Siku za Tashriq Si Siku za Kufunga

Shukrani zote zinamstahiki Allah, rehma na amani zimshukie Mtume (ﷺ), ali zake na masahaba wake pamoja na wote wenye kufuata mwenendo wake mpaka siku ya qiyama. 

Leo ni siku ya mwanzo kati aya siku tatu za Tashriq. Yaani tarehe 11, 12 na 13 za mwezi wa Dhul Hijjah. Siku hizi ni ziku zenye uzito mkubwa kwa vile zimetajwa katika Qur’aan Majiyd pale Allaah (عز وجل) alipotuambia:
وَٱذْكُرُوا۟ ٱللَّـهَ فِىٓ أَيَّامٍ مَّعْدُودَٰتٍ ۚ
Na mdhukuruni (mtajeni) Allah katika zile siku zinazo hisabiwa. [2:203]

Maulamaa ni wenye kukubaliana kuwa siku za zinazohisabiwa (ayyaman ma’duuudaat) zilizokusudiwa katika aya hii ni siku za Tashriq ikiwa ni pamoja na siku ya Idi ya tarehe 10 Dhul Hijjah. Imam Ibn Kathir katika maelezo yake ya aya hii ameeleza kuwa Ayaamin Ma’dudaat kuwa siku ya ‘Idi pamoja na siku za Tashriq na kasema huo ndio msimamo wa Ibn Umar, Ibn Az- Zubayr, Abu Musa, Ata, Mujahid, Ikrimah, Sa`id bin Jubayr, Abu Malik, Ibrahim An-Nakhai, Yahya bin Abu Kathir, Al-Hasan, Qatadah, As-Suddi, Az-Zuhri, Ar-Rabi bin Anas, Ad-Dahhak, Muqatil bin Hayyan, Ata Al- Khurasani, Malik bin Anas [radhi za Allah ziwashukie] na wengineo 

عَنِ ابْنِ عُمَرَ ـ رضى الله عنهما ـ قَالاَ لَمْ يُرَخَّصْ فِي أَيَّامِ التَّشْرِيقِ أَنْ يُصَمْنَ، إِلاَّ لِمَنْ لَمْ يَجِدِ الْهَدْىَ
Kutoka kwa ibn Umar (radhi za Allah ziwashukie) amesema hakun alaiyeruhusiwa kufunga siku za tashriq isipokuwa wale waisokuwa na uwezo wa hadi (kujincha) [Sahihi Bukhari, Mjeledi wa 30, Hadithi ya 103]

Hivyo basi yoyote ambaye amechinja, awe ni hujaji au si hujaji siku hizi haruhusiwi kufunga kabisa. Amenukuliwa tena Mtume (ﷺ) katika hadithi iliyopokelewa na ‘Uqba bin Aamir akisema:

يَوْمُ عَرَفَةَ وَيَوْمُ النَّحْرِ وَأَيَّامُ التَّشْرِيقِ عِيدُنَا أَهْلَ الإِسْلاَمِ وَهِيَ أَيَّامُ أَكْلٍ وَشُرْبٍ
Siku ya Arafa na siku ya Nahr na Siku za Tashriq ni ‘Idi (sikukuu) kwetu sisi Watu wa Uislamu (waislamu) Nazo ni siku za kula na kunywa. [Jami` at-Tirmidhi, Mjeledi wa 8, Hadithi ya 92]

Ama kwa siku ya Arafa ni kufunga siku hiyo sunna miongoni mwa sunna kubwa kwa watu ambao hawakusimama Arafa siku hiyo, yaani wale wasio mahujjaaj. Naye Bishri bin Suhaim (رضي الله عنه) amesema Mtume (ﷺ) khutbah katika siku za Tashriq na kusema: 

لاَ يَدْخُلُ الْجَنَّةَ إِلاَّ نَفْسٌ مُسْلِمَةٌ وَإِنَّ هَذِهِ الأَيَّامَ أَيَّامُ أَكْلٍ وَشُرْبٍ
Hatoingia yoyote peponi isipokuwa aliye Muislamu na hakika ya siku hizi ni siku za kula na kunywa. [Sunnan Ibn Majah, Mlango wa Siyam, Hadithi ya 1791]

Hivyo basi hadithi zote hizi zimeweka wazi kuwa siku hizi si siku za kufunga. Ni siku za ’Idi ambazo tunapaswa kula na kunywa huku kama ilivyoamrisha aya tuliyoinukuu mwanzo tukimdhukuru Allah kwa wingi mno. 

Tumdhukuru vipi Allah katika Siku hizi?
Tunashukuru mkwa kuleta wingi wa takbiri kila baada ya Sala. Na pia kuongeza takbir hizi kwa wingi katika nyakati mbali mbali katika siku hizi

Tuzishukuru neema za Allaah kila tunapokula na kunywa, hivyo kuleta wingi wa Tahmiyd. (yaani kusema Alhamdulillah), na pia kuendelea kumshukuru Allaah (عز وجل) katika nyakati mbali mbali ndani ya siku  hizi.

Na kila namna ambayo itaashiria kumdhukuru Allaah (عز وجل) zaidi basi huu ni wakati wa kufanya kwa wingi mno. 

Allah ndiye mjuzi zaidi 

FADHILA ZA KUSALI RAKAA NNE KABLA NA BAADA YA ADHUHURI

Shukrani zote zinamstahiki Allah Mola Mlezi wa viumbe wote. Rehma na amani zimshukie Mtume pamoja na ali zake, masahaba wake na wale wote wenye kufuata mwenendo wake mpaka siku ya qiyama.

Miongoni mwa sunna muhimu ni sunna ya kusali rakaa nne kabla na baada ya sala ya adhuhuri. Hadithi ifuatayo inaeleza wazi juu ya fadhila za kusali rakaa hizo za sunna: 

عَنْ أُمِّ حَبِيبَةَ رضي الله عنها عَنْ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ : ( مَنْ صَلَّى أَرْبَعًا قَبْلَ الظُّهْرِ وَأَرْبَعًا بَعْدَهَا لَمْ تَمَسَّهُ النَّارُ ) ]روى النسائي (1817) والترمذي (428)]
Amesimulia Umm Habibah (رضي الله عنه) kuwa Mtume rehma na amani juu yake amesema: mwenye kusali rakaa nne kabla ya adhuhuri na nne baada yake moto hautomgusa. [An-Nasaa’i (1817) and at-Tirmidhi (428)]

 ولفظ الترمذي : ( مَنْ حَافَظَ عَلَى أَرْبَعِ رَكَعَاتٍ قَبْلَ الظُّهْرِ وَأَرْبَعٍ بَعْدَهَا حَرَّمَهُ اللَّهُ عَلَى النَّارِ)
Na katika riwaya ya at-Tirmidhi amesema: (mwenye kuzihifadhi rakaa nne kabla ya adhuhuri na rakaa nne baada yake Allaah atamharamishia moto) 

والحديث صححه الألباني في صحيح النسائي .
Hadithi hii imesahihishwa na Imam Albani katika sahihi an-Nisaa’i

Kuhifadhi hapa ina maana ya kuwa mwenye kuziendeleza au mwenye kudumu kwenye rakaa nne nne hizi, huku akiwa ni mwenye kuyafuata masharti na kila lile ambalo limeambatana na ibada ya sala. 

