Tawhid hii ni kuamini na kudumisha imani kwamba hapana mola anayestahiki kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allah ‘azza wa jall. Tawhid hii ni wazi kuwa inatokana na sehemu ya kwanza ya nguzo ya kwanza ya Uislamu (Sehemu ya pili ikiwa ni Muhammad (salla Llahu ‘alayhi wa sallam) ni mtume wake), yaani Laa ilaha illa Llah.
Kwa hiyo utekelezaji wa Tawhid Uluuhiya ni kumuabudu Allah ta’ala, na katika kumuabudu huko tunalazimika kutompa washirika kwa namna yoyote. Ni lazima kwamba tunapomuadu Allah ‘Azza wa Jall tujue kuwa sisi ndio wahitaji hali ya kuwa pamoja na kutuumba si mwenye kutuhitajia kwa chochote. Allah (Sub-hanahu wa ta’ala) kuabudiwa ni haki yake na kumpa mwingine au chingine chochote haki hiyo ni dhulma dhidi ya nafsi yako mwenyewe.
Katika hili, yaani kumuabudu asiye Allah (‘Azza wa Jall) au kumuabudu Allah (‘Azza wa Jall) pamoja naye kiumbe chingine hata ikiwa ni Mtume (salla Llahu ‘alayhi wa sallam) au Issa (‘alayhi salam) ni dhambi au kosa ambalo Allah (‘Azza wa jall) ameahidi kutolisamehe kosa hilo. Allah (‘Azza wa Jall) amesema:
إِنَّ اللّهَ لاَ يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَلِكَ لِمَن يَشَاءُ وَمَن يُشْرِكْ بِاللّهِ فَقَدِ افْتَرَى إِثْماً عَظِيماً
Hakika Allah hasamehe kushirikishwa, na husamehe yaliyo duni ya hilo kwa amtakaye. Na anaye mshirikisha Allah basi hakika amezua dhambi kubwa (4:48)
Ni lazima tuzingatie kwamba anayezungumziwa kwamba hatasamehewa ni yule ambaye amefanya shirki na mpaka yamemjia mauti bila ya kufanya toba. Labda swali la kujiuliza ni kwa nini Allah asisamehe kosa hili? Sehemu ya jibu la swali hili ni kwamba lengo hasa la Allah (‘Azza wa Jall) kutuumba ni kumuadubu yeye bila ya ushirika. Allah (sub-hanahu wa ta’ala) anasema katika Qura’an:
وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ
Nami sikuwaumba majini na watu ila waniabudu (51:56)
Kwa maana hiyo kuabudu chochote au yoyote isipokuwa Allah ta’ala kunapoteza kabisa lengo la kuumbwa kwa binadamu. Hivyo basi aina zote za ibada ni lazima mkusudiwa awe ni Allah (‘azza wa jall) na zisipitie kwa kiumbe kwa ushirika wa aina yoyote.
Sidhani kama Tawhid uluuhiya inahitaji kutolewa ushahidi zaidi wa kuwepo kwake kutoka kwenye Qur’an kutokana na ukweli kwamba aya kadhaa tulizozitaja hapo juu tayari ni ushahidi wa kutosha, hata hivyo kwa kuongezea Allah ‘Azza wa Jall amesema:
أَمْ كُنتُمْ شُهَدَاء إِذْ حَضَرَ يَعْقُوبَ الْمَوْتُ إِذْ قَالَ لِبَنِيهِ مَا تَعْبُدُونَ مِن بَعْدِي قَالُواْ نَعْبُدُ إِلَـهَكَ وَإِلَـهَ آبَائِكَ إِبْرَاهِيمَ وَإِسْمَاعِيلَ وَإِسْحَاقَ إِلَـهاً وَاحِداً وَنَحْنُ لَهُ مُسْلِمُونَ
Je! Mlikuwapo yalipo mfikia Yaaqub mauti, akawaambia wanawe: Mtamuabudu nani baada yangu? Wakasema: Tutamuabudu Mungu wako na Mungu wa baba zako, Ibrahim na Ismail na Is- haaq, Mungu Mmoja tu, na sisi tunasilimu kwake (2:133)
وَإِلَـهُكُمْ إِلَهٌ وَاحِدٌ لاَّ إِلَهَ إِلاَّ هُوَ الرَّحْمَنُ الرَّحِيمُ
Na Mungu wenu ni Mungu mmoja tu, hapana mungu ila Yeye. Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu (2:163)
فَاعْلَمْ أَنَّهُ لَا إِلَهَ إِلَّا اللَّهُ وَاسْتَغْفِرْ لِذَنبِكَ وَلِلْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ وَاللَّهُ يَعْلَمُ مُتَقَلَّبَكُمْ وَمَثْوَاكُمْ
Basi jua ya kwamba hapana mungu ila Mwenyezi Mungu, na omba maghufira kwa dhambi zako na za Waumini wanaume na Waumini wanawake. Na Mwenyezi Mungu anajua mahali penu pa kwenda na kurudi, na mahali penu pa kukaa (47:19)
Kwa hiyo Tawhid ar Rubuubiya na Tawhid al asma’ wa sifaat ni masula ya kiitikadi, yaani tunahitaji kuamini juu ya sehemu hizi mbili za tawhid ka usahihi wake. Kwa upande mwingine Tawhid al Uluuhiya (au Al ‘Ibada) ni sehemu ya utekelezaji, kwani ibada ni utendaji.