Asili na chimbuko la Shirk

Shukrani zote zinamsahiki Allah, Rabb (Mola mlezi) wa viumbe vyote, na mwisho mwema ni wa wenye taqwa. Rehma na amani zimshukie Mtume wa Allah, pamoja na watu wake na Masahaba zake.
Kwa idhini ya Allah ‘azza wa jall, katika makala hii tutajadili juu ya mwanzo na chanzo cha dhambi ya shirk. Historia inaonesha kwamba watu walioishi miaka ipatayo 2000 ya mwanzo baada ya baba yetu Adam ‘alayhi salam kuletwa Duniani hawakuwa washirikina. Yaani watu wa Nabii Adam (‘alayhi salam) na Nabii Idris (‘alayhi salam), wao hawakumshirikisha Allah subhanahu wa ta’ala. Watu wa mwanzo kumshirikisha Allah ‘azza wa jall ni watu walioishi wakati wa Nabii Nuuh ‘alayhi salam. 
Ibn ‘Abbas radhi Allahu ‘anh amesema; baina ya Adam na Nuuh ni vizazi (Qarn) kumi, wote hawa walikuwa juu ya ukweli, kisha wakatofautiana, ndipo Alllah akawapelekea Mitume wenye kuwapa bishara njema na maonyo. [Ibn Jarir at Tabari katika tafsiri yake (4/275)]
Katika matn ya hadithi hii neno lilotumika kama vizazi (kumi) ni neno Qarn. Qarn linaweza kufasiriwa kama ama vizazi (generations) au karne yaani miaka mia moja. Lakini hoja kwamba hapa ni vizazi kumi ina nguvu kutokana na jina la Nabii Nuuh (‘alayhi salam)
Ibn Kathir amelitaja katika tafsiri yake jina kamili la nabii Nuuh ‘alayhi sallam kuwa “Nuuh bin Lamak bin Matushalakh bin Khanukh. Khahukh ni, kama wanavyodai, Nabii Idris ‘alayhi salam. Idris alikuwa ni mtu wa mwanzo kuandika kwa kutumia kalamu, naye alikuwa mwana wa Barad bin Mahlil, bin Qanin bin Yanish bin Shith bin Adam” Ukihisabu vizazi kutoka Adam ‘alayhi salam mpaka Nuuh ‘alayhi salam utapata kuwa ni vizazi kumi. 
Vile vile kwa mujibu wa Ibn Kathir tofauti ya muda baina ya Nabii Adam (‘alayhi salam) na Nabii Nuuh (‘layhi salam) ni miaka 1056. Hata hivyo idadi ya miaka 1056 ni kwa mujibu wa Biblia kitabu ambacho hatutakiwi kusadiki wa kukanusha ikiwa hakuna ushahidi mwingine wa kuthibitisha au kukanusha hoja yoyote kutoka kwenye mafunzo yetu, yaani Qur’ani tukufu na Sunnah. Kama utachukua miaka 1056 na umri aliopewa baba yetu Adam (‘alayhi salam) ambayo ni miaka 960 utapata jumla ya miaka ipatayo 2016, miaka hii imepita bila ya Allah ‘azza wa jall kushirikishwa. 
Watu hawa walioanza shirk walikataa kumfuata Nabii Nuuh ‘alayhi salam, badala yake waliabudu masanamu, na majina ya masanamu hayo ni Waddan, Suwa'a, Yaghuth, Ya'uq na Nasra. Allah ‘azza wa jall amewataja Miungu hii ya uongo katika Surat An Nuuh: 
وَقَالُوا لَا تَذَرُنَّ آلِهَتَكُمْ وَلَا تَذَرُنَّ وَدّاً وَلَا سُوَاعاً وَلَا يَغُوثَ وَيَعُوقَ وَنَسْراً
 Na wakasema: Msiwaache miungu yenu, wala msimwache Wadda wala Suwaa' wala Yaghuth, wala Yau'q, wala Nasra
Asili ya majina haya ni ya wachamungu waliyoishi katika jamii hii kabla yao. Baada ya Wadda wa wenziwe kufariki watu hawa walisimika masanamu yao yawe kama ni kumbukumbu ya wachamungu hawa. Ibn Kathir katika maelezo ya aya hii amesema “Masanamu haya yalipewa majina ya wacha mungu walioishi wakati wa Nabii Nuh. Walipokufa wachamungu hawa, shetani akawashawishi watengeneze masanamu kwa ajili ya kumbukumbu wa wachamungu hao, Wakafanya hivyo. Masanamu haya hayakuabudiwa, (muda ukapita na) waliojenga wakafariki na sababu ya kuwepo kwao (masanamu) ikawa haijulikani, ndipo masanamu hayo yakaanza kuabudiwa. 
