Mjue Nabii Yush'a Bin Nuun [يوشع بن نون عليه السلم]

Kaburi la Nabii Yush'a Bin Nuun (عليه السلم)
Shukrani zote zinamstahiki Allaah Mola Mlezi wa viumbe wote. Rehma na amani zimshukie Mtume  Muhammad, na watu wake, na masahaba wake na wale wote wenye kufuata mwenendo wake mpaka siku ya qiyama.

Nabii Yush'a Bin Nuun (عليه السلم) ni miongoni mwa manabii tunaowajua kupitia hadithi, kwa vile nabii huyu hakutajwa  kwenye Qur'aani tukufu kwa jina. Lakini Nabii Yush'a Bin Nuun ametajwa kwa kuwa kwake pamoja na Nabii Musa pale Allaah (عز وجل) alipoatumbia katika Surat Al Kahfi:

وَإِذْ قَالَ مُوسَىٰ لِفَتَاهُ لَا أَبْرَحُ حَتَّىٰ أَبْلُغَ مَجْمَعَ الْبَحْرَيْنِ أَوْ أَمْضِيَ حُقُبًا

Na pale Musa alipo mwambia kijana wake: Sitoacha kuendelea mpaka nifike zinapo kutana bahari mbili, au nitaendelea kwa muda mrefu. (18:60)

Akiielezea aya hii Imam Ibn Kathir (Allaah amrehemu) anasema "Sababu mazungumzo ya musa na mjakazi kijana wa kiume Yush'a Bin Nuun…" Hivyo basi "Kijana wake" katika aya hii ni Nabii Yush'a bin Nuun (عليه السلم). Nabii Yu'sha  ndiye aliyechukua uongozi wa Banii Israil mara baada ya Allaah kumchukua Nabii Haarun na  Musa  (amani iwe juu yao).

Kwa mujibu wa wana taarekh wa kiislamu Nabii Yu'sha katika damu ya utume ni kitukuu cha Nabii Yusuf (عليه السلم) Jina lake kamili ni Yu'sha Bin Nuun Bin Afraiym bin Yusuf. Nabii Yush'a alikuwa ni mtumishi wa Nabii Musa (عليه السلم), aliwaongoza Bani Israil katika Jihaad ya kuuteka mji wa Ariha ulioko upande wa pili wa mto Jordan kutoka muelekeo wa Bani Israil waliokuwa wakitokea Misri. 

 Nabii Yu'sha (عليه السلم) kama Mtume Muhammad (rehma na amani juu yake) Allah alimbarikia muujiza wa kulisimamisha jua. Ilikuwa ni siku ya Ijumaa katika nyakati za Alasiri wakati Yush'a aliliongoza Jeshi la Bani Israil dhidi ya maadui wa Allaah, mapigano yakaendelea mpaka jua likakaribia kutua, ambapo jua lingelitua Bani Israil wangelilazimika kuacha mapigano kwani ingeliisabiwa Jumamosi na wao hawakuruhusiwa kufanya kazi au shughuli kama vita katika siku ya Jumamosi. Ndipo Nabii Yush'a akamuomba Allaah (عز وجل) alisimamishe jua mpaka mapigano yatakapomalizika, na Allah akaipokea du'aa ya Nabii Yush'a. Mapigano haya yalikuwa ni ya kuikomboa Baytul Maqdis, na Allaah akalipa ushindi jeshi la Yush'a Bin Nuun (عليه السلم)

Mtume rehma na amani juu yake anasema "Yush'a aliliambia jua:

قال للشمس : انتى مأموره و انا مأمور , اللهم احبسها على شيأ 

 "Akasema kuliambia jua: Wewe unafuata amri na mimi nafuata amri, Ewe Allaah lisimamishe jua" 

Yush'a Bin Nuun aliuteka mji huu mtukufu akiwa na kizazi kipya. Mtume Muhammad rehma na amani juu yake anatueleza hakuna miongoni mwa wale waliobudu sanamu lilitongenezwa na Assamiriy alikuwemo kwenye jeshi la Yush'a bin Nuun lililokomboa Bayt al Maqdis. Akiwa Bayt al Maqdis Naabii Yush'a aliendelea kutawala kwa mafundisho ya Tawrat hadi mwisho wa maisha yake. Nabii Yush'a aliishi muda wa miaka 127.