Asslaamu alaykum warahmatu llahi wabarakaatuh;
Shukurani zote anastahiki Allah, na rehema na amani ziwe juu ya Mtume Muhammad.
Siku zote inatakiwa muislam asiwe mwenye kuzembea katika mambo mbali mbali yenye manufaa, khususani misimu ya utiifu kama vile Ramadhani. Bali inatakiwa awe wa mwanzo katika twa’a hizo na awe ni mwenye kushindana na kuhakikisha ya kwamba hakuna anaye mpita.
قال الله تعالي:( وَفِي ذَلِكَ فَلْيَتَنَافَسِ الْمُتَنَافِسُونَ)
المطففين:26
Anasema Allah ndani ya kitabu chake kitukufu:
(Na katika hayo {mambo ya kheri} washindanie wenye kushindana).
Suurat Al Mutwafifiin: 26
Imepita miezi, mawiki na masiku na hivi sasa umekaribia Mwezi wa Qur‘an, mwezi wa Baraka, mwezi wa ibada za usiku, mwezi wa kukubaliwa dua za waumini. Ewe Allah tufikishe Ramadhani!
Maswahaba walilelewa na madrasa ya Mtume wakihisi hisia hizi za kuwa na shauku ya kuufikia mwezi wa fadhila, wakiishi na dua hii "Ewe Allah tufikishe Ramadhaan!"
Wakawa wakimuomba Allah awafikishe Ramadhani kabla ya miezi sita, na miezi sita mingine wakimuomba Allah akubali ibada zao.
Bila shaka hisia hizi na hali hii haikujengeka kwa Maswahaba isipokuwa kwa kujua fadhila za mwezi huu, na nafasi ya mwezi wa Ramadhani. Je ili tuweze kuupatia haki mwezi huu mtukufu wa Ramadhani tunatakiwa tufanyaje?
MAANDALIZI YA MWEZI WA RAMADHANI:
Bila shaka shughuli yoyote ile huwezi kuifanya vizuri isipokuwa mpaka uwe na utaalam nayo na umeifanyia mazoezi. Tuchukulie mfano michezo, iwapo kama timu itakuwa na mechi basi hutenga muda maalumu kwa ajili ya mazoezi ili kujiweka fiti na mechi hiyo. Licha ya kwamba wana utaalamu na mpira lakini yawapasa wafanye mazoezi ili waweze zimudu pirika za uwanjani.
Vile vile ibaada mbali mbali ikiwemo funga ya mwezi mtukufu wa Ramadhani inahitaji ujuzi na maandalizi, ili tuweze kuzikusanya fadhila mbali mbali zilizomo ndani ya mwezi mtukufu wa Ramadhani. Ikiwemo kufutiwa madhambi, kukubaliwa ibaada hiyo ya funga na mengineyo.
Maandalizi hayo ni:
1. Kumuomba Allah Atufikishe Ramadhani
Kukithirisha kumuomba Allah atufikishe katika mwezi wa ramadhani "Ewe Allah tufikishe Ramadhani":
Masiku haya ambayo tumeukaribia mwezi mtukufu wa Ramadhaniinatubidi tuzidishe sana kumuomba Allah atufikishe ramadhani.Kwani kufikishwa ramadhaani ni moja ya neema za Allah.Watu wengi watamani kufikkishwa mwezi mtukufu wa ramadhani lakini si kila mmoja anaye tamani ataufikia.Kuna baadhi ya watu tulikuwa nao ramadhani iliyo pita lakini mpaka hivi sasa hatupo nao tena.Kwa hiyo sie tulio ruzukiwa uhai mpaka hivi sasa yatubidi tujitahidi kumuomba Allah atufikishe mwezi huu mtukufu wa ramadhani mwezi wa fadhila"Ewe Allah tufikishe ramadhani".
2. Kukithirisha kufunga katika mwezi wa shaabani:
Ni sunna kukithirisha swaumu katika mwezi wa shaabani kwa ajili ya kuiweka sawa nafsi kwa ajili ya kuupokea mwezi wa ramadhani.
Na hii ndio ilikuwa hali ya mtume,kama anavyo simulia Ummu al mu-uminiina Aisha radhi za Allah ziwe juu yake
(مَا رَأَيْتُ رَسُوْلَ الْلَّهِ صَلَّىَ الْلَّهُ عَلَيْهِ وَ سَلَّمَ اسْتَكْمَلَ صِيَامَ شَهْرٍ قَطُّ إِلَّا رَمَضَانَ وَ مَا رَأَيْتَهُ فِيْ شَهْرٍ أَكْثَرَ صِيَاما مِنْهُ فِيْ شَعْبَانَ)
رَوَاهُ الْبُخَارِيُّ
(Sikumuona Mtume anakamilisha swaumu mwezi mzima isipokuwa Ramadhani. Na sikumuona anakithirisha funga katika miezi kama alivyo kuwa akikithirisha kufunga katika mwezi wa Sha'baani)
Hadithi imepokelewa na Bukhari.
