MWAKA MPYA WA KIISLAMU(1433)


Tarehe 26/11/11 ni siku inayoafikiana na  tarehe moja  ya mwezi Muharram, yaani mwezi wa kwanza wa kiislamu, kwa hiyo tumeingia mwaka mpya wa kiislamu.Tumetoka katika Mwaka wa 1432 na tumeingia 1433.
Idadi ya miaka hii ni tokea kuhama kwa mtume kutoka Makka na kuelekea Madina. Bila shaka kuna mazingatio makubwa sana juu ya kuhama Huku kwa mtume, mazingatio ambayo tutayazungumzia InshaaAllah.
Waislamu hatuna sherehe maalumu ndani ya siku hii inayo tambulika kisheria tokea enzi za mtume, masahaba zake na mpaka hivi sasa. Bali siku hii huadhimishwa kwa kukumbuka kipindi hiki ambayo baada yake uislamu ulipata dola ya kujitegemea na waislamu kuwa na uhuru wa kufanya watakavyo tofauti  na kipindi walichokuwa Makkah. Yaani dola ya Uislamu wa umma huu wa Mtume Muhammad ilianza tarehe 1/1/1 Hijria baada ya Waislamu kuhamia Madinah.
Vile vile tukio hili latuzindua  Juu ya suala zima la wakati. Kwani kadiri miaka inavyosonga mbele ndivyo umri wetu unavyo zidi isha na hivyo kuukaribia umauti, tofauti na watu wa mila nyingine ambayo wao hudhani kuwa hii ni siku wa kufanyiwa sherehe. Waislamu kwetu hii ni siku wa kutafakari juu ya tunchozidi kukikaribia, yaani mauti.
Vile vile tukio hili latukumbusha fadhila za Allah juu yetu kwa kutuweka hai mpaka muda huu, kwani ndugu zetu wangapi tulikuwa nao na hivi sasa hatupo nao? Na wao kabla ya kufika siku yao hawakuwa wakitarajia kuwa leo wasingekuwa na sisi.
Je tumetoa fidia yoyote kwa Allah ta'ala mpaka katuacha hai hadi hivi sasa? Bila shaka hizi ni katika fadhila za Allah juu yetu, fadhila ambazo hatuna budi kumshukuru Allah kwa kufuata muongozo wake na kujiepusha na kumuasi. Vile vile hii ni fusra kwetu sisi kutubia juu ya madhambi tuliyo yatanguliza na kuanza ukurasa mpya na Allah 'azza wa jall.
Anasema Ibun Masu'ud radhi za Allah ziwe juu yake:
(ما ندمت على شيء ندمي على يوم غربت شمسه، نقص فيه أجلي، ولم يزدد فيه عملي)
(Sijawahi kusikitika juu ya kitu kulikoni masikitiko yangu juu ya siku ambayo limezama jua lake, umepungua umri wangu, na wala matendo yangu hayajazidi) 

Na anasema Abu  al Hasan  al Basriy (Allah amrehemu):
 (يا ابن آدم إنما أنت أيام  معدودة  إذا ذهب يوم ذهب بعضك)
(Ewe binadamu hakika wewe ni siku  zenye kuhesabika, pindi inapo ondoka siku basi juwa wazi ya kwamba imeondoka sehemu yako [katika muda wako wa kuishi]).

Haya ndugu zanguni hii ni fursa nyingine katika umri wetu, tuitumie vilivyo fursa hii na wala tusiichezee. Kwani hatujui  iwapo kama mwaka mwingine tutakuwa bado tupo hai.

Ewe Allah tuwafikishe katika yale unayo yapenda na kuyaridhia.