YAA UKHTA HAARUN!


UTANGULIZI
Shukrani zote zinamsatahiki Mwenyezi Mungu Mola mlezi wa viumbe wote, Rehma na amani zimshukie Mtume Muhammad na ali zake na Sahaba zake pamoja na wote wenye kufuata mwenendo wake mpaka siku ya mwisho.
Wenye kuipinga Qur’aan hutoa madai kuhusu aya hii kwamba: Qur'aan inamwita Maryam Ukhta Haarun (Dada yake Haarun) wakati watu wawili hawa hawakuishi wakati mmoja, yaani wamepishana miaka takriban 2000. Kwa hiyo Qur’aan imefanya kosa la Kihistoria.

Lengo la makala hii ni kuthibitisha kuwa Qur’an hapa haikufanya kosa bali wenye madai haya ama hufanya makusudi kwa lengo la kupotosha ukweli au hawakuelewa aya hii.
UFAFANUZI
Mwenyezi Mungu anatuambia katika Qur’aan tukufu aya ya 19:28 ninanukuu

يَا أُخْتَ هَارُونَ مَا كَانَ أَبُوكِ امْرَأَ سَوْءٍ وَمَا كَانَتْ أُمُّكِ بَغِيًّا 
Ewe dada yake Haarun! Baba yako hakuwa mtu muovu, wala mama yako hakuwa kahaba.
Aya hii ilikuwa ni jibu kwa Mayahudi wa Jerusalem wakati huo ambao walimsingizia mwanamke mkamilifu kuliko wanawake wote, yaani Maryam Bint Imraan (‘alayha salam) kuwa ni mzinifu kutokana na ujauzito wa kimiujiza wa Isa Bin Maryam (Amani iwe juu yake), ambaye ni Mtume wa Mwenyezi Mungu. Bila ya shaka ilikuwa ni faraja kubwa kwa Maryam kwamba Mwenyezi Mungu mwenyewe kamtakasa (kamsafisha kutokana na madai ya uongo), na sio katakaswa yeye tu, bali hata wazazi wake walikuwa ni watu wema, wakweli na wacha Mungu, na pia inshallah tutaona huko mbele kuwa kwa kumwita Ukhta Haarun hata uzao (lineage) wake unatakaswa.
Historia imethibiti kwamba Maryam na Haarun ni watu walioshi katika nyakati tofauti, wakiwa Duniani hawakuwahi kukutana. Kwa hiyo undugu kwa maana ya kawaida hauwezekani kuwepo baina yao. Lakini inshallah pia tutathibitisha kuwa kuna sababu nzito zilizopelekea Qur’aan kumwita Maryam dada yake Haarun.
Kwanza ni nani Haarun na Nani Maryam? 
Maryam kama tulivyosema hapo awali ni Mama yake Issa, anatokana na ukoo wa ‘Al Imraan, Qur’aan umeutaja kuwa ni ukoo wenye daraja kubwa (pamoja na ukoo wa Ibrahim) kisha Qur’aan imemtaja Maryam kuwa ni mwanamke aliyetakaswa kisha akatoharishwa na kuwa ni mwanamke bora kuliko wanawake wote Duniani.

Kwa upande wa Haarun ('alayhi salam), yeye alikuwa kaka yake Musa('alayhi salam), wote wawili walikuwa ni Mitume  walisaidiana katika “vita” dhidi ya Fir’aun na alipokufa Musa, yeye aliendeleza kazi ya kujaribu kuwaongoa Bani Israil na alipokufa kazi yake iliendelezwa na Yu’sha Bin Noon (amani ya imshukie) ambaye nae alikuwa Mtume aliyetajwa kwenye hadithi, Ni muhimu kuzingatia kutokana na maelezo nitakayotoa mbele kuwa Haarun alikuwa ni mkubwa kuliko Musa.
Mada
Mada kuu ni kwa nini Qur’aan inamwita Maryam dada yake Haarun wakati sio tu hawakazaliwa pamoja lakini pia wameishi nyakati tofauti kabisa. 