Rakaa nne hizi ni za kawaida ambazo tunazifahamu maarufu kama Kabliyya na Baadiyya ambazo wengi husali rakaa mbili mbili badala ya nne nne. Hata hivyo si makosa kusali mbili kabla na baada lakini fadhila hizi zimeelezewa kwa wale wenye kusali rakaa nne nne. Hivyo iwapo mja atasali rakaa mbili basi Allah atamlipa malipo mazuri.

Nyakati za rakaa hizi, zile za kabla husaliwa baada ya adhana ya adhuhuri (au baada ya kuingia wakati wa adhuhuri) na kabla ya kusaliwa sala ya adhuhuri. Ama zile mbili za baada husaliwa baada ya sala ya adhuhuri na kabla ya kuingia kwa wakati wa sala ya alasiri. 


Allah ndiye mjuzi zaidi. 

Kuihimiza Familia Kusali

Shukrani zote zinamstahiki Allah, Mola mlezi wa viumbe wote. Rehma na amani zimshukie Mtume na watu wake, na masahaba wake pamoja na wote wenye kufuata mwenendo wake mpaka siku ya qiyama. 

Kuiamrisha familia kusali ni amri ya Allaah, amri hii imewekwa wazi bilaya utata wa aina yoyote kwenye Qur’aan, Allah ta’ala anatumbia katika Surat at Ta-Ha: 
وَأْمُرْ أَهْلَكَ بِٱلصَّلَوةِ وَٱصْطَبِرْ عَلَيْهَا ۖ لَا نَسْـَٔلُكَ رِزْقًا ۖ نَّحْنُ نَرْزُقُكَ ۗ وَٱلْعَـقِبَةُ لِلتَّقْوَى ﴿٢٠:١٣٢﴾

Na waamrishe familia wako kusali, na uendelee mwenyewe kwa hayo. Sisi hatukuombi wewe riziki, bali Sisi ndio tunakuruzuku. Na mwisho mwema ni kwa mchamngu. (20:132)

Hii ina maana uikoe familia ya kutokana na adhabu ya Allah kwa kuiamrisha kusali, kuiamrisha familia kusali ndio ulikuwa mwennendo wa masahaba wengi wa Mtume (رضي الله عنهم), tuchukue mfano wa Umar ibn Al Khattab (رضي الله عنه) imesimuliwa: 

وَحَدَّثَنِي عَنْ مَالِكٍ، عَنْ زَيْدِ بْنِ أَسْلَمَ، عَنْ أَبِيهِ، أَنَّ عُمَرَ بْنَ الْخَطَّابِ، كَانَ يُصَلِّي مِنَ اللَّيْلِ مَا شَاءَ اللَّهُ حَتَّى إِذَا كَانَ مِنْ آخِرِ اللَّيْلِ أَيْقَظَ أَهْلَهُ لِلصَّلاَةِ يَقُولُ لَهُمُ الصَّلاَةَ الصَّلاَةَ ثُمَّ يَتْلُو هَذِهِ الآيَةَ {وَأْمُرْ أَهْلَكَ بِالصَّلاَةِ وَاصْطَبِرْ عَلَيْهَا لاَ نَسْأَلُكَ رِزْقًا نَحْنُ نَرْزُقُكَ وَالْعَاقِبَةُ لِلتَّقْوَى}

Amesimulia Maalik kutoka kwa Zayd ibn Aslam aliyesimulia kutoka kwa baba yake; Hakika Umar ibn Al Khattab alikuwa akisali mpaka mwisho wa usiku na aliwaamsha familia yake kusali alikuwa akiwambia “Salaah, Saalah, alwasomea aya Na waamrishe familia wako kusali, na uendelee mwenyewe kwa hayo. Sisi hatukuombi wewe riziki, bali Sisi ndio tunakuruzuku. Na mwisho mwema ni kwa mchamngu. (20:132) [Muwatta Malik, Mjeledi wa Tahajjud, mlango wa 7, Hadithi ya  259]

Aya hii ndio tunayoizungumzia hapo juu, na hivi ndivyo masahaba walivyoishi kuitekeleza Qur’aan kwa maneno na matendo. 

Faida ya kusimamisha na kuihiza familia kusimamisha salaah ni kubwa, lakini aya tunayoizungumzia imetaja faida moja., nayo ni:
لَا نَسْـَٔلُكَ رِزْقًا ۖ نَّحْنُ نَرْزُقُكَ

Sisi hatukuombi wewe riziki, bali Sisi ndio tunakuruzuku

Kuhusu sehemu hii ya aya t tutarjumu (kufasiri) maelezo ya Imam Ibn Kathir katika Tafsiri yake: “Hii ina maana ukisimamisha swali, utapata riziki kwa njia usizozitarajia” 
...وَمَن يَتَّقِ ٱللَّـهَ يَجْعَل لَّهُۥ مَخْرَجًا ﴿٢﴾ وَيَرْزُقْهُ مِنْ حَيْثُ لَا يَحْتَسِبُ ۚ وَمَن يَتَوَكَّلْ عَلَى ٱللَّـهِ فَهُوَ حَسْبُهُۥٓ ۚ إِنَّ ٱللَّـهَ بَـٰلِغُ أَمْرِهِۦ ۚ قَدْ جَعَلَ ٱللَّـهُ لِكُلِّ شَىْءٍ قَدْرًا ﴿٣﴾
...Na anaye mcha Mwenyezi Mungu humtengezea njia ya kutokea. (2) Na humruzuku kwa jiha asiyo tazamia. Na anaye mtegemea Mwenyezi Mungu Yeye humtosha. Hakika Mwenyezi Mungu anatimiza amri yake. Mwenyezi Mungu kajaalia kila kitu na kipimo chake. (65:2 -3)

Hivyo aya hii inathibitisha maelezo ya ibn Kathir kwamba pamoja na wajibu wetu wa kuitafuta riziki lakini kwa wenye taqwa na kutawakal basi Allah atawarahisishia riziki kwa njia wasizozitarajia. 

Hivyo ni muhimu kuhakikisha kwamba wanafamilia wote wanasali sala za faradhi na pia ni wajibu wako kuwahimiza kusali sala za sunnah. 

Hakika Allah ndio wakili katika kila tunalolifanya. 

Allah ndiye mjuzi zaidi

Maana Na Masharti 8 ya Hijaab

Hijaab ni amri ya Allaah ta’ala. Allaah ta’ala amefaradhisha hijaab katika aya mbali mbali nasi tutazizungumzia mbili tu, Allah ‘azza wa jall anatufahamisha katika Surat Al Ahzaab

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ قُل لِّأَزْوَاجِكَ وَبَنَاتِكَ وَنِسَاءِ الْمُؤْمِنِينَ يُدْنِينَ عَلَيْهِنَّ مِن جَلَابِيبِهِنَّ ۚ ذَٰلِكَ أَدْنَىٰ أَن يُعْرَفْنَ فَلَا يُؤْذَيْنَ ۗ وَكَانَ اللَّهُ غَفُورًا رَّحِيمًا
Ewe Nabii! Waambie wake zako, na binti zako, na wake za Waumini wajiteremshie nguo zao (Jalaabib zao). Hivyo ni karibu zaidi kuweza kutambulikana wasiudhiwe. Na Allaah ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu. [Qur’aan, Surat Al Ahzaab,  Aya  ya 59 (33:59)]

Hivyo hijaab ni amri ya Allaah ta’ala. Neno lililotumika kama vazi kwenye aya hii ni’jalaabib’ ambalo ni wingi wa jilbaab. Jilbaab ni guo refu lenye kunin’ginia lililo pana na la nje (Cowan, J.M., Dictionary of Modern Written Arabic, uk 153.)

