Tahwid Asma' wa Sifaat

Tawhid al asma’ wa sifaat inahusika na kuudumisha upweke wa Allah (‘Azza wa Jall) katika majina na sifa zake. Ni lazima Muislamu aamini kwa dhati kwamba Allah (‘Azza wa Jall) amekamilika kwa sifa ambazo hazina upungufu wala udhaifu. Allah (Sub-hanahu wa Ta’ala) katika sifa na majina yake hafanani na yoyote au chochote. Ingawa sisi binadamu tuna sifa ambazo kwa majina zinafanana na sifa za Allah ta’ala, lakini kwa uhakika sifa hizo hazifanani, kwa mfano katika Qur’ani tukufu Allah (sub-hanahu wa ta’ala) amesema:
وَيُعَذِّبَ الْمُنَافِقِينَ وَالْمُنَافِقَاتِ وَالْمُشْرِكِينَ وَالْمُشْرِكَاتِ الظَّانِّينَ بِاللَّهِ ظَنَّ السَّوْءِ عَلَيْهِمْ دَائِرَةُ السَّوْءِ وَغَضِبَ اللَّهُ عَلَيْهِمْ وَلَعَنَهُمْ وَأَعَدَّ لَهُمْ جَهَنَّمَ وَسَاءتْ مَصِيراً
Na awape adhabu wanafiki wanaume na wanafiki wanawake, na washirikina wanaume na washirikina wanawake, wanaomdhania Allah dhana mbaya. Utawafikia mgeuko mbaya, na Allah awakasirikie, na awalaani, na awaandalie Jahannamu. Na hayo ni marudio maovu kabisa. (48:6)
Katika aya hii tunaona kwamba Allah (‘Azza wa Jall) anaghadhibika (anakasirika). Sifa kama hii kwa jina pia tunayo sisi viumbe. Hata hivyo kinachofanana katika sifa hii ni jina tu. Lakini binaadamu anapoghadhibika sifa hii kwake huleta udhaifu mkubwa. Kwanza mara nyingi tunapoghadhibika sisi binaadamu tunapoteza subira na kupoteza uwezo wa kujizuia kufanya mabaya kama vile kupiga, kuharibu au kutumia lugha isiyotahiki. Sisi huishia kutenda yasiyostahiki na hivyo huingia makosani. Wenye uchache wa kumfahamu Allah (‘Azza wa Jall) wanaweza  kusema kwamba Allah ta’ala hana ghadhabu kwa vile ghadhabu kwa binadamu ni udhaifu. 
Ili kutofautisha mfanano wa namna hii ni lazima turudi kwenye Qur’an tukufu, Allah (sub-haahu wa ta’ala) amesema:
... لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ وَهُوَ السَّمِيعُ البَصِيرُ
...Hapana kitu kama mfano wake. Naye ni Mwenye kusikia Mwenye kuona. (42:11)
Kwa vile hakuna chochote au yoyote kama mfano wake, haiwezi kuwa ghadhabu zetu zifanane na Mola wetu. Said Qutb katika Fi dhilalil Qur’an juu ya aya hii amesema “hisia zetu kwa asili zitupelekee kuamini kwamba aliyeumbwa hawezi kufanana na muumba” Na Imam Ibn Kathir katika maelezo ya tafsiri yake anasema “Yeye Muumba wa mbea mbili ni wa aina ya pekee, amekamilika (mwenye kujitosheleza), Mfalme (yu mmiliki wa kila kitu), hana aliyesawa naye au anayefanana naye”
Ushahidi katika Tawhid asmaa’ wa sifaat upo katika aya nyingi mno katika Qur’an tukufu. Aya iliyopo juu (42:11) imetaja mbili kati ya sifa zake nyingi nazo ni kuona na kusikia. Allah (sub-hanahu wa ta’ala) pia amesema:
اللّهُ لاَ إِلَـهَ إِلاَّ هُوَ الْحَيُّ الْقَيُّومُ لاَ تَأْخُذُهُ سِنَةٌ وَلاَ نَوْمٌ لَّهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الأَرْضِ مَن ذَا الَّذِي يَشْفَعُ عِنْدَهُ إِلاَّ بِإِذْنِهِ يَعْلَمُ مَا بَيْنَ أَيْدِيهِمْ وَمَا خَلْفَهُمْ وَلاَ يُحِيطُونَ بِشَيْءٍ مِّنْ عِلْمِهِ إِلاَّ بِمَا شَاء وَسِعَ كُرْسِيُّهُ السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضَ وَلاَ يَؤُودُهُ حِفْظُهُمَا وَهُوَ الْعَلِيُّ الْعَظِيمُ
Allah - hapana mungu ila Yeye Aliye hai, Msimamia mambo yote milele. Hashikwi na usingizi wala kulala. Ni vyake pekee vyote viliomo mbinguni na duniani. Ni nani huyo awezaye kuombea mbele yake bila ya idhini yake? Anayajua yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma yao; wala wao hawajui chochote katika vilio katika ujuzi wake, ila kwa atakalo mwenyewe. Enzi yake imetanda mbinguni na duniani; na wala haelemewi na kuvilinda hivyo. Na Yeye ndiye aliye juu, na ndiye Mkuu. (2:255)
Sentensi kumi hizi kamilifu mno na zitoshe kufahamu sifa nyingine za Allah, kwani ni aya nyingi mno zinazozitaja sifa hizi zisizo pungufu. Jambo la msingi katika Tawhid al asma’ wa sifaat tutosheke kuyajua majina na kuzijua sifa Allah (‘Azza wa Jall) kama alivyotueleza katika kitabu chake kitukufu na kama alivyotufundisha mbora wa viumbe, Mtume (Salla Llahu ‘alayhiwa sallam). Tusijaribu kutaka kupunguza au kufahamu zaidi ya hapo. 
