Shirk katika Ibada - Ash Shirk Al Akbar

Shirk katika ibada ni shirk ambayo matendo ya ibada huelekezwa kwa asiye Allah sub-hanahu wata’ala. Shirk hii ambayo pia hujulikana kama Shirk katika uluuhiya, vinavyoabudiwa huwa ni viumbe kama vile banadamu, majini, miti, jua na kadhalika. Shirk katika ibada imegawika katika sehemu mbili nazo ni shirk al akbar (shirk kubwa) na shirk al asghar yaani shirk ndogo.
Ash Shirk al Akbar
Mitume yote imekuja kutoa maelekezo kuhusu namna ya kumuabudu Allah ‘azza wa jall, sehemu kuu ya mafunzo haya ni kuwafamisha wanadamu kuepuka shirk hii. Yaani kumuadubu muumba badala ya viumbe. Allah ‘azza wa jall anasema katika Qur’an:-
وَلَقَدْ بَعَثْنَا فِي كُلِّ أُمَّةٍ رَّسُولًا أَنِ اعْبُدُوا اللَّهَ وَاجْتَنِبُوا الطَّاغُوتَ
Na kwa hakika kwa kila umma tuliutumia Mtume kwamba: Muabuduni Allah na muepukeni twaaghut. (6:36)
Twaaghut ni chochote kinachoabudiwa pamoja na Allah ta’ala au badala ya Allah ta’ala. Na kufuata twaaghut ndio kuingia katika shirk al akbar. Ni lazima tufahamu kwamba si kila kinachoabudiwa ni chenye makosa kwani vingine ni chaguo la wafuasi kuabudu wanachokiabudu, ka mfano ‘Issa ‘alayhi salam hakutaka wala kuamrisha aabudiwe. Pia wako wale ambao wenyewe wametaka kuabudiwa kama vile Jathya Sai Baba na Fir’aun, hawa huingia makosani wao pamoja na wafuasi wao.
Ili kuweza kuepuka shirk hii tunalazimika kufuata maelekezo ya Mtume husika kwa wakati wako. Kwa nyakati zilizopita, ilikuwa sahihi kwa watu kufuata mafunzo ya Nabii Adam ‘alayhi salam, Halafu Nabii Idris ‘alayhi salam, halafu Nabii Nuuh ‘alayhi salam mpaka ikafika wakati wa nabii ‘Issa ‘alayhi salam. Kwa wakati tulionao hatuna budi kufuata mafunzo ya Mtume Muhammad sallallahu ‘alayhi wasallam. Kumfuata Mtume mwengine yoyote kwa wakati huu kisha ukamkataa Mtume Muhammad sallallahu 'alayhi wasallam itakuwa hukufuata maamrisho ya Allah ta'ala. Na kuwafuata mitume ni amri ya Allah 'azza wajall. Allah ta’ala anatuambia katika Qur’an:- 
مَّن يُطِعِ الرَّسُولَ فَقَدْ أَطَاعَ اللَّهَ
Mwenye kumt'ii Mtume basi ndio amemt'ii Allah (4:80)
Kwa hiyo kundi la kwanza linaloingia katika shirk al akbar ni lile ambalo limeasi au kukataa kutii mafunzo sahihi ya Allah ta’ala kupitia Mtume Muhammad (sallalahu ‘alayhi wasallam) na kuchagua kufuata upotofu mwingine wowote. 
Viel vile njia nyingine ambayo inaweza kupelekea watu kuingia katika shirk al akbar ni kuwa na mapenzi makubwa na kitu, katika uislam mapenzi kwa Allah ‘azza wajall huoneshwa kwa kuwa na utiifu kamili katika amri zake na makatazo yake, hapa hatuzungumzii mapenzi ambayo mtu humpenda mama yake, mwanawe, mke au mume kwani kumpenda Allah kwa namna hii kunaweza kumuingiza mja katika shirk ya Asmaa wa sifaat, kwani tumempa Allah mapenzi ya viumbe jambo ambalo halimstahiki. Mapenzi kwa Allah ni kujisalimisha kwake na kufuata matakwa ya Allah badala ya mapenzi ya moyo. Allah ta’ala anatuambia katika Qur’an: 
قُلْ إِن كُنتُمْ تُحِبُّونَ اللَّهَ فَاتَّبِعُونِي يُحْبِبْكُمُ اللَّهُ...
Sema: Ikiwa nyinyi mnampenda Allah basi nifuateni mimi, Allah atakupendeni...(3:31)