Ili kufahamu maana halisi ya hijaab, namna inavyotakiwa kuvaliwa na lengo lake halisi basi ni lazima tuyafahamu masharti yake kwa ukamilifu. Awali kabla ya masharti tuzungumzie lengo la hijaab: Lengo la hijaab ni mwanamke kuhifadhika na kuiepusha jamii na fitna ya zinaa. Mwanamke ajifunike atakavyojifunika iwapo kujifunika huko hakutaihifadhi jamii kutokana na fitna hii basi hijaab yaikukamilika. Yaani iwapo kujifunika kwake kutamfanya bado awe kivutio chenye kupelekea kwenye kuzini au kuikaribia zinaa basi hiyo hijaaba haikutimia lengo. 

Sasa na tuingie kwenye masharti:

1. Ifunike mwili mzima isipokuwa zile sehemu zilizoruhusiwa.

Katika kuielezea aya iliyofaradhisha hijaab (33:59) Imam Ibn Kathir ameelezea katika maelezo ya tafsiri yake kwamba, ninanukuu

أي : لا يظهرن شيئا من الزينة للأجانب إلا ما لا يمكن إخفاؤه ،
Hii ina maana wanawake hawatakiwi kuonyesha sehemu yoyote ya mapambo (sio tu mwili) kwa watu wasio mahrim wao, isipokuwa zile sehemu ambazo haziwezekani kufunikwa (mfano macho au baadhi ya wamazuoni wameeleza kuwa ni uso na viganja)

2. Isiwe ni pambo au kivutio.

Amri ya kuwa hijaab isionyeshe uzuri,  au isiwe ni pambo inapatikana kwenye surat An Nuur, Allaah (عز وجل) anatuambia:

…لَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا لِبُعُولَتِهِنَّ أَوْ آبَائِهِنَّ أَوْ آبَاءِ بُعُولَتِهِنَّ أَوْ أَبْنَائِهِنَّ أَوْ أَبْنَاءِ بُعُولَتِهِنَّ أَوْ إِخْوَانِهِنَّ أَوْ بَنِي إِخْوَانِهِنَّ أَوْ بَنِي أَخَوَاتِهِنَّ أَوْ نِسَائِهِنَّ  …
…Na waangushe shungi zao juu ya vifua vyao, wala wasionyeshe uzuri wao ila kwa waume zao, au baba zao, au baba wa waume zao, au watoto wao, au watoto wa waume zao, au kaka zao, au wana wa kaka zao, au wana wa dada zao, au wanawake wenzao… [24:1]

Hivyo ni wazi hijaab yenye mapambo au yenye kuvutio inavunja amri hii ya Allaah (عز وجل). Hali ya siku hizi ni kinyume, yaani wanawake wanapokuwa na waume zao ndio hawajipambi, lakini wanapotoka nje ambapo huonekana na wasio mahrim wao ndio hujipamba. 

3. Isiwe ni yenye kuonyesha (transparent au translucent)

يقول صلى الله عليه وسلم : "سيكون في آخر أمتي نساء كاسيات عاريات على رؤوسهن كأسنمة البخت العنوهن فإنهن ملعونات " زاد في حديث آخر :"لا يدخلن الجنة ولا يجدن ريحها وإن ريحها لتوجد من مسيرة كذا وكذا  رواه مسلم من رواية أبي هريرة .
Amesema Mtume (صلي الله عليه وسلم)  katika siku za mwisho za umma kutakuwa na wanawake ambao wamevaa lakini wapo utupu, vichwani mwao watakuwa na vitu mfano wa nundu ya ngamia (yaani jinsi watakavyozifunga nywele zao), walaanini kwani wamelaaniwa na katika hadithi nyingine “hawataingia peponi or hata kusikia harufu yake wakati harufu yake itasikika kwa masafa kadhaa wa kadhaa (marefu) [Imenakiliwa na Muslim katika riwaya ya Abuu Huraira]

Katika kuifafanua hadithi hii hasa yale maneno wamevaa lakini wako utupu imeelezwa:
قال ابن عبد البر :  أراد صلى الله عليه وسلم النساء اللواتي يلبسن من الثياب الشيء الخفيف الذي يصف لا يستر فهن كاسيات بالاسم عاريات في الحقيقة . نقله السيوطي في تنوير الحوالك (3/103)
Amesema  ibn Abul Barr alichokimaanisha  Mtume (صلي الله عليه وسلم)  ni kuwa .wanawake ambao wamevaa nguo ambazo ni za kitambaa chepesi au hazistiri inavyotakiwa. Wamevaa lakini wako utupu. [as-Suyuti katika Tanwiyr al-Hawaalik, 3/103.]

Kwanza kabisa hadithi hii imetudhihirishia kuwa wanawake ambao hawavai hijabu ipasavyo basi wamelaaniwa na Mtume (صلي الله عليه وسلم)  ametumrisha tuwalaani. huu ndio uzito wa kuidharau au kuiacha hijaab, na mwenye kulaaniwa basi maskani yake ni motoni. Dalili kubwa za wanawake hawa ni mbili:

Hijaab zao hazitowastiri (wamevaa lakini wako utupu)
Nywele zao zitatengenezwa au kusukwa kwa mitingo yenye kuzinyanyua kama nundu ya ngamia.
Haya hoye siku hizi tunayaona usiku na mchana, tena wanawake hawa hata wasi wasi hawana wanapofanya jambo hili lenye kupelekea wao kupata laana.


4. Isiwe ni yenye kubana na kufuata sehemu yoyote ya umbo

Turudie tena kuwa lengo la hijaab ni kuepusha fitna kwa hiyo iwapo nguo inabana au kuonyesha maumbile basi baso ni yenye kuleta fitna hivyo haitimizi lengo la hijaab. Hivyo hijaab iwe ni nguo ambayo haitoi taswira ya maumbile ya mwanamke kwa ukubwa au udogo wa sehemu yoyote.

Usama ibn Zayd amesema Mtume (صلي الله عليه وسلم)  amenipa guo la Kimasri kama zawadi ambayo alipewa na Duhya al Kalbi, nikampa mke wangu aivae. Akasema [Mtume (صلي الله عليه وسلم)] Mbona sikuoni kulivaa lile guo la Kimasri? Akasema (Usama) nimempa mke wangu alivae. Akasema [Mtume (صلي الله عليه وسلم)] akasema Mwambie avalie nguo nyingine kwani nakhofia huenda ikaonyesha maumbile yake ukubwa wa mifupa [Imesimuliwa na al-Diyaa’ al-Maqdisi katika al-Ahaadeeth al-Mukhtaarah, 1/442, na Ahmad pamoja na al-Bayhaqi, na isnaad yake ni hasan)

Hivyo ni wazi kuwa usia wa Mtume (صلي الله عليه وسلم)  katika riwaya hii ni ushahidi wa kutosha kuwa haifai nguo kuwa ni yenye kubana au kuonyesha umbo.  