Kwa hiyo yapendezwa kuanza kufunga tokea mwanzo mwa mwezi wa Sha’aban, vile vile siku tatu katika mwezi; yaani ayyaamul baidh (Siku za tarehe13,14 na15 za kalenda ya Hijri) Vile vile siku ya Jumatatu na Alkhamis.
NB: Haitakiwi kufunga siku moja au mbili kabla ya Ramadhani
عَنْ أَبِىْ هُرَيْرَةَ رَضِىَ الْلَّهُ عَنْهُ قَالَ:قَالَ رَسُوْلُ الْلَّهِ صَلَّىَ الْلَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ:(لَا تُقَدِّمُوا رَمَضَانَ بِصَوْمِ يَوْمٍ وَلَا يَوْمَيْنِ إِلَّا رَجُلٌ كَانَ يَصُوْمُ صَوْما فَلْيَصُمْهُ)
رَوَاهُ مُسْلِمٌ
Imesimuliwa kutoka kwa Abu Huraira radhi za Allah ziwe juu yake kasema: Kasema Mtume Muhammad rehema na amani ziwe juu yake (Msitangulize Ramadhani kwa kufunga siku au siku mbili, isipokuwa kwa yule aliye kuwa akifunga kabla yake basi afunge)
Hadithi imepokelewa na Muslim.
Yaani haitakiwi kufunga siku moja au mbili kabla ya Ramadhani isipokuwa kwa yule aliyekuwa akifunga kabla. Mfano kwa yule aliyekuwa akifunga siku ya Jumatatu na Alkhamisi. Basi ikidondokea moja ya hizo siku kabla ya Ramadhani kwa siku moja au mbili hakuna tatizo kwa mtu huyu kufunga. Au kwa yule mtu aliye panga kufunga mwezi wa shaabani karibia wote kama alivyo kuwa akifanya mtume basi hakuna tatizo. Au kwa mtu aliyekuwa kajizoesha kufunga siku na kufuturu siku basi hakuna tatizo kwake kufunga pia.
Vile vile haitakiwi kufunga siku ya shaka. Na siku ya shaka ni siku ya thelathini ya mwezi wa shaabani ikiwa usiku wake ulikuwa ni wenye mawingu mengi kiasi kwamba ikawa hawezekani kujua kama kuna mwezi au hapana.Imeitwa siku ya shaka kwa sababu katika hali hiyo ya mawingu tunakuwa na shaka je mwezi umeonekana au hauja onekana?
Wanazuoni wametofautiana kuhusiana na katazo la kufunga siku hii ya shaka. Je ni katazo linalo fidisha uharamu wa kufunga siku hii au ni katazo linalo fidisha karaha (yaani yachukiwa)kwa hiyo ni bora zaidi mtu asifunge?
Rai yenye nguvu juu ya suala hili ni kwamba katazo hili linafidisha uharamu kufunga siku hii kama inavyo onekana wazi katika hadithi za Mtume (rehma na amani juu yake)
3. Kuishi na Qur ani:
Yatakiwa kujitahidi katika kusoma Qur ani angalau juzu moja kwa siku, ili mpaka unaisha mwezi wa shaabani unakua ushakhitimisha Qur ani japo mara moja. Vile vile yatakiwa kutenga muda maalumu kwa ajili ya kusoma na kuzingatia aya mbali mbali katika Qur ani na wala si kutosheka kwa kuisoma haraka haraka tu.
4. Qiyamu llayli:
Yatakiwa kujitahidi kuswali ibaada za usiku tahajudi na witri; japo raakaa mbili tahajudi na rakaa moja witri. Swali rakaa mbili kwa mazingatio. Kumbuka swala ni mawasiliano kati ya mja na Mola wake. Wakati wa kuswali hisi ya kwamba unazungumza na Allah na anakuona na kukusikia. Soma suurat al Faatiha na sura baada yake kwa mazingatio na utulivu wa hali ya juu, kwa kufanya hivyo utahisi radha ya ibada isiyo sifika na kuhisi furaha ya maisha ya kweli. Kwani furaha ya maisha ya kweli inapatikana katika kumtii Allah sub-hanahu wata’ala na kukithirisha ibaada mbali mbali ikiwemo kuswali na ibaada za usiku. Na yule atakaye hisi ya kwamba kumtii Allah na kutekeleza ibaada mbali mbali ni kujibana na kuto yafaidi maisha basi dhana yake hiyo itakuwa ni potofu.
