SALAFU SWAALIH NA QIYAMU LLAYL KATIKA MWEZI WA RAMADHAN


Qiyamu llayl (kisimamo cha usiku/ibada za usiku) ni desturi ya watu wema, na  ni biashara ya waumini na Mola wao,  na ni katika matendo ya watu wenye kufuzu. Kwani Qiyamu llayli ni katika ibada zenye kuongeza imani ya mja na kumthibitisha  katika njia ya haki dhidi ya mitihani, maswaibu na misukosuko mbali mbali, anayo pambana nayo  katika maisha haya. Anasema Allah ndani ya kitabu chake kitukufu:
يَا أَيُّهَا الْمُزَّمِّلُ
Ewe uliye jifunika!
قُمِ اللَّيْلَ إِلَّا قَلِيلًا
Kesha usiku kucha, ila kidogo tu!
نِّصْفَهُ أَوِ انقُصْ مِنْهُ قَلِيلًا
Nusu yake, au ipunguze kidogo.
أَوْ زِدْ عَلَيْهِ وَرَتِّلِ الْقُرْآنَ تَرْتِيلًا
Au izidishe - na soma Qur'ani kwa utaratibu na utungo.
إِنَّا سَنُلْقِي عَلَيْكَ قَوْلًا ثَقِيلًا
Hakika Sisi tutakuteremshia kauli nzito. (73:1-5)
Muzzammil 1-5
Tutateremsha katika moyo wa muumini huyu kauli nzito. Kauli yenye kumthibitisha muumini juu ya njia ya haki dhidi ya mitihani, maswaibu na misukosuko  mbali mbali.
Na katika hadithi iliyo pokelewa na Sahli bin Saadi radhi za Allah ziwe juu yake ana sema:Hakika mjumbe wa Allah rehema na amani ziwe juu yake anasema: 
عَنْ سَهْلِ بْنِ سَعْدٍ رَضِيَ الْلَّهُ عَنْهُ أَنَّ رَسُوْلَ الْلَّهِ صَلَّىَ الْلَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ : «أَتَانِيَ جِبْرِيْلُ فَقَالَ: يَا مُحَمَّدُ ! عُشّ مَا شِئْتَ فَإِنَّكَ مَيِّتٌ وَأَحْبِبْ مَنْ شِئْتَ فَإِنَّكَ مُفَارِقَهُ وَاعْمَلْ مَا شِئْتَ فَإِنَّكَ مَجْزِيٌّ بِهِ وَاعْلَمْ أَنَّ شَرَفَ الْمُؤْمِنِ قِيَامُهُ بِالْلَّيْلِ وَعِزُّهُ اسْتِغْنَاؤُهُ عَنِ الْنَّاسِ» رَوَاهُ الْحَاكِمُ وَالْبَيْهَقِيُّ
(Alinijia Jibriil  alayhi salaam akasema: Ewe Muhammad! Ishi utakavyo lakini jua ya kwamba wewe ni maiti. Na mpende umtakaye lakini tambua ipo siku utafarikiana nae. Na tenda utakavyo lakini jua ya kwamba hakika wewe ni mwenye kulipwa. Na elewa  ya kwamba heshima  ya muumini ni Qiyamu llayl (ibada za usiku). Na utukufu wake ni kujitosheleza na watu)
Na makusudio ya Qiyamu llayli ni kuukidhi usiku au nusu yake au japo saa moja kwa kuswali, kusoma Qur ani kumdhukuru Allah na mfano wa ibada hizo. Kwa hiyo Tahajudi, Witiri, Taraaweh ni katika Qiyamu llayl.
Na kwa anaye simama kiasi cha usiku na wala si usiku wote basi yapendelewa zaidi kutekeleza ibada hii baada ya kulala kiasi,kwani kwa kufanya hivyo hupelekea akili yake kupumzika na moyo kutulia  hivyo kupelekea mazingatio zaidi katika ibada aifanyayo .Na ndio maana Allah akasema:
إِنَّ نَاشِئَةَ اللَّيْلِ هِيَ أَشَدُّ وَطْئًا وَأَقْوَمُ قِيلًا
(Hakika kuamka usiku kunawafikiana zaidi na moyo, na maneno yake yanatua zaidi (73:6)
Yaani kwa mtu aliye lala kabla ya kusimama katika ibada hii ya usiku basi kupumzika kwake huku hupelekea kauli yake kuwafikiana na moyo wake. Yaani anakuwa katika ibada yake ni mwenye kukizingatia na kukitafakari kile anacho kitamka. Si kwamba anakuwa anatamka kingine na anafikiria kingine kabisa: Kwa mfano anasoma Surat al Faatiha anafikiria kesho kazini itakuwaje? Na kutokana na umakini huu ndio maana tumeona    mifano ya baadhi ya maubbaadi (wenye kufanya ibada) walikuwa wakisimama usiku mzima kwa aya moja. Kama ilivyo pokelewa kutoka kwa muabudiaji   aliye simama usiku mzima na aya hii:
أَمْ حَسِبَ الَّذِينَ اجْتَرَحُوا السَّيِّئَاتِ أَن نَّجْعَلَهُمْ كَالَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ سَوَاءً مَّحْيَاهُمْ وَمَمَاتُهُمْ ۚ سَاءَ مَا يَحْكُمُونَ
(Je! Wanadhani wanao tenda maovu kuwa tutawafanya kama walio amini, na wakatenda mema, sawa sawa uhai wao na kufa kwao? Ni hukumu mbaya wanayo ihukumu!)