5. Isitiwe manukato wala kufukizwa

Kuna hadithi nyingi za Mtume (صلي الله عليه وسلم)  zinazokataza wanawake kujitia manukato wanapotoka nje. Tutanukuu baadhi ambazo zina isnaad zilizo sahihi:

عن أبي موسى الأشعري قال : قال رسول الله صلى الله عليه وسلم :"أيما امرأة استعطرت فمرت على قوم ليجدوا من ريحها فهي زانية "
Abuu Musa al Ash’ari amesema: Kasema Mtume (صلي الله عليه وسلم)  mwanamke yoyte anayejitia manukato na kupita mbele za watu basi ni mzinifu.

عن زينب الثقفية أن النبي صلى الله عليه وسلم قال : " إذا خرجت إحداكن إلى المسجد فلا تقربن طيبا ".
Zaynab ath Thaqafiya ameripoti kwamba Mtume (صلي الله عليه وسلم)  amesema: Yoyote kati yenu enyi wanawake anapokwenda msikitini basi asiguse manukato.

أبي هريرة قال : قال رسول الله صلى الله عليه وسلم : " أيما امرأة أصابت بخورا فلا تشهد معنا العشاء الآخرة " .
Abu Hurayra amesema: Kasema Mtume (صلي الله عليه وسلم): Mwanamke yoyote aliyejifukiza basi asije kusali nasi sala ya ‘Isha. 

Hivyo katazo la kujifukiza lipo kwenye nguo na hata mwili pale mwanamke anapotoka nje. Kujifukiza na kujitia manukato kunasihi pale mwanamke anapotaraji kukutana na mume wake na sio walio haramu kwake.

6. Isifanane na mavazi ya kiume

Kuna hadithi kadhaa ambazo zinathibitisha kwamba mwanamke anapovaa kujifananisha na mwanamme basi mwanamke huyo amelaaniwa, na pia mwanamme anayejifananisha kimavazi na mwanamke pia nae amelaniwa:
عن أبي هريرة قال:" لعن رسول الله صلى الله عليه وسلم الرجل يلبس لبسة المرأة، والمرأة تلبس لبسة الرجل" .
Abu Hurayra (Allah amuwie radhi) amesema, Mtume (صلي الله عليه وسلم)  amemlaani mwanamume anayevaa nguo za kike na mwanamke anayevaa nguo za kiume.

عن عبد الله بن عمرو قال: سمعت رسول الله صلى الله عليه وسلم يقول" ليس منا من تشبه بالرجال من النساء، ولا من تشبه بالنساء من الرجال" .
Amesema Abdullah ibn ‘Amr: Nimemsikia Mtume (صلي الله عليه وسلم)  akisema; “Si miongoni mwetu wanawake wenye kujifananisha na wanaume na wanaume wanaojifananisha na wanawake.


7. Isifanane na mavazi ya wanawake wa kikafiri

Sharia ya kiislamu inaeleza wazi kuwa waislamu wanawake na wanaume wasijifananishe au kuwaiga makafiri katika ibada, sherehe na mavazi yao.Hii ni kanuni muhimu lakini kwa bahati mbaya siku hizi inapuuzwa wa waislamu wengi. Hali hii inatokana na waislamu kutokuwa na elimu, kufuata matakwa ya nafsi zao, au kuacha kuifuata dini. Lakini huchngiwa zaidi na waislamu kujichanganya na mila ambazo kwa asili ni mila za kikafiri hasa wa bara la Ulaya na Amerika. 

Uislamu ni dini iliyokamilika, laiti ingelikuwa dini iliyokosa mila yake wenyewe basi isingelikuwa ni dini liyokamilika, katika kuufikia ukamilifu huo, Allaah (عز وجل) ametuamrisha katika Qur’aan kuhusu mila kwamba:

 بَلْ مِلَّةَ إِبْرَاهِيمَ حَنِيفًا ۖ وَمَا كَانَ مِنَ الْمُشْرِكِينَ 
…Bali tunashika mila ya Ibrahim mwongofu, wala hakuwa katika washirikina. [2:135]

Bila ya shaka tutakuwa ni wenye kukubaliana kuwa hakuna mavazi ni sehemu ya mila.Tena aya hii inamalizia kuwa Ibrahim hakuwa katika washirikina katika mila yake. Hivyo basi bila ya shaka yoyote ikiwa sisi ni wenye kumfuata baba yetu Ibrahim Mtume (عليه سلم) hatuna budi kuifuata mila yake ya uongofu ilijitenganisha na mila za kikafiri.

Kufuata mila za kikafiri ni moja kati ya sababu ya umma wa Waislamu leo kuwa ni umma dhaifu, kwani kufuata mila za kikafiri kumewafanya waislamu kuwa ni watumwa wa kifikra. Hili halitoondoshwa kwetu mpaka tutakapozibadili nafsi zetu. Kwani Allaah (عز وجل) anatuambia kwamba katika kitabu chake kitukufu:
…إِنَّ اللَّـهَ لَا يُغَيِّرُ مَا بِقَوْمٍ حَتَّىٰ يُغَيِّرُوا مَا بِأَنفُسِهِمْ…
…Hakika Mwenyezi Mungu habadili yaliyoko kwa watu mpaka wabadili wao yaliyomo naf- sini mwao… [13:11]

8. Isiwe ni nguo ya kujifakharisha au kujionyesha 

Kujifakhari si hulka miongoni mwa hulka za kiislamu kwani Allaah (عز وجل) ameweka wazi kwenye Qur’aan kuwa Yeye si mwenye kuwapenda kila wenye kupenda kujifalharisha, pale alipotueleza kwenye surat al Luqmaan:
إِنَّ اللَّـهَ لَا يُحِبُّ كُلَّ مُخْتَالٍ فَخُورٍ
Hakika Mwenyezi Mungu hampendi kila anaye jivuna na kujifakhirisha. [31:18]

Hivyo nguo za kufakharisha na kujivuna si nguo ambazo zinaendana na mila na desturi za kiislamu, kwame muislamu haifai kuvaa kwa lengo la kutafuta kujifakharisha kwani kujifakharisha ni kwenye kumchukiza Allaah (عز وجل). Pia tunafunzwa na Mtume (صلي الله عليه وسلم)  juu ya mavazi ya kifakhari kwamba:

فلحديث ابن عمر رضي الله عنه قال: قال رسول الله صلى الله عليه وسلم " من لبس ثوب شهرة في الدنيا ألبسه الله ثوب مذلة يوم القيامة ثم ألهب فيه ناراً

Amesimulia Ibn Umar (رضي الله عنهم): Amesema Mtume (صلي الله عليه وسلم)  kwamba: “Yoyote atakaevaa kwa ajili ya umaarufu na fakhari ya Dunia, Allaah atamvalisha guo la kumdhalilisha siku ya qiyama, na atamfanyia moto utakaomzunguka”

Siku 10 ambazo Allaah anapenda matendo mema

Shukrani zote zinamstahiki Allah na rehma na amani zimshukie Mtume Muhammad, watu wake, na masahaba wake na wale wote wenye kufuata mwenendo wake mpaka siku ya qiyama. 

