Kijana mmoja alimwendea Mtume (rehma na amani ziwe juu yake) akamwambia: Ewe Mtume wa Allah, nipe idhini ya kuzini. Watu wakamzunguka na kuanza kumuonya. Vipi anaomba kuruhusiwa kufanya maasi na Mtume wa Mwenyezi Mungu? Mtume akawaambia: Hebu mleteni karibu yangu. Yule kijana akamsogelea Mtume (rehema na amani ziwe juu yake) akakaa.
Mtume akamuuliza: Je utaridhia zinaa kwa mama yako?
Kijana akajibu: Hapana Wallahi.
Mtume akamwambia: vivyo hivyo na watu wengine hawaridhii kwa mama zao.
Mtume akamuuliza: je utaridhia kwa binti yako?
Kijana akajibu: Hapana ewe mjumbe wa Allah.
Mtume akamwambia: na watu wengine hawaridhii kwa mabinti zao.
Mtume akamuuliza:Je utaridhia kwa dada yako?
Kijana akajibu: Hapana Wallahi.
Mtume akamwambia: na watu wengine hawaridhii kwa dada zao.
Mtume akamuuliza: Je utaridhia kwa shangazi yako?
Kijana akajibu: Hapana Wallahi.
Mtume akamwambia: na watu wengine hawaridhii kwa shangazi zao.
Mtume akamuuliza: Je utaridhia kwa Amma yako{Mama mdogo/mkubwa}?
Kijana akajibu: Hapana Wallahi.
Mtume akamwambia: na watu hawaridhii kwa Amma zao.
Kisha mtume akaweka mkono wake katika kifua cha kijana huyu na kumuombea dua:
<< اَللّهُمَّ اغْفِرْ ذَنْبَهُ، وَطَهِّرْ قَلْبَهُ، وَحَصِّنْ فَرْجَهُ >>
<< Ewe Allah msamehe madhambi yake, na utwaharishe moyo wake, na ikinge tupu yake. >>
Kijana akawa baada ya hapo hageuki kutizama chochote (miongoni mwa maasi)
1) Ustahmilivu na upole wa Mtume (rehema na amani ziwe juu yake), hata kwa waovu, kutokana na hivyo ndio maana tunamuona alikuwa ni mwalimu bora. Kwa tabia ya upole hata wenye fikra ovu walio wadogo kwake hawakuona uzito kumuelekea na kumueleza matatizo yao kama alivyo fanya kijana huyu, ndio maana yeye ni rehma kwa walimwengu wote, bila ya kujali wema au uovu, ukubwa au udogo.
Bila shaka wazazi, walezi, mashekhe na wote wenye kujihusisha na harakati za dini basi tuna mengi ya kujifunza juu ya tukio hili. Vile vile inatupasa tujiulize: kwa nini vijana wetu na waumini kiujumla baadhi ya nyakati huwa ni wagumu kuja kutueleza matatizo yao?
Ni muhimu kuepuka kutumia njia ambazo si munasibu au zenya kuleta masuluhisho ya kudumu katika matatizo tuliyonayo. Njia kama vile kulazimisha mambo, ukali uliopindukia mpaka, kiburi (kujiona kutokana na mamlaka au elimu au cghochote kinachokufanya ujihisi uko juu), kutokuwa na ufahamu wa kutosha juu ya kujenga mahusiano mema na mja mwenye kukosea na ukatili, ni mingoni mwa sababu zenye kuwafanya wakoseaji washindwe kutueleza matatizo yao ili tuweze kuwatatulia au kuwapa msaada unaostahiki.
2.) Tuangalie ni jinsi gani Mtume (rehema na amani ziwe juu yake)alikuwa ni mwenye kudhibiti hisia zake na akili yake khususani katika kumsikiliza mkoseaji na kutatua tatizo lake, licha ya kwamba watu walikwisha anza kumuonya na kumpigia kelele kijana yule dhidi ya ombi lake toka kwa Mtume.
Bila shaka katika hili tunajifunza ya kwamba: msuluhishaji na mtengenezaji wa mambo haitakiwi aathirike na hali halisi inayo lizunguka tatizo lile, ili asije akaongeza ukubwa wa tatizo au yeye mwenyewe kudongokea katika makosa, isimpelekee awe na jazba. Bali anatakiwa awe ni mtaratibu na mwenye utulivu, ajaribu kumsoma mkoseaji na kulisoma tatizo lile katika pande zote na kutoa utatuzi kwa nnjia unayostahiki. Ndio maana tunaona watu waliokuwa wamehudhuria katika majlisi ile ,walikuwa wakimkemea kijana yule, waliingiwa na jazba lakini mtume akawaambia hebu mleteni karibu yangu! subuhaana LLAH!
3.) Hebu jaribu kujenga picha ya tukio hili: Kijana anaomba ruksa ya kuzini, watu wote wamshangaa kijana huyu na kuanza kumkemea kwa sauti ya juu, vuta hisia utengeneze taswira halisi ya hali ya kijana huyu, Alikuwa katika hali gani?
Mtume akamkaribisha kwake ili ahisi hali ya amani na utulivu moyoni, akajaribu kutoa khofu ya makemeo ya wahudhuriaji walio ona ya kwamba kijana kakosa adabu sana, Vipi anamuomba Mtume ruksa ya kuzini? Mtume alimkaribisha kwake ili aweze mponya jeraha la makemeo aliyo yapata kijana huyu,na ili aweze mtoa katika zogo lile ili dawa atakayo mpatia iweze mfaa.
4)Pia vuta fikra alijisikia vipi kijana yule baada ya kuambiwa na Mtume: mkaribisheni kwangu! Katika hali ya zogo kama lile. Kijana hakumiliki isipokuwa kumkaribia mtume haraka pasina ya kusita na kuhisi amani ya hali ya juu. Usulubu wa Mtume rehema na amani ziwe juu yake ulikuwa ni smaku ya kumvuta kijana huyu.
5):Yule kijana baada ya kumkaribia Mtume akakaa, na hapa ulikuwa ni ukamilifu wa maandalizi ya Mtume kwa kijana huyu kwa ajili ya kuanza kumtibu. Kumpatia tiba ya kumfanya kijana aachane na suala lile analo likusudia kwa hoja za wazi na kukinaika.
6.) Katika tukio hili la kimalezi limejaa upole wa Mtume wa kivitendo na kimaneno. Kivitendo alimkaribisha kwake, na kimaneno (Je utaridhia [zinaa] kwa mama yako? Je utaridhia kwa binti yako? Je utaridhia kwa dada yako? Je waridhia kwa shangazi yako? Je utaridhia kwa amma yako?) Upole baadhi ya nyakati huwa ni ufunguo muafaka sana katika kukinaisha kihoja na kutatua matatizo.
Haya ni baadhi ya mazingatio mengi tunayoyapata kutoka katika hadithi hii iliyo jaa faida.