Qur’aan imebadili mambo mengi ikiwa ni pamoja na maana ya maneno katika lugha ya kiarabu. Kwa mfano kabla ya kuja kwa Mtume Muhammad (salla Llahu 'alayhi wasallam) kwa Waarabu neno 'Swalaah' (sala) ilikuwa na maana sawa na 'Du'aa', yaani maombi yoyote kwa Mwenyezi Mungu. Baada ya Uislamu wa Ummati Muhammad kuanza neno Swalaah (sala) katika lugha ya kiarabu likabadilika maana na kuwa ni ibada maalum inayotanguliwa na nia na kuanza kwa takbir ya kuhirimia na kuishia na salam. Ndani yake ina rakaa kadhaa (kulingana na sala ipi unayosali yaani alfajiri, alasiri, isha n.k) na kila rakaa ina rukuu na sujudu mbili, pia ina tasibhi mbali mbali, Surat Al Fat-ha na sura nyingine.

Kwa hiyo leo ukimuambia muarabu, kwa maana katika suala la kilugha Du'aa (anaelewa ni maombi ya aina yoyote kwa Mungu) na “Swalaah” anajua maana yake ni hiyo nilioeleza hapo juu.

Neno kaka au dada [akhi kwa mwanamme na  ukhta au ukht kwa mwanamke] limeandikwa katika Qur’aan kiasi mara 57, hii ni kuonesha namna gani Qur’aan inasisitiza sana katika suala la undugu. Sasa undugu wa ajabu zaidi ya ule undugu wa Harun na Maryam upo sehemu mbili:

UNDUGU KATIKA DINI
Qur’aan 49:10
إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ إِخْوَةٌ فَأَصْلِحُوا بَيْنَ أَخَوَيْكُمْ ۚ وَاتَّقُوا اللَّهَ لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ

Hakika Waumini ni ndugu, basi patanisheni baina ya ndugu zenu, na mcheni Mwenyezi Mungu ili mrehemewe.
Sasa kama Tunashangaa kuwa Maryam ni dada yake Haarun, nadhani Tutashangaa zaidi kuwa hata Shith (‘alayhi salam) ambaye ni mtoto wa Nabii Adam ('alayhi salam) ni ndugu wa Muhammad (rehma na amani juu yake) kwa vile waumini wowote ni ndugu.
Kwa hiyo undugu wa Haarun na Maryam ni undugu wa kiislamu na sio undugu wa damu, ushahidi ndio huo kuwa waislamu wote ni ndugu, ni kama vile kwenye mijadala ya mlinganyo wa kidini (hasa katika lugha ya kiingereza) Mayahudi na Waarabu huitwa cousins) kutokana na Ismail na Is-haaq. Au tukumbuke pale Mtume Muhammad (rehma na amani juu yake) alipowaita Ma-answari “Enyi watoto wa Isma’il” kwa vile makabila ya Ma-answari yaani Al Aus na Al Khazraj yanatokana na kizazi cha Is’mail (‘alayhi salam).
Kwa hiyo katika Uislamu kuna undugu wa aina mbili:
1. Undugu katika Dini  (ushahidi ni aya 49:10)
2. Undugu wa kuzaliwa. 
Undugu wa Dini katika Uislam ni muhimu na bora zaidi kuliko undugu wa damu. Ndio maana waislamu huwa tunaitana akhii au ukhti wakati mwingi tunapozungumza hata kama hamjuani ili mradi nyote ni waislamu. 
UNDUGU WA UZAO (LINEAGE)
Hiyo ndio sababu ya Msingi na ya kwanza, Pili katika Uislamu tunaamini kuwa Mitume yote ina lineage moja (yaani ni ndugu wa kuzaliwa kwa mlolongo wa wazazi) Ndio maana Mayahudi wanajaribu sana kumkataa kataa Isma’il kwa sababu wanajua kuwa wakukibali kuwa Ismail nae ni mcha Mungu na pia ni kizazi "halali" cha Nabii Ibrahim ('alayhi salam) kutakuwa hakuna sababu ya kumkataa Muhammad katika suala la uzao, pia hujaribu kukataa kwamba jangwa aliloachwa Ismail na mama yake Hajira sio Makkah. Lakini bahati mbaya hata Biblia imeitaja Makka kwa dalili nyingi tu kuwa ndio jangwa alilowachwa Isma’il, nimegusia masuala haya ili tujue kuwa wasomi katika Dunia ya leo wanalifahamu hilo.