Dhul Hijjah ni mwezi miongoni mwa miezi ya Allah, ni mwezi ambao una ibada muhimu kabisa, ambayo ni nguzo ya tano ya kiislamu isiyopatikana katika mwezi mwengine wowote. Mbali na ibada ya hijjah, siku kumi za mwanzo katika mwezi huu ni siku maalum, ni siku zenye fadhila kubwa, kama inavyonukuliwa katika hadithi iliyosimuliwa na Ibn Abbaas:

عن ابن عباس رضي الله عنهما، أن النبي صلى الله عليه وسلم قال: ((مَا مِنْ أَيَّامٍ الْعَمَلُ الصَّالِحُ فِيهَا أَحَبُّ إِلَى اللَّهِ مِنْ هَذِهِ الْأَيَّامِ)) يَعْنِي أَيَّامَ الْعَشْرِ قَالُوا:  يَا رَسُولَ اللَّهِ وَلَا الْجِهَادُ فِي سَبِيلِ اللَّهِ؟  قَالَ: ((وَلَا الْجِهَادُ فِي سَبِيلِ اللَّهِ إِلَّا رَجُلٌ خَرَجَ بِنَفْسِهِ وَمَالِهِ فَلَمْ يَرْجِعْ مِنْ ذَلِكَ بِشَيْ)) البخاري

Imetoka kwa Ibn Abbaas (radhi za Allah zimshukie) kwamba Mjumbe wa Allaah amesema: <<Hakuna siku ambazo vitendo vyake vyema Anavipenda Allaah kama siku kumi hizi>> (siku kumi za mwanzo wa mwezi wa Dhul-Hijjah) Akaulizwa, je, hata Jihaad katika njia ya Allaah? Akajibu (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ((Hata Jihaad katika njia ya Allaah isipokuwa mtu aliyekwenda na nafsi yake na mali yake ikawa hakurudi na kimojawapo)) [Al-Bukhaariy].

Hivyo basi Allaah ta’ala anapendezewa sana na ibada zifanywazo katika siku kumi za Dhul Hijjah, Mtume (rehma na amani juu yake) amezipa ubora ibada zifanywazo katika siku kumi hizi kuliko hata jihaad, ukiondoa yule ambaye amekufa shahid na pia metumia mali zake kwa ajili ya jihaad. Tukizingatia wengi miongoni mwetu hatukupata bahati ya kuwa katika jihaad, basi siku kumi hizi hatuna budi kufanya juhudi kubwa katika utekelezaji wa ibada. 

Allaah ‘azza wa jall amezipia siku kumi hizi katika surat al Fajr, pale Allah alopotuambia:
وَالْفَجْرِ 
وَلَيَالٍ عَشْرٍ 
Naapa kwa Alfajiri
Na kwa masiku kumi (Al-Fajr: 1-2)
Hivyo kwa kuziapia siku hizi, Allah ‘azza wa jall amezitukuza. Pia mbali na ibada ya Hijjah katika siku kumi hizi kunapatikana siku ya ‘Arafa, ambayo ni ya tisa ya mwezi wa Dhul Hijjah. Kufunga katika siku tisa za mwanzo za mwezi wa Dhul Hijjah ni sunna miongoni mwa sunna kubwa za mwezi huu. 

وعن هنيدة بن خالد عن امرأته عن بعض أزواج النبي صلى الله عليه وسلم قالت : ( كان رسول الله صلى الله عليه وسلم يصوم تسع ذي الحجة ويوم عاشوراء وثلاثة أيام من كل شهر أول اثنين من الشهر وخميسين ) رواه الإمام أحم ، وصححه الألباني 

Kutoka kwa Hunaydah ibn Khaalid aliyesimulia kutoka kwa mkewe ya kwamba mmoja kati ya wake za Mtume amesema: << Mtume rehma na amani juu yake alikuwa akifunga siku tisa za Dhul Hijjah na siku ya ‘Ashura na siku tatu za kila mwezi, na Jumatatu ya mwanzo na Alkhamisi mbili (Imesimuliwa na Imam Ahmad na Imam Albani amesema kuwa ni hadithi sahihi)

Hivyo basi kwa wale ambao hawakujaaliwa kwenda Hijjah kufunga siku tisa za mwanzo ni ibada ambayo imesunniwa. Pia tukumbuke kuwa ni haram kufunga siku ya ‘Idi. Kwa ibada zaidi za kutekeleza katika mwezi huu fuata link hii siku 10 za mwezi wa Dhul Hijjah, tunamalizia kwa kukumbusha tena maneno ya Mtume (rehma na amani juu yake kwamba “Hakuna siku ambazo vitendo vyake vyema Anavipenda Allaah kama siku kumi hizi”

SIKU KUMI ZA MWEZI WA DHUL HIJJAH


USIPITWE NA FURSA HII: Anasema mtume wa Allah rehema na amani ziwe juu yake, (Hakuna siku ambazo matendo mema ndani yake ni yenye kupendezwa zaidi mbele ya Allah kulikoni Siku hizi (siku kumi za mwezi wa Dhul Hijja) Maswahaba wakauliza: Ewe mtume wa Allah: Wala Jihadi kwa ajili ya njia ya Allah?
Akawajibu: Wala jihadi kwa ajili ya njia ya Allah, Isipokuwa kwa yule mtu aliyetoka na nafsi yake na mali zake kisha kikawa hakijarudi chochote katika hivyo (nafsi na mali). Hadithi imesimuliwa na Ibun Abbasi radhiya Allahu anhumaa na kupokelewa na Abu Dawud na Ibn Majah.
JE MATENDO HAYO YANAYO PENDEZWA KUYAFANYA NDANI YA SIKU HIZI NI YAPI?
  1. KUFANYA IBADA YA HIJJAH NA UMRA: Kama anavyo tueleza Mtume rehema na amani ziwe juu yake: (Ibada ya umra mpaka ibada ya umra ni kifutio cha madhambi yaliyo kati yake, na ibaada ya hijja iliyo kamilisha nguzo zake na masharti yake, haina malipo isipokuwa pepo) 
  2. KUFUNGA SIKU HIZI ZOTE TISA AU KADIRI YA UWEZO KHUSUSANI SIKU YA TISA SIKU YA ARAFA: Bila shaka ibada ya swaumu ni katika ibaada zenye thawabu mbele ya Allah Azza Wajalla na katika hadithi zilizokuja kuelezea umuhimu na fadhila za swaumu ni hadithi hii ya Mtume salla Allahu alayhi wasallam: (Mwenye kufunga siku moja kwa ajili ya Allah basi Mwenyezi Mungu utauweka uso wake mbali na moto wa jahanamu muda wa miaka sabini) Na kuhusiana na fadhila za kufunga siku ya Arafa mtume anatueleza ya kwamba: (Funga ya siku ya Arafa ninatarajia Allah atawafutia waja madhambi ya mwaka ulio pita na mwaka ujao) 
  3. Kuzidisha adhkari: Nyiradi mbali mbali katika siku hizi kumi, kama vile Takbira (ALLAHU AKBARU:Mungu mkubwa) ALHAMDULILLLAHI: Shukurani zote anastahiki Mwenyezi Mungu. ISTIGHFARI: Kumtaka msamaha Mwenyezi Mungu. Na mfano wa hizo katika adhkari zilizo pokelewa katika mwongozo wa mtume wetu Muhamadi rehema na amani ziwe juu yake. 
  4. KUTUBIA KWA ALLAH NA KUJING`OA KUTOKA KATIKA MAASI YOTE. Kwani utiifu (Kumtii Allah) ni katika sababu za kumfanya mja awe karibu na Allah na maasi au madhambi ni katika mambo yanayo muweka mja mbali na Allah. Na toba ni katika mambo yanayo mfurahisha Allah. 
  5. KUZIDISHA KUFANYA MAMBO YA KHERI: Kama vile kuswali swala zote kwa nyakati zake. Vile vile kuzidisha ibaada za suna na kutoa sadaka na kuamrishana mambo mema, kukatazana maovu na kadhalika
  6. KUCHINJA SIKU YA IDDI EL ADH-HA: Kwa kumuiga kigezo chetu na mtume wetu Nabii Ibrahimu alayhi salaam. Na mtume wetu Muhammad rehma na amani ziwe juu yake. Ibada hii ya kuchinja ni ibaada ya sunna na wanyama wanao faa kuwachinja ni ngamia, ng`ombe, mbuzi na kondoo. Ngamia au ng`ombe wanaweza changia watu saba, ama mbuzi na kondoo ni kwa mtu mmoja tu. Mnyama huyu inapaswa asiwe na kasoro kama vile uchongo upofu na kilema. 
  7. KWA MWENYE KUTAKA KUCHINJA NDANI YA SIKU YA IDDI: Basi ni sunna kwa mtu huyu asinyoe nywele zake na kukata kucha zake mpaka siku ya kuchinja.
  8. KUJITAHIDI KUSWALI IBADA YA SWALA YA IDI: Kwani ibaada hii kwa mwaka ni mara moja tu,kwa hiyo ni muhimu kujitahidi kutekeleza ibaada hii.

