Shirk Katika Asmaa’ na Sifaat

Shirki katika majina na sifa za Allah (سبحنه وتعل) imegawika sehemu mawili. Sehemu ya mwanzo ni kumpa Allah (سبحنه وتعل) sifa au majina ya viumbe sehemu ya pili ya shirki hii ni kuwapa viumbe kama vile binadamu, majini au wanyama sifa na majina ya Allah (سبحنه وتعل) mabazo haziwastahiki kwa vile wao ni viumbe na sifa hizo hawanazo.
Shirk kwa Kumpa Allah (سبحنه وتعل) sifa za viumbe
Shirk hii hujumuisha kumpa Allah majina na sifa za viumbe mbali mbali kama vile wanyama, ,miti, mwezi, jua na hasa binadamu. Mara nyingi zaidi ni binadamu ambaye hufananishwa au kupewa sifa za uungu.
Hii ni kutokana na ukweli kwamba binadamu huchukuliwa kuwa ni kiumbe mwenye utawala, nguvu na akili kuliko viumbe wengine. Kwa hiyo anayeitakidiwa kuwa ni Mungu huchongwa au kuchorwa kama binadamu na mara nyingi huchorwa kama mtu afananaye na watu wa jamii husika. Kwa mfano Mahindu na Mabudha huwachora na kuwachonga waungu wao wakifanana na watu wa jamii zao. Vile vile Michelangelo amechora picha ya Yesu akiwa utupu tena ni mzungu, picha hiyo imechorwa kwenye Sistine Chapel ndani ya jiji la Vatican, kwa vile Michelangelo alikuwa ni Mtaliana. Hivyo basi  picha au masanamu yao huabudiwa (Yesu, Budha) kwa imani kwamba wao ni waungu. 
Ni muhimu kufahamu kwamba haifai kumpa Allah (عز وجل) majina au sifa ambazo yeye mwenyewe hakujinasibisha nazo katika Qur’an au katika sunna za Mtume Muhammad (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ). Kwa mfano hatuwezi kumwita Allah ‘azza wajall mkandarasi kwa vile ameiumba Dunia. Inawezekana kwa akili zetu wenyewe tukadhani kuwa ukandarasi (engineer) ni sifa nzuri lakini pia au inafanana na Al Khaaliq (mwenye kuumba) lakini wakandarasi ni dhaifu kwa mfano hawana uwezo wa kulitunza jengo kwa namna Allah anavyovitunza vile ambavyo ameviumba.
Shirk kwa kuwapa viumbe sifa au Majina ya Allah (عز وجل)
Shirk ya kuwapa viumbe majina na sifa za Allah ta’la hupatikana hata miongoni mwa jamii mabazo wenyewe hujiitakidi kuwa ni Waislam. Ni muhimu kusisitiza kwamba ziko sifa ambazo Allah (عز وجل) anazo na kwa jina pia binadamu amepewa sifa kama hizo. Kwa mfano katika Qur’an Alaah (عز وجل) anatuambia: -

لَقَدْ جَاءَكُمْ رَسُولٌ مِّنْ أَنفُسِكُمْ عَزِيزٌ عَلَيْهِ مَا عَنِتُّمْ حَرِيصٌ عَلَيْكُم بِالْمُؤْمِنِينَ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ [٩:١٢٨]
Hakika amekwisha kujieni Mtume kutokana na nyinyi wenyewe; yanamhuzunisha yanayo kutaabisheni; anakuhangaikieni sana. Kwa Waumini ni mpole na mwenye huruma.