Surat Al Jaathiya: 21

BAADHI YA MIFANO YA SALAF SWAALIH NA   QIYAMU LLAYL KATIKA MWEZI MTUKUFU WA RAMADHAN
Imamu Maaliki anasimulia kutoka kwa Abdullahi bin Ubaya bin Abii Bakar anasema: Nimemsikia baba akisema: Tulikuwa mwezi wa Ramadhani tukitoka (msikitini)  baada ya kumaliza  Qiyamu llayl kuelekea majumbani mwetu, wakawa wafanyakazi wetu wakiharakisha  kuandaa chakula (daku) kwa kuhofia kuchomoza alfajiri.
Bila shaka hadithi hii inaonesha ni jinsi gani walivyo kuwa wakirefusha  ibada ya qiyamu llayl, mpaka wanatoka misikitini karibia na kuchomoza alfajiri.
Na imesimuliwa kutoka kwa Dawd bin Huswayn kutoka kwa Abdulrahman kasema: Walikuwa  maimamu wakiswalisha na mfano wa Surat al Baqarah, katika rakaa nane. Na iwapo kama baadhi ya maimamu wataswalisha kwa mfano wa urefu wa Suurat al Baqarah katika rakaa kumi na mbili basi basi nawahisi  wamewafanyia takhfifu.
Subuhaana LLAH !!! Tukumbuke ya kwamba suurat al baqara ina juzuu mbili karibia na nusu,kwa hiyo maimamu hawa walikuwa wakiswalisha katika rakaa nane na surat al baqara au mfano wake  kwa urefu wa kisomo (kwani hakuna sura ndefu zaidi ya al Baqarah) na baadhi ya maimamu walikuwa wakiswalisha rakaa kumi na mbili kwa sura hii au mfano wake.
Nafii rehema na amani ziwe juu yake anasema: Alikuwa Ibn ‘Umar  (Allaah amridhie yeye na baba yake) akiswali ibada za usiku katika mwezi wa Ramadhan nyumbani kwake. Watu wakisha ondoka msikitini basi alikuwa akichukua chombo chake cha maji na kuelekea katika msikiti wa mtume rehema na amani ziwe juu yake. Haondoki humo mpaka aswali swala ya alfajiri.
Kwa hiyo hadithi hii yaonesha ya kwamba baadhi ya maswahaba walikuwa hawalali usiku mzima katika mwezi mtukufu wa Ramadhani, bali walikuwa wakiuhuisha kwa ibada mbali mbali.
Na imepokelewa kutoka kwa Abdu Swamad anasema: ametusimulia Abu Al ash-abu Amesema:
Alikuwa baba Rajaau akikhitimisha Qur’ani katika kutuswalisha ndani ya  mwezi wa ramadhani kila baada ya siku kumi.
Yaani  kila siku walikuwa wakiswali taraaweh kwa juzuu tatu. Subuhaan LLAAH! Tupo wapi na hii mifano ya salafi swaalih katika swala zetu?
Hii ni baadhi tu ya mifano ya salaf swaalih na Qiyamu llayl ndani ya mwezi mtukufu wa Ramadhan. Lakini tukumbuke ya kwamba hawa watu si kwamba walikuwa wakijitahidi katika  ibaada ndani ya mwezi mtukufu wa Ramadhani kisha wakaachana nazo katika miezi mingine, la hasha. Bali walikuwa wakizitekeleza ibada hizi katika miezi mingine pia kama tulivyo ona upande wa usomaji wa Qur ani. Kwani makusudio ya Ramadhani si kumfanya mtu awe karibu na Allah katika mwezi wa Ramadhani tu, kisha baada ya hapo awe mbali na Allah, hapana. Matatizo yanayo jitokeza kwa watu wengi kwa kuwa karibu na Allah ndani ya mwezi mtukufu wa ramadhani na kuwa mbali naye katika miezi mingine, ni kuto jua au kusahau ni nini  makusudio ya mwezi mtukufu wa Ramadhani na kuto kuwa na maandalizi mazuri juu ya mwezi mtukufu huu.
Abu Othmani Annahdiy anasimulia ya kwamba: Nilimkaribisha Abu Hurayra 'radhi za Allah ziwe juu yake' nyumbani kwangu yeye na mkewe na mfanyakazi wake. Wakawa wanaugawa usiku sehemu kuu tatu: Anaswali huyu kisha anamuamsha huyu kisha anamuamsha huyu.
Alikuwa Shaddaadi bin ‘Awsi 'Allaah amridhie' pindi anapo elekea kulala, alikuwa ni kama vile mfano wa  punje katika kikaango. Kisha anasema "Ewe Allah hakika moto wa jahannam wanifanya mie nisilale”. Kisha anaamka na kuanza kuswali.
Mifano hii miwili na mingineyo mingi yajulisha ya kwamba Salaf swaalih walikuwa hawamuabudu Allaah au kuwa karibu na Allaah ndani ya mwezi  mtukufu wa Ramadhani tu. Bali walikuwa na miezi mingine ni wenye hima ya juu katika ibada pia, isipokuwa hima yao ndani ya mwezi mtukufu wa Ramadhani ilikuwa ni ya juu zaidi kutokana na fadhila za mwezi huu mtukufu.
Twamuomba Allah atuwakikishe katika yale anayo yapenda na kuyaridhia.