Idh-haar katika lugha maana yake ni kuweka wazi au kudhihirisha, maana ya idh-haar katika tajwid ni kutamka herufi kwa uwazi kwa usahihi kutoka katika sehemu yake ya kutamkia bila ya kutia ghunna. Idh-haar shafawi ni kuitamka mim (م) kwa uwazi.
Herufi za Idh-haar shafawi: Hukmu hii ina herufi ishirini na sita (26), nazo ni herufi zote za kiarabu ukitoa baa (ب) na mim (م) kwa vile hizi zipo kwenye hukumu za Idghaam swaghiir na Ikhfaa shafawi.
Namna inavyotokea: Hukmu hii inatokea iwapo mim saakina (مْ) itafuatiwa na moja katika ya herufi ishirini na sita za hukmu hii. Hutokea ndani ya neno moja au baina ya maneno mawili.
Namna ya kutamka: Mim saakina (مْ) hutamkwa kwa uwazi na usahihi kutoka katika sehemu yake ya kutamkia bila ya kutia ghunna.
Tahadhari: Msomaji anatakiwa kuwa makini zaidi anapotamka idh-haar shafawi iwapo mim saakina inafuatiwa na herufi za faa (ف) na waw (و) asije kutamka kwa ikhfaa. Uwezekano wakutia ikhfaa unatokana na ukaribu wa matamshi ya mim (م) na herufi mbili hizi yaani faa (ف) na waw (و)
Mifano ya Idh-haar shafawi
Suratul Fat-ha (1:2): idh-haar shafawi iko katika neno Alhamdu baina ya herufi za mim saakina na dal
الْحَمْدُ لِلَّهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ
Suratul Ikhlaas (112:3): Idh-haar shafawi baina ya lam na yaliid na pia baina ya lam na yuulad
لَمْ يَلِدْ وَلَمْ يُولَدْ
Suratul ‘Aadiyaat (100:5); Idh-haar shafawi ipo kwenye neno jam’aa baina ya herufi za mim na ‘ayn.
فَوَسَطْنَ بِهِ جَمْعًا