Allah (عز وجل) katika aya hii amemtaja Mtume kuwa ni Rauf na Rahim yaani mpole na mwenye huruma (Na sio Ar Rauf na Ar Rahim). Hizi pia ni sifa za Allah (سبحنه وتعل). Hivyo basi sifa hizi hazina shirki anapopewa kiumbe kama binadamu lakini ni muhimu pia tufahamu kwamba kwa binadamu sifa hazina ukamilifu kama zilivyo kwa Allah ‘azza wajall, ndio maana Allah ni Ar Rahim na viumbe hawawezi kutanguliziwa ‘Ar’.
Aina hii ya shirk hujumuisha watu ambao hupewa au kujipa sifa au majina ya Allah (سبحنه وتعل). Kwa mfano Waarabu wakati wa ujahiliya waliwapa masanamu yao waliyoyaitakidi kuwa ni waungu majina ya Lata (La Laat) ambalo asili yake ni Ilaahi, ‘Uzza mabayo asili yake ni Al ’Aziz na Manata (La Manaat) ambayo asili yake ni Al Mannaan. Wakati wa Mtume (sallallahu ‘alayhi wasallam) Mtume wa uongo wa Yamama alijipa jina la Rahmaan. Jina hili ni la Allah na hakuna kuimbe mwenye kuchukua jina au sifa hii. 
Vilevile wako ambao wenyewe hujiitakidi kuwa ni waislamu lakini huingia katika shirk hii kwa namna moja au chingine. Mfano kundi la Mashia Nusayria wao huitakidi kuwa Ali bin Abi Talib (رضي الله عنه), Salman Al Farsi (رضي الله عنه) na Mtume (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) ni waungu waliokuja Duniani kwa umbile la binadamu, kama wanavyoitakidi Wakristo juu ya Issa (عليه السلام) au Yesu. Shia Ismailia pia huamini kuwa Agha Khan ni Mungu aliyekuja Duniani umbile la mtu. Itikadi hizi za kishirikina pia hupatikana miongoni mwa Wasufi kama vile Al Hajjaaj.
Vile vile nadharia ya Darwin ambaye amejaribu kuelezea asili ya binadamu kuwa ni kitu kilichoanza kikiwa hakina uhai na kwamba binadamu hakuumbwa ni shirki inayoingia kwenye kundi hili. Nadharia ya Albert Einstein ya Nguvu (Energy) ambayo inaelezea kwamba nishati (energy) haina mwanzo wala mwisho ni shirki inayoingia katika kundi hili. Kwani kila kitu kimeumbwa yaani kina mwanzo na kila kitu  kina mwisho au kitakuwa na mwisho, hakuna kitakachodumu milele isipokuwa Allah (سبحنه وتعل). Allah (سبحنه وتعل) natuambia katika Qur’ani tukufu:- 
اللَّهُ خَالِقُ كُلِّ شَيْءٍ ۖ وَهُوَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ وَكِيلٌ [٣٩:٦٢]
Allah ndiye Muumba wa kila kitu, na Yeye ndiye Mlinzi juu ya kila kitu. (39:62)
Vile vile Qur’ani inathibitisha juu ya mwisho wa kila kitu katika Surat Ar Rahmaan, Allah amesema: 
كُلُّ مَنْ عَلَيْهَا فَانٍ [٥٥:٢٦]
Kila kilioko juu yake kitatoweka. (55:26)
Baadhi yetu hutumbukia katika shirki hii kwa kuitana majina ambayo hayafai. Majina haya yanatokana na sifa timilifu za Alllah ta’ala ambazo binadamu hawanazo. Kwa mfano haifai kumwi ta mtu jina la Rahmaan, hii ni sifa ya Allah ambayo viumbe wote hawana.  Vile vile kuambatanisha neno Abdul (mja) na kufuatia na majina au sifa ambazo si za Allah ta’ala. Moja katika majina maarufu ya namna hii ni Abdul-Rasul (Mja wa Mtume) ambalo linaashiria kwamba kiumbe huyu ameumbwa na kupata ulinzi kutoka kwa Mtume (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ), jambo ambalo katika itikadi sahihi ya Kiislam ni shirk.
Ni lazima tuwe makini sana juu ya namna tunavyomsifu Allah (سبحنه وتعل), na isizidia au kupungua juu ya namna Allah (سبحنه وتعل) alivyojisifu mwenyewe katika mafunzo ya Kiislam kupitia Qur’ani na Sunna na pia namna ya tunavyojipa majina na sifa sisi wenyewe tusije tukajitukuza kupita kiasi kama walivyofanya baadhi ya watawala Ulimwenguni.