Laylatul Qadr


Laylatul Qadr kilugha, maana yake ni usiku wenye nguvu au usiku wenye kudra au usiku wa cheo kitukufu, ni usiku maalum ambao unapatikana mara moja tu katika kila mwaka ndani ya mwezi wa Ramadhani. Huu ni usiku ambao Allaah ta’ala anatuambia  katika kitabu chake kitukufu kuwa Qur’ani imeteremshwa, Allaah ta’ala  anatuarifu:-

إِنَّا أَنزَلْنَاهُ فِي لَيْلَةِ الْقَدْرِ
Hakika Sisi tumeiteremsha (Qur'ani) katika Laylatul Qadri, Usiku wa Cheo Kitukufu.
Kama tunavyofahamu kuwa Qur’ani ni kitabu ambacho kina faida nyingi ndani yake ikiwa ni pamoja na kuwa ni muongozo kwa wenye taqwa, ni shifaa kwa wenye kuiamini, ni maelekezo ya maisha sahihi kwa wenye kukifata ni chanzo mama cha sharia za Allaah ta’ala kwa waislamu na wanaadamu kwa ujumla. Bila shaka usiku huu unastahiki kuwa na hadhi kubwa. Kuhusu uteremkaji huo wa Qur’ani Ibn Abbas (radhi za Allaah ziwe juu yake) anasema:-
Allaah ameishusha Qur’ani yote ikiwa imehifadhiwa kwenye al Lahwul mahfudh kwenda kuwekwa kwenye Baytul ‘izza ambayo ipo kwenye mbingu ya dunia. Kisha ikaletwa kwa Mtume sehemu baada ya sehemu kwa mujibu wa matukio kwa muda wa miaka ishirini na tatu.
Mtume rehma na amani juu yake ameuzungumzia usiku huu katika hadithi mbali mbali. Kama hii ilivyosimuliwa na Abuu Hurayra:-
 عن أبي هريرة ، قالَ : كَانَ رسولُ اللهِ صلي الله عليه وسلم يُبَشِّرُ أصْحَابَةُ ، يقولُ : " قَدْ جَاءَكُمْ شَهْرُ رَمَضانَ شَهْرٌ مُبَارَكٌ فَرَضَ اللهُ عليكم صِيَامَهُ ، تُفَتَّحُ فيه أبوابُ الجَنَّةِ ، وَتغلَّقُ فيه أبوابُ النَّارِ ، فيه لَيْلَةٌُ خَيْرٌ من ألفِ شَهْرٍ ، مَن حُرِمَ خَيْرَها فقد حُرِمَ "
Imetokana na Abu Hurayra (radhi za Allaah ziwe juu yake) amesema: Amekuja Mtume rehma na amani juu yake na kuwabashiria maswahaba na kasema “Umekujieni mwezi wa Ramadhani, mwezi wenye baraka, Allaah amekufaradhishieni ndani yake kufunga, hufunguliwa ndani yake milango ya peponi na hufungwa milango ya motoni, ndani yake kuna usiku ulio bora kuliko miezi elfu, atakaekosa kheri zake basi amenyimwa
Pia ubora wa usiku huu umethibitishwa katika Qura’ni pale Allaah ‘azza wa jall anapotuambia:-
لَيْلَةُ الْقَدْرِ خَيْرٌ مِّنْ أَلْفِ شَهْرٍ
تَنَزَّلُ الْمَلَائِكَةُ وَالرُّوحُ فِيهَا بِإِذْنِ رَبِّهِم مِّن كُلِّ أَمْرٍ
Laylatul Qadri ni bora kuliko miezi elfu.
Huteremka Malaika na Roho katika usiku huo kwa idhini ya Mola wao Mlezi kwa kila jambo.
Mbali na kuwa na ubora kuliko miezi elfu pia kwa idhini yake Allaah ta’ala huteremshwa malaika katika usiku huo kutokana na wingi wa kheri za usiku huo. Vile vile Mtume rehma na amani zimshukie ameuzungumzia usiku huu kuwa ni usiku wa kusamehewa dhambi, kama ilivyoelezewa katika hadithi ifuatayo:- 