5. Kujifunza hukumu zinazo husiana na Ramadhani:
Inatakiwa muislamu amuambudu Allah ‘azza wa jall kwa elimu au ujuzi, kwani kujua hukumu za faradhi mbali mbali ambazo Allah ta’ala kazifaradhisha kwa wanaadamu ni lazima kwa kila muislamu. Na katika faradhi hizo ni faradhi ya funga ya mwezi mtukufu wa Ramadhani. Kwa hiyo yatakiwa kujua hukumu na mas’ala mbali mbali yanayo husiana na funga ya mwezi mtukufu wa Ramadhani ili funga zetu ziwe sahihi na ziweze kubaliwa. Kwa hiyo yatupasa kusoma vitabu mbali mbali vinavyo husiana na funga ya Ramadhani na kuwauliza wenye elimu katika yale mambo tunayo tatizwa nayo.
Anasema mwenyezi Mungu mtukufu ndani ya Qur ani
فَاسْأَلوا أَهْلَ الذِّكْرِ إِنْ كُنْتُمْ لا تَعْلَمُونَ))
الأنبياء :7
(Basi waulizeni wenye elimu ikiwa nyinyi hamjui.)
Al anbiyaa:7
6. Kuizoesha nafsi kwa kupunguza baadhi ya vyakula:
Inatakiwa ujizoeshe kuacha baadhi ya vyakula licha ya kwamba wavipenda ili nafsi yako itakapo fika Ramadhani iwe ishazoea hali ya kuacha baadhi ya mambo, hali itakayo pelekea kufunga Ramadhani kiurahisi. Yatakiwa ujitahidi kuipa dunia mgongo (Azzuhdi) kiasi kwamba mwezi wa shaabani kwako uwe una tofauti kiasi na miezi mingine katika vyakula, vinywaji mavazi na mengineyo. Mfano mzuri katika hili ni wale ambao huumwa na vichwa kwa sababu ya kukosa chai asubuhi, basi inafaa kuanza kujizowesha kukosa kunywa chai hata kabla ya mfungo wa Ramadhani ili ikifika Ramadhani jambo hili lisikupe taabu.
7. Mazoezi ya ulimi:
Yatakiwa ujizoeshe kusema ukweli na kuachana na uongo, usengenyaji na ufitinishaji. Kwani mambo haya hayatakiwi yafanywe na muislamu yoyote na kwa mfungaji basi makatazo yake ni ya hali ya juu. Haitakiwi mfungaji awe ni mwenye kudanganya kusengenya na kufitinisha watu.
قَالَ الرَسُوْلُ الله صَلَّى الله عَلَيْهِ وََسَلَّم: "مَنْ لَمْ يَدَعْ قَوْلَ الزُّوْرِ وَالعََمَلَ بِهِ فَلَيْسَ لِله حَاجَةٌ فِيْ أَنْ يَدَعَ طعَامَهُ وَشَرَابَهُ" (رواه البخاري والترمذي وأبو داود وابن ماجه وأحمد)
Imetokana na Abu Hurairah (Radhi za Allaah ziwe juu yake), Amesema Mtume rehma za Allaah na amani zimshukie): “Yoyote ambaye hatoacha kauli za uwongo (chafu) pamoja na matendo, basi Allaah hana yaja ya mtu huyu kuacha kula na kunywa. (Imepokelewa na Bukhari, MuslimAbu Dawud, Ibn Majah na Ahmad)
Hadithi hii itatuthibitishia kwamba ulimi mchafu ni tosha kuwa sababu ya kutokubali kwa funga ya mfungaji.
8. Kuihesabu nafsi:
Ni bora kila mwisho wa siku ukakaa na kuihesabu nafsi yako umefanya madhambi mangapi na kumtubia Allah na kuahidi ya kwamba huto rudia tena, na kukumbuka adhabu ya moto, je mwili wako upo tayari kuishi motoni? Bila shaka hii pia itakusaidia katika kutekeleza funga ya mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa ukamilifu. Kwani funga ya Ramadhani si kujizuia na vyakula vinywaji na yale yenye kufuturusha, bali ni funga ya mauvo pia. Lengo la funga ya mwezi mtukufu wa Ramadhani ni kuwafanya watu wawe wachamungu. Na uchamungu ni kufuata maamrisho ya Allah na kuachana na makatazo yake.
Bila shaka maandalizi haya iwapo kama tutayatekeleza kiukamilifu, basi ya yanatosha kuwa sababu kuufunga mwezi wa Ramadhani kiukamilifu, kiurahisi na kuhisi thamani ya Ramadhani na kutamani laiti mwaka wote ungekuwa ni Ramadhani.
Ewe Allah tufikishe Ramadhani na ukubali ibada zetu, hakika Wewe ni Msikivu, Mjuzi wa yote na juu ya kila jambo ni Muweza.