Masjid Abdullah Quilliam - Msikiti wa Kwanza Uingereza


Masjid Abdullah Quilliam ndio msikiti wa kwanza nchini Uingereza. Miskiti huu ulikuwa jengo lililonunuliwa na William Henry Quilliam aliyesilimu nchini Morocco na kuitwa Abdullah akiwa na umri wa miaka 17. Pia Abdullah Quilliam alikuwa mwandishi wa kwanza wa jarida la Kiislamu Uingereza. Jarida hili lilijulikana kama "Mwezi Muandamo" (The Cresent). Jarida hili lilitafsiriwa katika lugha 13 tofauti ambapo lilipelekea Sheikh Abdullah Quilliam kupata umaarufu mkubwa katika Ulimwengu wa Kiislamu.

Historia fupi ya msikiti huu ni kwamba ulianzishwa mwishoni mwa karne ya 18 (mwaka 1889) katika mji wa Liverpool na kuwepo kwa jamii ya kwanza ya Kiislamu katika mji huo. Mwanzilishi wa jamii hiyo Sheikh Abdullah Quilliam mara kwa mara alimtembelea khalifah wa mwisho wa Kiislamu wa Khilafatul Uthmaaniya, Abdulhamid wa pili huko nchini uturuki, ambaye alikuwa ni rafiki wa Sheikh Abdullah Quilliam. Pia katika msikiti huo palikuwa na Chuo cha Kiislam kilichoongwa na Nasrullah Warren.

Katika moja ya safari zake kwenda Uturuki Abdullah Qulliam alikaa muda mrefu akisoma Uislamu, aliporudi Uingereza alikuta jamii aliyoisilimisha imeuhama mji wa Liverpool, bila ya shaka kutokana na madhila makubwa waliyotapata, Waislamu hao walihamia mji wa Working ulioko kusini mwa Uingereza, Abdullah Qulliam nae aliwafuata Waislamu wenzake katika mji huo.

Kufuatia kuhama kwa jamii hii ya Waislamu msikiti wa Abdullah Quilliam ulikufa na kubaki kuwa "gofu". Hivi karibuni Waislamu wa UK wameanzisha "Abdullah Quilliam Society" kwa  lengo la kufufua msikiti  huu na kuanzisha makumbusho ya kuenzi kazi alizozifanya Sheikh Abdullah Quilliam. Pia sehemu hii itafanywa kuwa ni kitivo cha elimu na mijadala ya kidini.  Kitivo hicho kwa sasa kipo katika ujenzi na kitakapo kamilika kabisa kitakuwa kimegharimu zaidi ya paundi milioni mbili na nusu.

Idadi ya watu waliosilimishwa na Sheikh Abdullah inasadikiwa kufikia watu 600, ambapo Kitivo hicho kipya pia kanakusudia kufanya utafiti juu ya maisha ya Waislamu hao. 

Sheikh Abdullah Quilliam pia alimsilimsha Abdulhalim Nodda, mjapani wa kwanza katika nyakati zetu kusilimu, Sheikh Nodda naye pia ameacha athari kubwa nzuri ya Uislamu huko Japan.

Allah amremehu Sheikh Abdullah Henry Quilliam aliyefariki akiwa na umri wa miaka 76, ambapo alikuwa ni muislamu wa kwanza kutangaza Uislamu wazi wazi nchini UK kwa karne za karibuni.

Tathmini Baada ya Ramadhani

Tunamshukuru kwa dhati kabisa Allah sub-hanahu wa ta'ala kwa kutuwezesha kufika tulipo fika katika mwezi huu wa Ramadhani, pia rehma na amani zimshukie Mtume, pamoja watu wake na sahaba zake na wale wote wenye kufuata mwenendo wake mpaka siku ya qiyama. Na tunashuhudia kwamba hapana Mola anayestahiki kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allah na Muhammad ni mja na Mtume wake.

Mwezi mtukufu wa Ramadhani ndio umefikia ukingoni, wengi ni wenye huzuni kwani ingawa ni mwezi mmoja tu, wamejenga mazoea makubwa ya kufanya mambo mbali mbali ambayo hatuyapati katika miezi mingine, mikusanyiko ya pamoja katika milo ya iftaar, misikiti kujaa, itikafu, qiyamul layl  na du’a za kuomba maghfira kama vile
 (اللَّهُمَّ إِنَّكَ عَفُوٌّ تُحِبُّ الْعَفْوَ فَاعْفُ عَنِّيْ)
Haya ni baadhi tu ya mambo ambayo wengine yanawatoa machozi kwani hatuna uhakika wa kuwa hai mpaka mwezi wa Ramadhani mwakani.

Laylatul Qadr


Laylatul Qadr kilugha, maana yake ni usiku wenye nguvu au usiku wenye kudra au usiku wa cheo kitukufu, ni usiku maalum ambao unapatikana mara moja tu katika kila mwaka ndani ya mwezi wa Ramadhani. Huu ni usiku ambao Allaah ta’ala anatuambia  katika kitabu chake kitukufu kuwa Qur’ani imeteremshwa, Allaah ta’ala  anatuarifu:-