عَنْ  أَبِيْ هُرَيْرَةَ  رَضِيَ الْلَّهُ عَنْهُ ‏عَنْ الْنَّبِيِّ  صَلَّىَ الْلَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ  قَالَ  مَنْ قَامَ لَيْلَةَ الْقَدْرِ إِيْمَانا وَاحْتِسَابا غُفِرَ لَهُ مَا تَقَدَّمَ مِنْ ذَنْبِهِ 
Amesimulia Abu Hurayra kwamba amesema Mtume rehma na amani juu yake “mwenye kusimama katika laylatul qadr kwa imani na kutaraji malipo atasamehewa dhambi zake zote zilizotangulia.
Kusamehewa dhambi ni kitu ambacho kila binadamu anakihitaji kwa vile sote ni watenda dhambi. Hii ni neema kubwa kwa Waislamu kwa hiyo hatuna budi kujitahidi kusimama kwenye ibada katika kuutafuta usiku wenye ubora wa hali ya juu na neema nyingi.
Usiku huu unapatikana katika usiku witiri wa kumi la mwisho la mwezi huu ambapo sasa zimebaki siku chache tu kama anavyotuthibitishia Mtume rehma na amani juu yake:-
 عَنْ عُبَادَةَ بْنِ الصَّامِتِ , أَنّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ , قَالَ : " لَيْلَةُ الْقَدْرِ فِي الْعَشْرِ الْبَوَاقِي , مَنْ قَامَهُنَّ ابْتِغَاءَ حِسْبَتِهِنَّ فَإِنَّ اللَّهَ يَغْفِرُ لَهُ مَا تَقَدَّمَ مِنْ ذَنْبِهِ , وَهِيَ لَيْلَةُ وِتْرٍ تِسْعٌ أَوْ سَبْعٌ أَوْ خَمْسٌ أَوْ ثَلاثٌ أَوْ آخِرُ لَيْلَةٍ " .
Imetokana na ‘Ubada bin As Swaamit (radhi za Allaah zimshukie) Hakika Mtume rehma na amani juu yake amesema: “Laylatul Qadr inatokea katika mwezi wa ramadhani katika kumi la mwisho, mwenye kusimama kwa imani na matarajio basi hakika Allaah atamsamehe dhambi zote zilizotangulia, nao ni usiku wa witiri, ama tisa au saba au tano au tatu au usiku wa mwisho.
 Huu ndio uthibitisho wenye uhakika juu ya ni lini usiku huu unapatikana kinyume na ile itikadi isiyo sahihi kwamba usiku huo ni usiku wa kuamkia ramadhani ya ishirini na saba.
Hivyo basi ni muhimu sana kwetu sisi waislamu kuendelea kufanya ibada katika siku zilizobaki za kumi hili ili kwa rehma zake Allaah tukawa ni wenye kuupata usiku huu na Allaah kutukubalia dua, istigfaar, toba na ibada zote nyingine.  Tunamuomba Allaah atukubalie funga zetu, sala zetu, du’aa zetu na atutenge sisi na madhambi kama ilivyotengana mashariki na magharibi.


1 Qur’ani Suratul Qadr aya ya 1 (97:1)


2 Qur’ani, Suratul Baqara aya ya 2 (2:2)


3 Ni kifaa maalum (mfano wa tableti au ubao) ambapo Qur’ani yote iliandikwa na kuhifadhiwa kwenye kifaa hicho .


4 Baytul ‘izza ni nyumba tukufu iliyoko kwenye nbingu ya dunia ambapo Qur’ani ikiwa kwenye Lahwul Mahfudh ilihifadhiwa kwenye nyumba hiyo.


5 Maelezo haya ya Ibn Abbas yanapatikana kwenye Tafsiri ya Ibn Kathir katika maelezo ya aya ya kwanza ya Suratul Qadr. 


6 Imenakiliwa kwenye Sahihi Bukhari .


7 Imenakiliwa kwenye Sahihi Bukhari.


8 Hadithi hii umekaririwa kwenye maelezo ya tafsiri ya ibn Kathir ya Surat al Qadr.