BAADHI YA MAMBO YANAYO SAIDIA KATIKA TOBA


1.) Kuwa na ikhlasi kwa ajili ya Allah Azza Wa jallah. na kuelekea kwake.
Ikhlasi kwa ajili ya Allah ni dawa yenye manufaa zaidi. Pindi mja akiwa na ikhlasi kwa ajili ya Mola wake, na akawa ni mkweli katika kutafuta toba, basi Allah atamsaidia juu ya jambo hilo, atakuwa nae na atamuondoshea vizuizi na vipingamizi katika njia ya toba.


2.) Kutokuwa na matumaini makubwa juu ya dunia na kukumbuka Akhera. 
  • Mja pindi atakapo tambua ufupi wa maisha ya duniani,na uharaka wa kuondoka kwake. 
  • Na akatambua ya kwamba dunia ni shamba kwa ajili ya akhera, 
  • Na akatambua ya kwamba dunia ni fursa ya kuchuma thawabu kwa ajili ya akhera,
  • Na akakumbuka neema za milele zilizopo akhera,
  • Na akakumbuka yale yaliyo motoni miongoni mwa  adhabu ziumizazo.
Wakati huo atapunguza kujiachia katika matamanio ya nafsi,na atajirejea kwa kufanya matendo mema dhidi ya uovu alio utanguliza.

3.) Kujishughulisha na mambo yenye manufaa na kujiepusha na upweke na kukaa bure pasina ya shughuli. Kwani kukaa bure pasina ya shughuli kunapelekea kupata/kuambatana na marafiki waovu, hali itakayo sababisha kuporomoka kitabia na kukosa maadili, kutokana na kuambatana na marafiki waovu.

Na pindi mja atakapo jishughulisha na mambo yenye manufaa Duniani na Akhera, basi itapungua hali yake ya kukaa pasina ya shughuli,na hatopata nafasi ya kufanya maovu na uharibifu.

4.) Kujiepusha na vishawishi vya maasi na kila kile chenye kukumbusha maasi. Kama vile:
  • Kutizama filamu chafu,
  • kusikiliza miziki,
  • kusoma magazeti ya udaku pamoja na majarida ya riwaya zenye kuchochea maasi.
Kama inavyo takiwa kujiepusha na kila sababu zinazo weza kumkumbusha maasi kama vile marafiki vijiwe na makempu.

5.) Kusuhubiana {kuambatana} na watu wema na kujiepusha na waovu. Kwani kusuhubiana na wema huuisha moyo na hupelekea kuwaiga watu wema. Na kusuhubiana na waovu kunapelekea kuyaona maovu kuwa ni mema na mema kuyaona kuwa ni maovu. Kwani rafiki humvuta rafiki yake katika kila jambo.

6.) Daima kukumbuka madhara ya madhambi na maasi.
Kwani miongoni mwa madhara yake ni kunyimwa elimu, kupunguziwa riziki na kukosa utulivu wa moyo. Pamoja na kufanyiwa uzito katika mambo yako, kuhisi kiza katika moyo, udhaifu wa mwili na kuharamishiwa matendo mema.
           
Maasi hupanda katika moyo mbegu za maasi mengine, na husababisha kuichukia toba kidogo kidogo,mpaka inafutika katika moyo wa mja fikra ya toba.Mwenyezi Mungu Mtukufu
atulinde na hayo.

7.) Kushikamana na dua: Kama vile kumuomba Allah akuepushe na maasi,akukinge na maasi au akutoe katika maasi. Kwani dua ni katika sababu kubwa za kujiepusha na maasi na ni dawa yenye kufaa zaidi.

Nayo{Dua} ni adui wa mabalaa huyazuia na huyaponya na huyapunguza na kuyaondoa.