MAANA YA TWAHARA NA UMUHIMU WAKE KATIKA SALA


Twahara katika lugha maana yake ni kujisafisha/usafi. Tunapozungumza twahara katika Uislamu ni kuondoa uchafu na vyenye kuchafua, hii ni sehemu ya usafi wa kimwili au mahala au kivazi. Lakini pia twahara ina upande wa kiimani au tuseme usafi wa ki’akida. Na Allaah anatuambia katika Qur’aan:

خُذْ مِنْ أَمْوَالِهِمْ صَدَقَةً تُطَهِّرُهُمْ وَتُزَكِّيهِم بِهَا وَصَلِّ عَلَيْهِمْ ۖ إِنَّ صَلَاتَكَ سَكَنٌ لَّهُمْ ۗ وَاللَّهُ سَمِيعٌ عَلِيمٌ 
Chukua sadaka katika mali zao, uwasafishe na uwatakase kwazo, na uwaombee rehema. Hakika maombi yako ni utulivu kwao. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia Mwenye kujua. [9:103]

Bila ya shaka yoyote twahara itakayotokana na sadaqa itakuwa sio twahara ya kimwili bali ni twahara ya kuitakasa mali kiimani.

Kinyume chake katika sura hito hito Allaah anatuambia:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِنَّمَا الْمُشْرِكُونَ نَجَسٌ 
Enyi mlio amini! Hakika washirikina ni najsi [9:28]

وَلُوطًا آتَيْنَاهُ حُكْمًا وَعِلْمًا وَنَجَّيْنَاهُ مِنَ الْقَرْيَةِ الَّتِي كَانَت تَّعْمَلُ الْخَبَائِثَ ۗ إِنَّهُمْ كَانُوا قَوْمَ سَوْءٍ فَاسِقِينَ
Na Luut' tukampa hukumu na ilimu na tukamwokoa na ule mji ulio kuwa ukifanya maovu. Hakika hao walikuwa watu wabaya, wachafu. [21:74]
Aya hizi zinatudhihirishia kuwa kinyume cha twahara sio uchafu tu wa kimwili bali pia uchafu wa matendo ya haramu na kufuru.
Ni kawaida ya mafuqahaa (maulamaa wa fiqhi) kuanza mafundisho ya Fiqh na mlango wa twahara kwa sababu  twahara ni sharti miongoni mwa masharti ya swalaah, pia swalaah ni nguzo ya pili baada ya shahada na twahara ndio ufunguo wa swalaah. Huwezi kuswali bila ya kuwa na twahara. Mbali na kuswali pia twahara inatulazima tunapofanya ibada nyingine kama vile ibada ya twawafu (kutufu al Ka’ba). Hata hivyo katika somo letu litalenga katika swalaah.
Pia kuna suala muhimu kuhusiana na twahara ambalo zaidi linawalenga ma’ulamaa na wenye kutafuta elimu ya dini ya Allaah, Uislamu. Watu hawa wanatakiwa kuzisafisha nyoyo zao, yaani kutafuta kwao elimu iwe ni kwa ajili ya kutafuta radhi za Allaah tu na si vingivenyo, hiyo ndio nia pekee iliyo sahihi. Pia wanatakiwa kuachana na matendo machafu yote ambayo Allaah ‘azza wa jall ameyaharamisha. Si kwamba wengine hawatakiwi kuwa na haya lakini waliofungamana na elimu wa jukumu zaidi katika haya. Mambo mengine yanayowahusu maulamaa ni pamoja na kufuata sharia’h, kutangaza dini kwa watu na kuondoa ujimga katika jamii ili watu wamuabudu Allaah kwa ujuzi. 


SWALA BILA YA TWAHARA HAISWIHI
عَنْ أَبِي هُرَيْرَة رَضِيَ عَنْهُ قَالَ: قَالَ رَسُوْلُ اللهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: لَا يَقْبَلُ اللهُ صَلَاةَ أَحَدِكُمْ إِذَا أَحْدَثَ حَتَّى يَتَوََضَأً
Amesimulia Abu Hurayrah [radhi za Allaah zimshukie]; Amesema Mtume wa Allah (rehma na amani juu yake): Allaah haikubali swalaah ya mmoja wenu ikiwa ataingiwa na hadhath (tahara itamtoka) mpaka atakapotawadha.

MAZINGATIO YA HADITHI
1. Swalah haikubaliki mpaka mtu awe na twahara kamili; yaani ajisafishe kutokana na hadath ndogo (mfano kutokwa na udhu) na kubwa (mfano kuingiwa na janaba). 
2. Al Hadhath (kushuta, kufanya naja ndogo au kubwa n.k) ni kwenye kutoa/kukata udhu na iwapo hadah itakukuta ukiwa kwenye sala basi hubatilisha sala yako.
3. Maana ya “Allaah haikubali swalaah” ni kwamba Swalaah haitokuwa sahihi na anayeitekeleza katika hali hiyo hatapa malipo yaliyokusudiwa.
4. Hadithi hii pia ina maana kwamba twahara ni sharti ambalo lazima litimiswe kabla kuingia kwenye ibada ya swalaah.