إِنَّا أَنزَلْنَاهُ فِي لَيْلَةِ الْقَدْرِ
Hakika Sisi tumeiteremsha (Qur'ani) katika Laylatul Qadri, Usiku wa Cheo Kitukufu.
Kama tunavyofahamu kuwa Qur’ani ni kitabu ambacho kina faida nyingi ndani yake ikiwa ni pamoja na kuwa ni muongozo kwa wenye taqwa, ni shifaa kwa wenye kuiamini, ni maelekezo ya maisha sahihi kwa wenye kukifata ni chanzo mama cha sharia za Allaah ta’ala kwa waislamu na wanaadamu kwa ujumla. Bila shaka usiku huu unastahiki kuwa na hadhi kubwa. Kuhusu uteremkaji huo wa Qur’ani Ibn Abbas (radhi za Allaah ziwe juu yake) anasema:-
Allaah ameishusha Qur’ani yote ikiwa imehifadhiwa kwenye al Lahwul mahfudh kwenda kuwekwa kwenye Baytul ‘izza ambayo ipo kwenye mbingu ya dunia. Kisha ikaletwa kwa Mtume sehemu baada ya sehemu kwa mujibu wa matukio kwa muda wa miaka ishirini na tatu.
Mtume rehma na amani juu yake ameuzungumzia usiku huu katika hadithi mbali mbali. Kama hii ilivyosimuliwa na Abuu Hurayra:-
 عن أبي هريرة ، قالَ : كَانَ رسولُ اللهِ صلي الله عليه وسلم يُبَشِّرُ أصْحَابَةُ ، يقولُ : " قَدْ جَاءَكُمْ شَهْرُ رَمَضانَ شَهْرٌ مُبَارَكٌ فَرَضَ اللهُ عليكم صِيَامَهُ ، تُفَتَّحُ فيه أبوابُ الجَنَّةِ ، وَتغلَّقُ فيه أبوابُ النَّارِ ، فيه لَيْلَةٌُ خَيْرٌ من ألفِ شَهْرٍ ، مَن حُرِمَ خَيْرَها فقد حُرِمَ "
Imetokana na Abu Hurayra (radhi za Allaah ziwe juu yake) amesema: Amekuja Mtume rehma na amani juu yake na kuwabashiria maswahaba na kasema “Umekujieni mwezi wa Ramadhani, mwezi wenye baraka, Allaah amekufaradhishieni ndani yake kufunga, hufunguliwa ndani yake milango ya peponi na hufungwa milango ya motoni, ndani yake kuna usiku ulio bora kuliko miezi elfu, atakaekosa kheri zake basi amenyimwa
Pia ubora wa usiku huu umethibitishwa katika Qura’ni pale Allaah ‘azza wa jall anapotuambia:-
لَيْلَةُ الْقَدْرِ خَيْرٌ مِّنْ أَلْفِ شَهْرٍ
تَنَزَّلُ الْمَلَائِكَةُ وَالرُّوحُ فِيهَا بِإِذْنِ رَبِّهِم مِّن كُلِّ أَمْرٍ
Laylatul Qadri ni bora kuliko miezi elfu.
Huteremka Malaika na Roho katika usiku huo kwa idhini ya Mola wao Mlezi kwa kila jambo.
Mbali na kuwa na ubora kuliko miezi elfu pia kwa idhini yake Allaah ta’ala huteremshwa malaika katika usiku huo kutokana na wingi wa kheri za usiku huo. Vile vile Mtume rehma na amani zimshukie ameuzungumzia usiku huu kuwa ni usiku wa kusamehewa dhambi, kama ilivyoelezewa katika hadithi ifuatayo:- 
عَنْ  أَبِيْ هُرَيْرَةَ  رَضِيَ الْلَّهُ عَنْهُ ‏عَنْ الْنَّبِيِّ  صَلَّىَ الْلَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ  قَالَ  مَنْ قَامَ لَيْلَةَ الْقَدْرِ إِيْمَانا وَاحْتِسَابا غُفِرَ لَهُ مَا تَقَدَّمَ مِنْ ذَنْبِهِ 
Amesimulia Abu Hurayra kwamba amesema Mtume rehma na amani juu yake “mwenye kusimama katika laylatul qadr kwa imani na kutaraji malipo atasamehewa dhambi zake zote zilizotangulia.
Kusamehewa dhambi ni kitu ambacho kila binadamu anakihitaji kwa vile sote ni watenda dhambi. Hii ni neema kubwa kwa Waislamu kwa hiyo hatuna budi kujitahidi kusimama kwenye ibada katika kuutafuta usiku wenye ubora wa hali ya juu na neema nyingi.
Usiku huu unapatikana katika usiku witiri wa kumi la mwisho la mwezi huu ambapo sasa zimebaki siku chache tu kama anavyotuthibitishia Mtume rehma na amani juu yake:-
 عَنْ عُبَادَةَ بْنِ الصَّامِتِ , أَنّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ , قَالَ : " لَيْلَةُ الْقَدْرِ فِي الْعَشْرِ الْبَوَاقِي , مَنْ قَامَهُنَّ ابْتِغَاءَ حِسْبَتِهِنَّ فَإِنَّ اللَّهَ يَغْفِرُ لَهُ مَا تَقَدَّمَ مِنْ ذَنْبِهِ , وَهِيَ لَيْلَةُ وِتْرٍ تِسْعٌ أَوْ سَبْعٌ أَوْ خَمْسٌ أَوْ ثَلاثٌ أَوْ آخِرُ لَيْلَةٍ " .
Imetokana na ‘Ubada bin As Swaamit (radhi za Allaah zimshukie) Hakika Mtume rehma na amani juu yake amesema: “Laylatul Qadr inatokea katika mwezi wa ramadhani katika kumi la mwisho, mwenye kusimama kwa imani na matarajio basi hakika Allaah atamsamehe dhambi zote zilizotangulia, nao ni usiku wa witiri, ama tisa au saba au tano au tatu au usiku wa mwisho.
 Huu ndio uthibitisho wenye uhakika juu ya ni lini usiku huu unapatikana kinyume na ile itikadi isiyo sahihi kwamba usiku huo ni usiku wa kuamkia ramadhani ya ishirini na saba.
Hivyo basi ni muhimu sana kwetu sisi waislamu kuendelea kufanya ibada katika siku zilizobaki za kumi hili ili kwa rehma zake Allaah tukawa ni wenye kuupata usiku huu na Allaah kutukubalia dua, istigfaar, toba na ibada zote nyingine.  Tunamuomba Allaah atukubalie funga zetu, sala zetu, du’aa zetu na atutenge sisi na madhambi kama ilivyotengana mashariki na magharibi.


1 Qur’ani Suratul Qadr aya ya 1 (97:1)


2 Qur’ani, Suratul Baqara aya ya 2 (2:2)


3 Ni kifaa maalum (mfano wa tableti au ubao) ambapo Qur’ani yote iliandikwa na kuhifadhiwa kwenye kifaa hicho .


4 Baytul ‘izza ni nyumba tukufu iliyoko kwenye nbingu ya dunia ambapo Qur’ani ikiwa kwenye Lahwul Mahfudh ilihifadhiwa kwenye nyumba hiyo.


5 Maelezo haya ya Ibn Abbas yanapatikana kwenye Tafsiri ya Ibn Kathir katika maelezo ya aya ya kwanza ya Suratul Qadr. 


6 Imenakiliwa kwenye Sahihi Bukhari .


7 Imenakiliwa kwenye Sahihi Bukhari.


8 Hadithi hii umekaririwa kwenye maelezo ya tafsiri ya ibn Kathir ya Surat al Qadr. 

Kufuru Katika Fizikia


Shukrani zote zinamstahiki Allaah Mola mlezi wa viumbe wote. Rehma na amani zimshukie Mtume wetu na ali zake, masahaba wake na wote wenye kufuata mwenendo wake mapaka siku ya Qiyama.


Kwa wale waliobobea kwenye somo la fizikia wanatambua kuwa kuna kauli maarufu inayosema “Energy can neither be created nor destroyed” katika ile nadharia maalum ya relativity (special theory of relativity), ambapo energy inalingwanishwa na mass katika ile formula maarufu ya E = mc2 (Energy = Mass x Speed Square), Nadharia hii imeandikwa na mwanasayansi maarufu anayeaminiwa kuwa na akili kuliko kupindukia Albert Einstein. 

