Maana ya Ikhfaa
Ikhfaa katika lugha ina maana ya kuficha au kufunika, katika istilaah, ikhfaa maana yake kuficha nun saakina au tanwin inapofuatiwa na herufi za ikhfaa. Nun saakina au tanwin huwa na ghunna yenye haraka mbili, au hutamkwa baina ya idghaam na idh haar. Hukmu hii pia inajulikana kama ikhfaa haqiqiya (إخفاء حقيقيا)
Herufi za Ikhfaa
Herufi za ikhfaa ni kumi na tano nazo ni:
االتاء - الثاء - الجيم - الدال - الذال - الزاء - السين - الشين - الصاد - الضاد - الطاء - الظاء - الفاء - القاف - الكاف (ت، ث، ج، د، ذ، ز، س، ش، ص، ض، ط، ظ، ف، ق، ك)
Ili kuweza kukumbuka herufi za Ikhfaa kirahisi, toa herufi zote za hukmu za idghaam (herufi 6), idh haar(herufi 6) na Iqlaab (herufi 1), zinazobakia zote ni herufi za ikhfaa.
Matokeo ya Ikhfaa
Ikhfaa hutokea iwapo moja kati ya herufi za ikhfaa itafuatiwa na nun saakina katika neno moja au baina ya maneno mawili au tanwin baina ya maneno mawili yaani la mwanzo linaishia nun saakina au tanwin na la pili linaanzia herufi ya ikhfaa.
Utamkaji wa Ikhfaa
Ikhfaa hutamkwa kwa kuficha sauti ya noon (katika nun saakina au tanwin) na nun au tanwin hutamkwa kwa ghunna (iliyo fupi yaani haraka mbili)
Wakati ikhfaa inapotamkwa ni lazima mtamkaji afanye tahadhari ya kuitamka nun bila ya kugusa sehemu ya juu ya mdomo kwa ncha ya ulimi, iwapo msomaji atafanya kosa hili, nun itasikika kwa kudhihirika na hivyo badala ya kuwa ikhfaa na itakuwa nun mudhwaharah (نُوْن مُظَهَرَة)
Mifano ya Ikhfaa
1. Ikhfaa inapatikana baina ya maneno min na sharri
مِنْ شَرِّ الْوَسْوَاسِ الْخَنَّاسِ [١١٤:٤]
2. Ikhfaa ipo baina ya maneno naaran na dhaata
سَيَصْلَىٰ نَارًا ذَاتَ لَهَبٍ [١١١:٣]
3. Ikhfaa ipo katikati ya neno antum baina ya herufi za nun na taa.
وَلَا أَنْتُمْ عَابِدُونَ مَا أَعْبُدُ [١٠٩:٥]
4. Hukmu ya ikhfaa ipo baina ya ‘an na swalaatihim.
الَّذِينَ هُمْ عَنْ صَلَاتِهِمْ سَاهُونَ [١٠٧:٥]
5. Ikhfaa ipo baina ya maneno dharratin na sharra.
وَمَنْ يَعْمَلْ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ شَرًّا يَرَهُ [٩٩:٨]
Tanbihi
Noon saakina inapotanguliwa na herufi yenye dhwammah (ضَمَّة) katika ikhfaa, hefuri hii inatakiwa kutamkwa kwa “kujaa mdomoni - kwa uzito”, pia ni lazima ifanyike tahadhari juu ya muda wa kutamka, yaani usizidishwe. Hii ina maana dhwamma isije kutiwa madda na kuivuta kama kwamba ina waw (و) yenye sukun. Mfano wa kosa hili hufanyika katika neno kuntum (كُنْتُمْ). Vile vile heruhi kabla ya nun ya ikhfaa inapokuwa na kasra (كَسْرَة) kama kwenye neno minkum (مِنْكُمْ) kosa kama hili pia hufanyika.