Kwa hiyo sasa kwa vile Qur’aan ilikuwa inataja walivyotakasika wazazi wa Maryam pia imejaribu kutoa mwangaza (hint) kwamba kutakasika kwa lineage ya Maryam kumeanzia kwenye ukoo wa Haarun, sio tu Baba na Mama. Kwa hiyo mpaka hapa tunapata kwamba undugu wenyewe ni wa Kiislamu na sababu ya kutajwa kwa Haarun ni kutakasika kwa uzao wake kutoka vizazi vya nyuma, sasa hakutajwa Musa 
('alayhi salam) kwa sababu Haarun ni mkubwa wake wa kuzaliwa, pamoja na kwamba Musa alipewa utume mwanzo  na pia utume wa Musa ulikuwa na hadhi ya juu kwa sababu yeye ni rusul (amepewa kitabu ambacho ni Tawraat) na kaka yake alikuwa ni Nabii tu.

Kwa hiyo kimantiki ameingia Haarun kuonesha namna kutakasika kwa Maryam kulivyoanzia mbali mno sio tu kwa Baba na Mama, sasa kwa nini iwe Haarun?

KWA NINI HAARUN?
Mayahudi wa wakati huo walokuwa wanajifanya kwamba wao ni wenye kufuata taurati, tena wanampenda sana Musa, kwa hiyo wanatajiwa Haarun kwa vile Huyo ni kaka yake Musa, yaani wanakumbushwa kwamba kama nyinyi kweli mnamfuata Musa basi na huyu nae ni dada yake kiukoo (uzao), kwa nini mumsingizie uzinifu? 
Kwa hiyo sasa naamini tunapata picha kwa nini Qur’aan inamwita Maryam Binti ‘Imraan, Ukhta Haarun! Lakini pamoja na yote hayo maskini mayahudi waliendelea kumkataa Issa na kumsingizia uzinifu Maryam!

UTUKUFU WA UZAO KWA MAYAHUDI NA WAARABU
Tatu: Qur’aan inamtaja Maryam kama ukhta Haarun kwa vile makabila mawili ambayo ni Binamu (Bin ‘ammi), Waarabu na Mayahudi wana tabia ya kutafuta utukufu kwa kufuata ukoo. Kwa hiyo kwa mfano miongoni mwao ni jambo lililozoeleka kuitana kwa mfano Yaa Ukhta Tamim kwa mwanamke anayetokana na ukoo wa Bani Tamim au Yaa Ukhta Mudar kwa mwanamke aliyetokanana na kabila la Mudari. Hivyo kiukweli kwa waarabu na Mayahudi hili si jambo la kushangaza ila kwa sisi waswahili ambao hatujui hata majina ya vizazi vitano katika koo zetu ni lazima tushangae. Nikumbushe tena kuwa Mtume salla Llahu ‘alayhi wasallam aliwahi kuwaita Al Aus na Al Khazraj watoto “Enyi watoto wa Is’mail.
HITIMISHO
Hizo ndio sababu tatu kuu na za msingi kwa Qur’aan kumwita Maryam ukhta Haarun. Maneno kama haya ya kukumbusha undugu si jambo geni katika Qur’aan, kwa mfano Mussa alipomkamata Haarun akiwa na Hasira baada ya kurudi akitoka kuchukua amri kumi na kuwakuta Mayahudi wakiabudu sanamu la mnyama lililotengenezwa na As Saamirii, Harun alimwita mdogo wake Yaa Ibn Ummi, Yaani Ewe mtoto ya Mama yangu, akijaribu kutuliza hasira za Musa kwa kutumia undugu, kweli kabisa kauli ile ilimrudishia upole Musa. Hizi si miongoni mwa busara na hulka za kiswahili kwa hiyo sisi huwa tunapata taabu kuelewa mambo kama haya, lakini ni busara zilizotumika na kunakiliwa katika Qur’aan tukufu. Na Allah ndiye mjuzi zaidi.