Kauli hii yenye maana "Nishati haiwezi kuumbwa wala haiwezi kuharibiwa" ni shirki katika Rubuubiyyah ambayo ni kinyume cha Tawhid ar Rubuubiyyah. Abapo Tawhid ar Rubuubiyyah maana yake kwa kifupi ni kumpwekesha Allaah katika kuumba na kuviendesha (kuviendeleza au kuvipa maisha) alivyoviumba. Hivyo kusema nishati haikuumbwa ni kosa na ni kinyume na mafundisho wa kiislamu kwa sababu Allaah anatuambia katika Qur'aani tukufu kwamba:

اللَّهُ خَالِقُ كُلِّ شَيْءٍ وَهُوَ عَلَى كُلِّ شَيْءٍ وَكِيلٌ


Allah ndiye Muumba wa kila kitu na yeye ndiye Mlinzi wa kila kitu (39:62)

Mjue Nabii Yush'a Bin Nuun [يوشع بن نون عليه السلم]

Kaburi la Nabii Yush'a Bin Nuun (عليه السلم)
Shukrani zote zinamstahiki Allaah Mola Mlezi wa viumbe wote. Rehma na amani zimshukie Mtume  Muhammad, na watu wake, na masahaba wake na wale wote wenye kufuata mwenendo wake mpaka siku ya qiyama.

Nabii Yush'a Bin Nuun (عليه السلم) ni miongoni mwa manabii tunaowajua kupitia hadithi, kwa vile nabii huyu hakutajwa  kwenye Qur'aani tukufu kwa jina. Lakini Nabii Yush'a Bin Nuun ametajwa kwa kuwa kwake pamoja na Nabii Musa pale Allaah (عز وجل) alipoatumbia katika Surat Al Kahfi:

وَإِذْ قَالَ مُوسَىٰ لِفَتَاهُ لَا أَبْرَحُ حَتَّىٰ أَبْلُغَ مَجْمَعَ الْبَحْرَيْنِ أَوْ أَمْضِيَ حُقُبًا

Na pale Musa alipo mwambia kijana wake: Sitoacha kuendelea mpaka nifike zinapo kutana bahari mbili, au nitaendelea kwa muda mrefu. (18:60)

Akiielezea aya hii Imam Ibn Kathir (Allaah amrehemu) anasema "Sababu mazungumzo ya musa na mjakazi kijana wa kiume Yush'a Bin Nuun…" Hivyo basi "Kijana wake" katika aya hii ni Nabii Yush'a bin Nuun (عليه السلم). Nabii Yu'sha  ndiye aliyechukua uongozi wa Banii Israil mara baada ya Allaah kumchukua Nabii Haarun na  Musa  (amani iwe juu yao).

Kwa mujibu wa wana taarekh wa kiislamu Nabii Yu'sha katika damu ya utume ni kitukuu cha Nabii Yusuf (عليه السلم) Jina lake kamili ni Yu'sha Bin Nuun Bin Afraiym bin Yusuf. Nabii Yush'a alikuwa ni mtumishi wa Nabii Musa (عليه السلم), aliwaongoza Bani Israil katika Jihaad ya kuuteka mji wa Ariha ulioko upande wa pili wa mto Jordan kutoka muelekeo wa Bani Israil waliokuwa wakitokea Misri. 

 Nabii Yu'sha (عليه السلم) kama Mtume Muhammad (rehma na amani juu yake) Allah alimbarikia muujiza wa kulisimamisha jua. Ilikuwa ni siku ya Ijumaa katika nyakati za Alasiri wakati Yush'a aliliongoza Jeshi la Bani Israil dhidi ya maadui wa Allaah, mapigano yakaendelea mpaka jua likakaribia kutua, ambapo jua lingelitua Bani Israil wangelilazimika kuacha mapigano kwani ingeliisabiwa Jumamosi na wao hawakuruhusiwa kufanya kazi au shughuli kama vita katika siku ya Jumamosi. Ndipo Nabii Yush'a akamuomba Allaah (عز وجل) alisimamishe jua mpaka mapigano yatakapomalizika, na Allah akaipokea du'aa ya Nabii Yush'a. Mapigano haya yalikuwa ni ya kuikomboa Baytul Maqdis, na Allaah akalipa ushindi jeshi la Yush'a Bin Nuun (عليه السلم)

Mtume rehma na amani juu yake anasema "Yush'a aliliambia jua:

قال للشمس : انتى مأموره و انا مأمور , اللهم احبسها على شيأ 

 "Akasema kuliambia jua: Wewe unafuata amri na mimi nafuata amri, Ewe Allaah lisimamishe jua" 

Yush'a Bin Nuun aliuteka mji huu mtukufu akiwa na kizazi kipya. Mtume Muhammad rehma na amani juu yake anatueleza hakuna miongoni mwa wale waliobudu sanamu lilitongenezwa na Assamiriy alikuwemo kwenye jeshi la Yush'a bin Nuun lililokomboa Bayt al Maqdis. Akiwa Bayt al Maqdis Naabii Yush'a aliendelea kutawala kwa mafundisho ya Tawrat hadi mwisho wa maisha yake. Nabii Yush'a aliishi muda wa miaka 127. 

KIJANA ALIYEOMBA IDHINI YA KUZINI



Kijana mmoja alimwendea Mtume (rehma na amani ziwe juu yake) akamwambia: Ewe Mtume wa Allah, nipe idhini ya kuzini. Watu wakamzunguka na kuanza kumuonya. Vipi anaomba kuruhusiwa kufanya maasi na Mtume wa Mwenyezi Mungu? Mtume akawaambia: Hebu mleteni karibu yangu. Yule kijana akamsogelea Mtume (rehema na amani ziwe juu yake) akakaa.

Mtume akamuuliza: Je utaridhia zinaa kwa mama yako?
Kijana akajibu: Hapana  Wallahi.
Mtume akamwambia: vivyo hivyo na watu wengine hawaridhii kwa mama zao.

Mtume akamuuliza: je utaridhia kwa binti yako? 
Kijana akajibu: Hapana ewe mjumbe wa Allah.
Mtume akamwambia: na watu wengine hawaridhii kwa mabinti zao.

Mtume akamuuliza:Je utaridhia kwa dada yako?
Kijana akajibu: Hapana Wallahi.
Mtume akamwambia: na watu wengine hawaridhii kwa dada zao.

Mtume akamuuliza: Je utaridhia kwa shangazi yako?
Kijana akajibu: Hapana Wallahi.
Mtume akamwambia: na watu wengine hawaridhii kwa shangazi zao.

Mtume akamuuliza: Je utaridhia kwa Amma yako{Mama mdogo/mkubwa}?
Kijana akajibu: Hapana Wallahi.
Mtume akamwambia: na watu hawaridhii kwa Amma zao.

Kisha mtume akaweka mkono wake katika kifua cha kijana huyu na kumuombea dua:

<< اَللّهُمَّ اغْفِرْ ذَنْبَهُ، وَطَهِّرْ قَلْبَهُ، وَحَصِّنْ فَرْجَهُ >>


<< Ewe Allah msamehe madhambi yake, na utwaharishe moyo wake, na ikinge tupu yake. >>
Kijana akawa baada ya hapo hageuki kutizama chochote (miongoni mwa maasi)

MAZINGATIO TOKA KATIKA HADITHI