Ibn Jarir at Tabari amesema “Kisha wakatengeneza masanamu yao,  baada ya kufa kwa wale waliotengeneza, kizazi kilichofuata walijiwa na Iblis na kuambiwa ‘walioishi kabla yenu waliyaabudu masanamu haya na wakapata mvua, watu hawa nao wakaanza kuayaabudu’
Binadamu kwa asili yake ameumbwa hali akitambua kwamba shirk si jambo linalifaa kutendwa. Yaani kila mmoja wetu huzaliwa hali kwamba anatambua mamlaka ya Allah sub-hanahu wa ta’ala, hii ni kwa sababu kila mmoja wetu huzaliwa akiwa ni mwenye fitra sahihi. Imekaririwa riwaya hii katika Sahihi Muslim:-
عَنْ أَبَا هُرَيْرَةَ  قَالَ قَالَ رَسُولُ اللَّهِ  صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ  مَا مِنْ مَوْلُودٍ إِلَّا يُولَدُ عَلَى الْفِطْرَةِ ثُمَّ يَقُولُ اقْرَءُوا  فِطْرَةَ اللَّهِ الَّتِي  فَطَرَ  النَّاسَ عَلَيْهَا لَا تَبْدِيلَ لِخَلْقِ اللَّهِ ذَلِكَ الدِّينُ الْقَيِّمُ
Abu Hurayra amesema, kasema Mtume (salla Llahu ‘alayhi wa sallam) Hakuna mtoto aliyezaliwa isipokuwa katika Fitra. Kisha akasema, Hapana mabadiliko katika uumbaji wa Allah. Hiyo ndiyo Dini iliyo nyooka sawa. (Muslim)
Ayah ii Aliyoisoma Mtume (salla Llahu ‘alayhi wa sallam) ni aya ya 30 katika Surat ar Rum. Hadith hii kwa ujumla inadhihirisha kwamba kwa asili, Allah ‘azza wa jall ametuumba na fahamu kwamba ushirikina ni jambo lisilofaa, vile vile iwapo binadamu hakufundishwa hawezi kuwa mshirikina.
Wakati tulionao shirk imeota mizizi kwenye Dini zote zisizo Uislam, wako wenye kumuabudu Nabii ‘Issa (‘alayhi salam) na Budha, wako wenye kuabudu Jua , mwezi na nyota, wako wenye kuabudu miti na mashetani. Miongoni mwa wenye kufanya shirk ni pamoja wa wale wanaokanusha kuwepo kwa Mwenye Enzi Mungu. Shirk vile vile imoeta mizizi hata miongoni mwa wanaojiitakidi kuwa ni Waislamu. Kwa mfano Shia Alawi (au Nusayri) ambao wapo Syria wao wanashudia kwamba “Laa ilaha illa ‘Ally” (yaani hapana Mola anayestahiki kuabudiwa kwa haki Isipokuwa ‘Ally) Ni kundi hili la Mashia ambalo ndilo limewanyanyua ‘Ali (radhi Allah ‘nh), Salman Al Farsi (radhi Allah ‘anh) na Muhammad (Salla Llahu ‘alayhi wa sallam) kuwa ni waungu au wamejigeuza kuwa watu kutoka kwenye ‘Uungu’
Mwisho kabisa kuabudu visivyokuwa Allah (‘azza wa jall) hupelekea kupata maradhi ya kuzama kwenye shirk kwani humfanya mtendaji kuamini kwamba anavyoviabudu ni vyenye nguvu za kufanikisha mambo mengi ayatakayo, na hivyo hupelekea  anavyovitumia kumshirikisha Allah ‘azza wa jall kuchukua nafasi ya Allah katika moyo na akili ya muhusika. Mwenye kufanya shirk hata kama si yote anayofanikiwa katika anayofanyia shirk, lakini huwa anayakumbuka yale ambayo anayofanikiwa na kisahau mengi ambayo hakufanikiwa.