Uhakika ni kwamba hatuna uwezo wa kumfahamu Allah zaidi ya alivyotufahamisha mwenyewe. Ni vipi akili iliyo na upungufu tuliopewa na aliyetuumba iweze kumfahamu aliyekamilika zaidi alivyotaka mwenyewe? Hili linapojaribiwa mara nyingi mdadisi huishia kwenye kufru na shirki na kukosa majibu ya maswali mengi ambayo hata akipewa majibu hayamsaidii kufika kusikofikika. Kutafuta elimu ya namna hii kutaishia kupata elimu isiyo na manufaa, isiyostahiki hata kuitwa elimu.
Mambo yafuatayo ni lazima yazingatiwe katika Tawhid hii:
1.) Ni lazima tumtaje Allah (Sub-hanahu wa ta’ala) kwa majina ambayo yameelezewa kwenye Qur’an na kama alivyotufundisha Mtume (Salla Llahu ‘alayhi wa sallam). 
2.) Hatuwezi kumuongezea Allah sifa au majina ambayo hayamo katika Qur’an na Sunna, hata kama tunadhani kwamba majina hayo au sifa hizo ni nzuri au zinamuelekea. Mathalan hatuwezi kumwita Allah (‘Azza waJall) Al Ghaadib (mwenye hasira au mwenye kukasirika) pamoja na kwamba Qur’an imetuelezea kwamba ameghadhibika.
3.) Hatuwezi kumpa Allah (‘Azza wa Jall) sifa za viumbe. Mathalan watu wa imani zisizo Uislamu wanaamini kwamba Allah (‘Azza wa Jall) ameumba Dunia kwa siku sita na siku ya saba akapumzika. Ni kweli Allah (Sub-hanahu wa ta’ala) ameumba Ardhi, Mbingu na vilivyomo baina yake kwa siku sita, lakini kusema kwamba alipumzika ni kosa kwani mwenye kupumzika anakuwa amechoka na hii ni sifa ya viumbe na si ya Muumba.
4.) Watu (au kiumbe chochote) hakiwezi kupewa sifa za Allah (sub-hanahu wa ta’ala) kama Manasara walivyomfanya Issa (‘Alayhi salam) kuwa ni Mungu au mwana wa Mungu.
5.) Viumbe hatuwezi kutumia majina ya Allah bila ya kutanguliza ‘Abd’ na hasa majina yaho yanapotanguliwa na kiambishi awali ‘ar’, ( Ar Rahmaan) au ‘Al’ (Al Baasit). Viambishi awali hivi vinapokosekana huruhusu baadhi ya majina au sifa hizi kutumika kwa viumbe, kwa mfano Allah (sub’hanahu wa ta’ala) katika Qur’ani amemwita Mtume wetu (salla Llahu ‘alayhi wa sallam) Rauf na tena Rahim; Allah (‘Azza wa Jall) amesema:
لَقَدْ جَاءكُمْ رَسُولٌ مِّنْ أَنفُسِكُمْ عَزِيزٌ عَلَيْهِ مَا عَنِتُّمْ حَرِيصٌ عَلَيْكُم بِالْمُؤْمِنِينَ رَؤُوفٌ رَّحِيمٌ
Hakika amekwisha kujieni Mtume kutokana na nyinyi wenyewe; yanamhuzunisha yanayo kutaabisheni; anakuhangaikieni sana. Kwa Waumini ni mpole na mwenye huruma. (9:128)
6.) Haifai kutumia kiambishi awali Abd’ katika majina yetu kisha ikafuatiwa na majina ya viumbe. Mfano Abdur Rasuul, Abdun Nabii, Abdul Husayn na kadhalika. 
Kwa hiyo sisi binadamu haifai kujipa sifa au majina ya Allah ‘azza wa jall na pia haifai kumpa Allah sub-hanahu wa ta’ala majina au sifa zetu sisi viumbe. Na hata tukiwa na sifa yenye jina moja basi pia sifa hiyo haina usawa au ulunganifu wowote kati yetu sisi na Allah ta’ala.