya tarehe 10 Dhul Hijjah. Imam Ibn Kathir katika maelezo yake ya aya hii ameeleza kuwa Ayaamin Ma’dudaat kuwa siku ya ‘Idi pamoja na siku za Tashriq na kasema huo ndio msimamo wa Ibn Umar, Ibn Az- Zubayr, Abu Musa, Ata, Mujahid, Ikrimah, Sa`id bin Jubayr, Abu Malik, Ibrahim An-Nakhai, Yahya bin Abu Kathir, Al-Hasan, Qatadah, As-Suddi, Az-Zuhri, Ar-Rabi bin Anas, Ad-Dahhak, Muqatil bin Hayyan, Ata Al- Khurasani, Malik bin Anas [radhi za Allah ziwashukie] na wengineo
عَنِ ابْنِ عُمَرَ ـ رضى الله عنهما ـ قَالاَ لَمْ يُرَخَّصْ فِي أَيَّامِ التَّشْرِيقِ أَنْ يُصَمْنَ، إِلاَّ لِمَنْ لَمْ يَجِدِ الْهَدْىَ
Kutoka kwa ibn Umar (radhi za Allah ziwashukie) amesema hakun alaiyeruhusiwa kufunga siku za tashriq isipokuwa wale waisokuwa na uwezo wa hadi (kujincha) [Sahihi Bukhari, Mjeledi wa 30, Hadithi ya 103]
Hivyo basi yoyote ambaye amechinja, awe ni hujaji au si hujaji siku hizi haruhusiwi kufunga kabisa. Amenukuliwa tena Mtume (ﷺ) katika hadithi iliyopokelewa na ‘Uqba bin Aamir akisema:
يَوْمُ عَرَفَةَ وَيَوْمُ النَّحْرِ وَأَيَّامُ التَّشْرِيقِ عِيدُنَا أَهْلَ الإِسْلاَمِ وَهِيَ أَيَّامُ أَكْلٍ وَشُرْبٍ
Siku ya Arafa na siku ya Nahr na Siku za Tashriq ni ‘Idi (sikukuu) kwetu sisi Watu wa Uislamu (waislamu) Nazo ni siku za kula na kunywa. [Jami` at-Tirmidhi, Mjeledi wa 8, Hadithi ya 92]
Ama kwa siku ya Arafa ni kufunga siku hiyo sunna miongoni mwa sunna kubwa kwa watu ambao hawakusimama Arafa siku hiyo, yaani wale wasio mahujjaaj. Naye Bishri bin Suhaim (رضي الله عنه) amesema Mtume (ﷺ) khutbah katika siku za Tashriq na kusema:
لاَ يَدْخُلُ الْجَنَّةَ إِلاَّ نَفْسٌ مُسْلِمَةٌ وَإِنَّ هَذِهِ الأَيَّامَ أَيَّامُ أَكْلٍ وَشُرْبٍ
Hatoingia yoyote peponi isipokuwa aliye Muislamu na hakika ya siku hizi ni siku za kula na kunywa. [Sunnan Ibn Majah, Mlango wa Siyam, Hadithi ya 1791]
Hivyo basi hadithi zote hizi zimeweka wazi kuwa siku hizi si siku za kufunga. Ni siku za ’Idi ambazo tunapaswa kula na kunywa huku kama ilivyoamrisha aya tuliyoinukuu mwanzo tukimdhukuru Allah kwa wingi mno.
Tumdhukuru vipi Allah katika Siku hizi?
Tunashukuru mkwa kuleta wingi wa takbiri kila baada ya Sala. Na pia kuongeza takbir hizi kwa wingi katika nyakati mbali mbali katika siku hizi
Tuzishukuru neema za Allaah kila tunapokula na kunywa, hivyo kuleta wingi wa Tahmiyd. (yaani kusema Alhamdulillah), na pia kuendelea kumshukuru Allaah (عز وجل) katika nyakati mbali mbali ndani ya siku hizi.
Na kila namna ambayo itaashiria kumdhukuru Allaah (عز وجل) zaidi basi huu ni wakati wa kufanya kwa wingi mno.
Allah ndiye mjuzi zaidi