Kwa hiyo utiifu huambatana na mapenzi. Ikiwa binadamu atakuwa na mapenzi makubwa kupita kiasi na hivyo anachokipenda kikawa baina yake na Allah basi huenda akakiabudu anachokipenda bila hata kujijua. Kwa maelezo haya, wapo wenye kuabudu pesa, mpira au michezo mingine, muziki, televisheni, vitu vya kuchezea (PS3, PSP, Xbox), kompyuta  na kadhalika. 
Vile vile mtu huingia katika shirk al akbar kwa kufuata matamanio ya nafsi, Allah ta’ala anatuambia katika Qur’an:

أَرَأَيْتَ مَنِ اتَّخَذَ إِلَٰهَهُ هَوَاهُ
Je! Umemwona aliye yafanya matamanio yake kuwa ndio mungu wake?
Hivyo basi kufuata matamanio ya nafsi hupelekea kutokutii amri za Allah ta’ala na kutoyaepuka makatazo ya Allah sub-hanahu wata'ala na kuvunja msingi mkuu wa ibada ambao ni kumtii Allah ta’ala.
Ash shirk al akbar ni dhambi kubwa mno kiasi kwamba hufuta wema wowote ambao mja ameufanya katika maisha yake na ndio sababu iwapo mja hajatubu dhambi hii Allah ta’ala hatoisamehe na mwenye kutenda ataishia kwenda motoni. 


Dini zote za uongo huwa ni wenye kufanya shirk hii kwa kuabudu viumbe mbali mbali badala ya Allah ‘azza wajall. Wakristo humuabudu Yesu, Mabuda humuabudu Budha, wako wenye kumuabudu Sai Baba, wenye kuabudu wanyama, jua na viumbe vinginevyo. Waislam wenye itikadi za kisufi pia huingia katika shirk hii kwa kuitakidi na kufanya maombi kupitia mashekhe fulani au makaburi ya masharifu  fulani.
Shirk hii hupoteza lengo zima la kuumbwa kwetu nalo ni kumuadubu Allah pekee bila ya mshirika.  Katika suratudh Dhaariyaat, allah ta’ala anasema:- 
ومَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ [٥١:٥٦]
Nami sikuwaumba majini na watu ila waniabudu. (51:56)
Ni lazima tuwe makini katika suala shirk al akbar kwa vile hupoteza muelekeo na lengo zima la kuumba kwetu na Allah ta’ala. Allah ametupa ukumbusho ili kuwazindua wale waliozama kwenye shirk hii kwa kuwaabudu viumbe wengine, Allah anasema:- 
قُلْ أَرَأَيْتَكُمْ إِنْ أَتَاكُمْ عَذَابُ اللَّهِ أَوْ أَتَتْكُمُ السَّاعَةُ أَغَيْرَ اللَّهِ تَدْعُونَ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ [٦:٤٠]
Sema: Mnaonaje ikikujieni adhabu ya Allah, au ikakufikieni hiyo Saa (Qiyama) - mtamwomba asiye kuwa Allah, ikiwa nyinyi ni wakweli?
Ni wazi kwamba hakuna atayeliomba jua, jini au binadamu mwenziwe amsamehe siku hiyo, hakuna atayetaka msamaha kwa chochote ambacho si Allah saa hiyo itakapofika na hivyo vyenye kuabudiwa pia katika siku hiyo vitakuwa vinatarajia msamaha wa Allah ta’ala ili viumbe hivyo vifanikiwe ikiwa ni miongoni mwa majini au binadamu, sasa kwa nini tuabudu viumbe badala ya Muumba?